Luka MT. 12
12
1HUKO nyuma mkutano wa watu, watu elfu nyingi walipokusanyika hatta wakakanyagana, akaanza kuwaambia wanafunzi wake khassa, Jihadharini na chachu ya Mafarisayo, yaani unafiki. 2Lakini hakuna neno lililofunikwa ambalo halitafunuliwa khalafu, wala lililostirika ambalo halitajulika khalafu. 3Bassi yo yote mliyoyasema gizani, yatasikiwa katika nuru: nalo mlilolisema katika sikio la mtu katika vyumba vya ndani litakhubiriwa juu darini. 4Lakini nawaambia ninyi rafiki zangu, Msiwaogope wao wauuao mwili na baada ya haya hawana neno la kutenda la zaidi. 5Illa nitawaonya mtakaemwogopa: Mwogopeni yule aliye na uweza baada ya kuua mtu kumtupa katika Jehannum: naam, nawaambieni, Mwogopeni yule. 6Haviuzwi videge vitano kwa pesa mbili? na hatta kimojawapo hakisahauliwi mbele ya Mungu: 7walakini hatta nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope bassi: ninyi bora kuliko videge vingi. 8Nami nawaambieni, Killa atakaenikiri mbele za watu, Mwana wa Adamu nae atamkiri mbele za malaika wa Mungu. 9Nae aliyenikana mbele ya watu, atakanwa mbele za malaika wa Mungu. 10Na killa mmoja atakaesema neno juu ya Mwana wa Adamu, atasamehewa, bali yeye aliyemtukana Roho Mtakatifu hatasamehewa. 11Na watakapowapeleka mbele za sunagogi na maliwali na wenye mamlaka, msifadhaike kwa kuwaza jinsi mtakavyojibu au mtakavyosema: 12kwa kuwa Roho Mtakatifu atawafundisha saa hiyo hiyo yawapasavyo kuyanena.
13Mtu mmoja katika makutano akamwambia, Mwalimu, mwambie ndugu yangu anigawie urithi wetu. 14Akamwambia, Ee mwana Adamu, nani aliyemweka kuwa kadhi au mgawanyi juu yenu? 15Akawaambia, Angalieni, jilindeni na kutamani, maana uzima wa mtu hautoki katika mali zake, kwa sababu ana wingi wa mali. 16Akawaambia mfano, akisema, Palikuwa na mtu tajiri, shamba lake likastawi. 17Akaanza kuwaza moyoni, akisema, Nifanyeje, maana sina pa kuweka akiba mavuno yangu? 18Akasema, Nitafanya hivi: nitavunja ghala zangu, nitajenga kubwa zaidi: na humo nitaweka akiba nafaka zangu zote, na mali zangu. 19Kiisha nitaiambia roho yangu, Ee roho yangu, nna mali nyingi ulizojiwekea akiba kwa miaka mingi: pumzika, hassi, ule, unywe, ufurahi. 20Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo, wanakutaka roho yako. Nayo uliyojiwekea tayari yatakuwa ya nani? 21Ndivyo alivyo yeye ajiwekeae nafsi yake akiba wala hawi tajiri machoni pa Mungu. 22Akawaambia wanafunzi wake, Kwa sababu hii nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mleni: wala miili yenu mvaeni. 23Kwa maana maisha ni zaidi ya chakula na mwili zaidi ya mavazi. 24Watafakarini kunguru, hawapandi wala hawavuni: hawana pa kuweka akiba wala ghala, na Mungu huwalisha. Ninyi si hora sana kuliko ndege? 25Yupi wenu awezae kwa kusumbuka kujiongeza kimo chake mkono mmoja? 26Bassi ikiwa hamwezi hatta neno lililo dogo, ya nini kujisumbulia mambo mengine? 27Yatafakarini maua jinsi yameavyo: hayatendi kazi wala hayasokoti, nami nawaambieni ya kwamba hatta Sulemani, katika fakhari yake yote hakuvikwa kama mojawapo la hayo. 28Bassi ikiwa Mungu huvika hivi haya majani ya kondeni yaliyopo leo, yakatupwa kalibuni kesho, si ninyi zaidi sana, enyi wa imani haba? 29Bassi ninyi msitafute mtakavyokula wala mtakavyokunywa, wala msiwe na roho yenye tashwishi. 30Maana mataifa wa dunia huyatafuta hayo yote, lakini Baba yenu anajua ya kuwa mnahitaji hayo. 31Bali utafuteni ufalme wa Mungu, na haya yote mtazidishiwa. 32Msiogope, enyi kundi dogo, kwa kuwa Baba yenu ameona vyema kuwapeni ufalme. 33Viuzeni mlivyo navyo, katoeni sadaka, jifanyieni mifuko isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, asikokaribia mwizi, wala nondo kuharibu. 34Kwa maana hazina yenu ilipo ndipo na itakapokuwa na mioyo yenu.
35Mwe, bassi, mmefungwa viuno, na taa zikiwaka; 36na ninyi kama watu wanaomngojea bwana wao, atakapoondoka arusini, illi akija na kubisha, wamfungulie marra moja. 37Wa kheri watumishi wale ambao bwana wao ajapo atawakuta wanakesba. Amin, nawaambieni, atajifunga, atawaketisha, atakuja kuwakhudumia. 38Na akija kesha la pili au akija kesha la tatu, na kuwakuta hivi, wa kheri watumishi wale. 39Lakini jueni haya ya kuwa mwenye nyumba angaliijua saa atakayokuja mwizi, angalikesha asiache nyumba yake kuvunjwa. 40Na ninyi, bassi, mwe tayari, kwa sababu saa msiyodhani, Mwana wa Adamu yuaja.
41Petro akasema, Bwana, unatuambia sisi mfano huu au watu wote pia? 42Bwana akasema, Nani, bassi, aliye wakili mwaminifu niwenye busara, ambae Bwana wake atamweka juu ya ntumishi wake wote, awape watu posho lao kwa saa yake? 43Yu kheri mtumishi yule ambae bwana wake ajapo atamkuta amefanya hivyo. 44Amin, nawaambieni, atamweka juu ya mali zake zote. 45Bali mtumwa yule akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia kuja; akaanza kuwapiga wajoli wake, wanaume na wanawake, na kula na kulewa; 46bassi, bwana wa mtumwa yule atakuja siku asiyodhani na saa asiyojua, atamkata vipande vipande, atampa sehemu yake pamoja na wasioamini. 47Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya Bwana wake, asijiweke tayari, wala kutenda mapenzi yake, atapigwa mapigo mengi; 48na yule asiyejua, nae amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa mapigo machache. Killa aliyepewa vingi kwake huyu vitatakwa vingi: nae waliyemkabidhi vingi, kwake yeye watataka vingi zaidi.
49Nimekuja kutupa moto duniani, na ukiwa umekwisha kuwashwa nataka nini zaidi? 50Nina ubatizo wa kubatizwa nao, na nina dhiiki namna gani hatta utakapotimizwa! 51Je! wadhani kwamba nimekuja niipe dunia amani? Nawaambieni, Sivyo, bali mafarakano. 52Kwa maana tangu sasa katika nyumba moja watakuwa watu watano wamefarakana, watatu na wawili, na wawili na watatu. 53Baba wa mtu atafarakana na mwanawe, na mwana na baba yake, mama ya mtu na binti yake, na binti na mama yake, mkwe mtu na mkwewe, mkwe na mkwe mtu.
54Akawaambia na makutano pia, Killa muonapo wingu likizuka magharibi, mwasema marra, Mvua inakuja. 55Na killa ivumapo kaskazi mwasema, Itakuwa joto; ikawa. 56Enyi wanafiki, mwajua kuufasiri uso wa inchi na mbingu; imekuwaje, bassi, hamjui kuyafasiri majira haya? 57Na mbona ninyi katika nafsi zenu hamwamui yaliyo haki?
58Bassi, unapofuatana na mshitaki wako kwenda kwa liwali, njiani ujitahidi kupatanishwa nae: asije akakukokota mbele ya kadhi, yule kadhi akakutia katika mikono ya askari, yule askari akakutupa gerezani. 59Nakuambia, Hutoki humo kabisa hatta uishe kulipa roho pesa ya mwisho.
Iliyochaguliwa sasa
Luka MT. 12: SWZZB1921
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.