Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zekaria 14

14
Yerusalemu na watu wa mataifa mengine
1Tazama, siku ya ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu inakuja. Siku hiyo, enyi watu wa Yerusalemu, mali yenu itagawanywa mbele ya macho yenu. 2Mwenyezi-Mungu atayakusanya mataifa yote ili kuushambulia mji wa Yerusalemu. Mji utatekwa, nyumba zenu zitatekwa nyara, na wanawake wenu watanajisiwa. Nusu ya wakazi wa mji watapelekwa uhamishoni, lakini nusu itakayosalia haitachukuliwa nje ya mji. 3Kisha Mwenyezi-Mungu atatoka na kuyapiga vita mataifa hayo, kama afanyavyo daima siku za vita. 4Siku hiyo, atasimama kwenye mlima wa mizeituni ulio mashariki ya mji wa Yerusalemu. Mlima huo utagawanywa sehemu mbili na bonde pana sana litatokea toka mashariki hadi magharibi. Nusu moja itaelekea kaskazini na nusu nyingine kusini. 5Nyinyi mtakimbia kupitia bonde hilo, katikati ya milima miwili ya Mwenyezi-Mungu. Mtakimbia kama wazee wenu walivyokimbia tetemeko la ardhi wakati wa utawala wa mfalme Uzia wa Yuda. Kisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, atakuja na watakatifu wote pamoja naye.
6Wakati huo hakutakuwa baridi wala baridi kali.#14:6 baridi wala baridi kali: Maana katika Kiebrania si dhahiri. 7Mchana utaendelea bila giza kuingia. Wakati huo wajulikana kwa Mwenyezi-Mungu peke yake. Hakutakuwa mchana wala usiku, kwa maana hata saa za jioni mwanga utaendelea kuwapo.
8Wakati huo, maji ya uhai yatabubujika kutoka mji wa Yerusalemu, na nusu ya maji hayo yatatiririkia kwenye bahari ya mashariki, na nusu nyingine kwenye bahari ya magharibi. Maji hayo yataendelea kububujika wakati wa kiangazi kama yalivyo wakati wa masika.
9Wakati huo, Mwenyezi-Mungu atakuwa ndiye mfalme pekee wa dunia yote; naye atakuwa ndiye Mwenyezi-Mungu pekee, mmoja tu, na jina lake litakuwa ndilo jina pekee.
10Nchi yote, tangu Geba hadi Rimoni, kusini mwa Yerusalemu, itageuzwa kuwa mbuga tambarare kabisa. Lakini mji wa Yerusalemu utabaki juu mahali pake tokea lango la Benyamini mpaka lango la zamani, hadi kwenye lango la Konani, tangu mnara wa Hanareli hadi kwenye mashinikizo ya mfalme. 11Mji wa Yerusalemu utakaliwa na watu kwani ndani yake haitakuwapo laana tena; naam, watu watakaa humo kwa usalama.
12Lakini kuhusu wale watu ambao walikuja kupigana na Yerusalemu, haya ndiyo maafa ambayo Mwenyezi-Mungu atawaletea: Miili yao itaoza wangali hai; macho yao yataoza yakiwa kwenye matundu yake na ndimi zao zitaoza zikiwa vinywani mwao. 13Siku hiyo, hofu kutoka kwa Mwenyezi-Mungu itawakumba watu, na kila mtu atamshambulia mwenzake. 14Watu wa Yuda watapigana kuulinda mji wa Yerusalemu; utajiri wa mataifa yote yanayoizunguka nchi ya Yuda utakusanywa: Watakusanya dhahabu, fedha na mavazi kwa wingi sana. 15Maafa makubwa yatawakumba farasi, nyumbu, ngamia, punda na wanyama wote watakaokuwamo katika kambi hizo za maadui.
16Kisha, kila mtu aliyesalimika kati ya mataifa yote yaliyokuja kuushambulia mji wa Yerusalemu, atakuwa akija Yerusalemu mwaka hata mwaka, kumwabudu Mwenyezi-Mungu wa majeshi aliye mfalme, na kuadhimisha sikukuu ya vibanda. 17Iwapo taifa lolote duniani halitakwenda Yerusalemu kumwabudu Mwenyezi-Mungu wa majeshi aliye mfalme, basi, mvua haitanyesha katika nchi yao. 18Iwapo Wamisri watakataa kuiadhimisha sikukuu ya vibanda, basi, Mwenyezi-Mungu atawapiga kwa ugonjwa uleule atakaowapiga nao mataifa yote yanayokataa kuiadhimisha sikukuu hiyo. 19Hiyo itakuwa ndiyo adhabu itakayolipata taifa la Misri pamoja na mataifa yote yasiyoadhimisha sikukuu ya vibanda.
20Wakati huo, kwenye njuga za farasi yataandikwa maandishi haya: “Wakfu kwa Mwenyezi-Mungu Vyungu vilivyomo katika hekalu la Mwenyezi-Mungu vitakuwa kama mabakuli yaliyoko mbele ya madhabahu. 21Kila chungu katika mji wa Yerusalemu na nchi ya Yuda kitawekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ili wote wanaotoa tambiko waweze kuvichukua na kuchemshia nyama ya tambiko. Wakati huo, hakutakuwapo mfanya biashara yeyote katika hekalu la Mwenyezi-Mungu wa majeshi.

Iliyochaguliwa sasa

Zekaria 14: BHND

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia