Luka 17
17
Dhambi na Msamaha
(Mt 18:6-7,21-22; Mk 9:42)
1Yesu akawaambia wafuasi wake, “Mambo yanayosababisha watu kutenda dhambi yatatokea hakika. Lakini ole wake mtu anayesababisha hili litokee. 2Ingekuwa vizuri kwa mtu huyo kama jiwe la kusagia lingefungwa shingoni mwake, na akatupwa baharini, kuliko kusababisha mmojawapo wa wanyenyekevu hawa kutenda dhambi. 3Hivyo iweni waangalifu!
Ikiwa ndugu au dada yako katika familia ya Mungu akikukosea, umwonye. Akitubu, msamehe. 4Hata kama akikukosea mara saba katika siku moja, lakini akakuomba msamaha kila anapokukosea, msamehe.”
Imani Yako Ni Kubwa Kiasi Gani?
5Kisha mitume wakamwambia Bwana, “Tuongezee imani.”
6Bwana akasema, “Imani yenu ingekuwa kubwa kama mbegu ya haradali, mngeuambia mforosadi huu, ‘Ng'oka, ukajipandikize baharini,’ nao ungewatii.
Iweni Watumishi Wema
7Chukulia mmoja wenu ana mtumishi ambaye amekuwa shambani akilima au akichunga kondoo shambani. Akirudi kutoka shambani au machungani, utamwambia nini? Je! utamwambia, ‘Njoo ndani, keti, ule chakula’? 8Hapana! Utamwambia mtumishi wako, ‘Nitayarishie chakula nile. Jitayarishe na unihudumie. Nitakapomaliza kula na kunywa, ndipo utakula.’ 9Mtumishi asipewe shukrani maalumu kwa kufanya kazi yake. Anafanya kile alichoagizwa na mkuu wake. 10Vivyo hivyo nanyi. Mkimaliza kufanya yote mliyoamriwa kufanya, mseme, ‘Sisi ni watumwa, hatustahili shukrani yoyote maalumu. Tumefanya kazi tunayotakiwa kufanya.’”
Yesu Awaponya Baadhi ya Wayahudi na Msamaria
11Yesu alikuwa anasafiri kwenda Yerusalemu. Alipotoka Galilaya alisafiri akipita kando ya mpaka wa Samaria. 12Aliingia katika mji mdogo, na wanaume kumi walimwendea. Hawakumkaribia, kwa sababu wote walikuwa na ugonjwa uliogopewa sana wa ngozi. 13Lakini watu wale wakaita kwa kupaza sauti wakisema, “Yesu! Mkuu! Tafadhali utusaidie!”
14Yesu alipowaona, akasema, “Nendeni mkajioneshe kwa makuhani.”#17:14 mkajioneshe kwa makuhani Sheria ya Musa ilisema kwamba, kuhani ndiye anayeamua ikiwa mtu mwenye ugonjwa hatari wa ngozi amepona ugonjwa hatari wa ngozi wake.
Wale watu kumi walipokuwa wanakwenda kujionesha kwa makuhani, waliponywa. 15Mmoja wao alipoona kuwa amepona, alirudi kwa Yesu huku akimsifu Mungu kwa kupaza sauti. 16Akaanguka kifudifudi miguuni pa Yesu, akamshukuru. (Alikuwa Msamaria.) 17Yesu akasema, “Watu kumi wameponywa, wengine tisa wako wapi? 18Mtu huyu wala si mmoja wa watu wetu. Ni yeye peke yake aliyerudi kumsifu Mungu?” 19Ndipo Yesu akamwambia, “Inuka! Unaweza kwenda. Umeponywa kwa sababu uliamini.”
Kuja Kwa Ufalme Wa Mungu
(Mt 24:23-28,37-41)
20Baadhi ya Mafarisayo walimuuliza Yesu, “Ufalme wa Mungu utakuja lini?” Yesu akajibu, “Kuja kwa ufalme wa Mungu si kitu unachoweza kuona. 21Watu hawatasema, ‘Tazama ufalme wa Mungu uko hapa’ au ‘Ule pale!’ Hapana, Ufalme wa Mungu upo hapa pamoja nanyi.”#17:21 Mungu upo hapa pamoja nanyi Au “umo ndani yenu”.
22Kisha Yesu akawaambia wafuasi wake, “Wakati utakuja, ambapo mtatamani angalau kuwa na Mwana wa Adamu hata kwa siku moja, lakini hamtaweza. 23Watu watawaambia, ‘Tazameni, yuko kule!’ au ‘Tazameni, yuko hapa!’ Kaeni pale mlipo; msitoke kwenda kumtafuta. 24Iweni na subira kwa sababu Mwana wa Adamu atakaporudi, mtatambua. Siku hiyo atang'aa kama mwanga wa radi umulikavyo angani kutoka upande mmoja hadi mwingine. 25Lakini kwanza, ni lazima Mwana wa Adamu ateseke kwa mambo mengi na watu wa leo watamkataa.
26Mwana wa Adamu atakaporudi, itakuwa kama ilivyokuwa Nuhu alipoishi. 27Watu walikuwa wakila, wakinywa, wakioa na kuolewa hata siku Nuhu alipoingia katika safina. Ndipo gharika ilikuja na kuwaangamiza wote.
28Ilikuwa vivyo hivyo katika wakati wa Lutu, Mungu alipoteketeza Sodoma. Watu wa Sodoma walikuwa wakila, wakinywa, wakinunua, wakiuza, wakipanda na kujijengea nyumba. 29Lakini siku ambayo Lutu alitoka Sodoma, moto na baruti vilinyesha kutoka mbinguni na kuwaua wote. 30Hivi ndivyo itakavyokuwa siku ambayo Mwana wa Adamu atarudi.
31Siku hiyo, ikiwa mtu atakuwa juu ya paa ya nyumba yake, hatakuwa na muda wa kushuka kwenda ndani ya nyumba kuchukua vitu vyake. Ikiwa atakuwa shambani, hataweza kurudi nyumbani. 32Kumbukeni yaliyompata mke wa Lutu!#17:32 mke wa Lutu Simulizi kuhusu mke wa Lutu inapatikana katika Mwa 19:15-17,26.
33Kila atakayejaribu kutunza maisha aliyonayo atayaangamiza. Lakini yeyote atakayeyasalimisha maisha yake atayaokoa. 34Usiku ule watu wawili wataweza kuwa wamelala katika chumba kimoja, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa. 35Wanawake wawili watakuwa wanasaga nafaka pamoja, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.” 36#17:36 Nakala chache za Kiyunani zimeongeza mstari wa 36: “Watu wawili watakuwa shambani, mmoja atachukuliwa, mwingine ataachwa.”
37Wafuasi wake wakamuuliza, “Hii itakuwa wapi Bwana?”
Yesu akajibu, “Ni kama kuutafuta mzoga, utaupata pale ambapo tai wamekusanyika.”
Iliyochaguliwa sasa
Luka 17: TKU
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International