Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 16

16
Utajiri Halisi
1Yesu aliwaambia wafuasi wake, “Alikuwepo mtu mmoja tajiri, aliyekuwa na msimamizi wa kuangalia biashara zake. Baadaye akagundua kuwa msimamizi wake alikuwa anapoteza pesa zake. 2Hivyo, akamwita, akamwambia, ‘Nimesikia mambo mabaya juu yako. Nipe taarifa namna ulivyosimamia pesa zangu. Huwezi kuendelea kuwa msimamizi wangu.’
3Hivyo msimamizi akawaza moyoni mwaka, ‘Nitafanya nini? Bwana wangu ananiachisha kazi yangu ya usimamizi. Sina nguvu za kulima, kuomba omba naona aibu. 4Najua nitakalofanya! Nitafanya kitu nipate marafiki. Ili nitakapopoteza kazi yangu, watanikaribisha katika nyumba zao.’
5Hivyo msimamizi akawaita mmoja mmoja wale waliokuwa wanadaiwa pesa na bwana wake. Akamwuliza wa kwanza, ‘Mkuu wangu anakudai kiasi gani?’ 6Akamjibu, ‘Ananidai mitungi#16:6 mitungi Kiyunani batous, kutoka kwa Kiebrania bath, sawa na galoni 8 au lita 34. 100 ya mafuta ya zeituni.’ Msimamizi akamwambia, ‘Chukua hati yako ya deni, kaa chini, fanya haraka, badilisha iwe mitungi hamsini.’
7Kisha akamwambia mwingine, ‘Na wewe kiasi gani unadaiwa?’ Akajibu, ‘Vipimo#16:7 Vipimo Kiyunani korous, kutoka kwa Kiebrania cor, kipimo sawa kama galoni 89 au lita 390. mia moja vya ngano.’ Akamwambia, ‘Chukua hati yako ya deni, ibadilishe iwe vipimo themanini.’
8Baadaye bwana wake akamsifu msimamizi asiye mwaminifu kwa sababu ya kutenda kwa busara. Ndiyo, watu wa ulimwengu huu wana busara katika kufanya biashara kati yao kuliko wana wa Mungu.
9Ninamaanisha hivi: Vitumieni vitu vya kidunia mlivyonavyo sasa ili muwe na ‘marafiki’ kwa ajili ya siku za baadaye. Ili wakati vitu hivyo vitakapotoweka, mtakaribishwa katika nyumba ya milele. 10Mtu yeyote anayeweza kuaminiwa kwa mambo madogo anaweza kuaminiwa kwa mambo makubwa pia. Mtu asiye mwaminifu katika jambo dogo hawezi kuwa mwaminifu katika jambo kubwa. 11Ikiwa huwezi kuaminiwa kwa mali za kidunia, huwezi kuaminiwa kwa mali za mbinguni. 12Na kama hauwezi kuaminiwa kwa vitu vya mtu mwingine, hautapewa vitu kwa ajili yako wewe mwenyewe.
13Mtumwa hawezi kuwatumikia mabwana wawili wakati mmoja, hata ninyi hamwezi. Utamchukia mmoja na kumpenda mwingine, au utakuwa mwaminifu kwa mmoja na hautamjali mwingine. Pia, huwezi kumtumikia Mungu na pesa.”#16:13 pesa Au “mamona”, neno la Kiaramu linalomaanisha “utajiri”.
Sheria Ya Mungu Haiwezi Kubadilishwa
(Mt 11:12-13)
14Mafarisayo walikuwa wakiyasikiliza mambo haya yote. Walimdhihaki Yesu kwa sababu wote walipenda pesa. 15Yesu aliwaambia, “Mnajifanya kuwa wenye haki mbele za watu, lakini Mungu anajua hakika kilichomo mioyoni mwenu. Jambo ambalo watu hudhani kuwa la muhimu, kwa Mungu ni chukizo.
16Kabla ya Yohana Mbatizaji kuja, watu walifundishwa Sheria ya Musa na maandishi ya Manabii. Lakini tangu wakati wa Yohana, Habari Njema kuhusu ufalme wa Mungu inahubiriwa. Na kila mtu anajitahidi sana ili kuingia katika ufalme wa Mungu. 17Ni rahisi sana kwa mbingu na dunia kutoweka, kuliko sehemu ndogo ya herufi katika Sheria ya Musa kutoweka. 18Mwanaume yeyote anayemtaliki mkewe na kumwoa mke mwingine anazini. Na mwanaume anayeoa mwanamke aliyetalikiwa anazini pia.”
Tajiri na Lazaro
19Yesu akasema, “Alikuwepo mtu mmoja, tajiri ambaye daima alivaa nguo za thamani sana, alikuwa tajiri sana kiasi kwamba alifurahia vitu vizuri kila siku. 20Alikuwepo pia maskini mmoja aliyeitwa Lazaro ambaye mwili wake ulikuwa umejaa vidonda. Mara nyingi aliwekwa kwenye lango la tajiri. 21Lazaro alitaka tu kula masalia ya vyakula vilivyokuwa sakafuni vilivyodondoka kutoka mezani kwa tajiri. Na mbwa walikuja na kulamba vidonda vyake.
22Baadaye Lazaro alikufa. Malaika walimchukua na kumweka kifuani pa Abrahamu. Tajiri naye alikufa na kuzikwa. 23Alichukuliwa mpaka mahali pa mauti#16:23 mahali pa mauti Kwa maana ya kawaida, “Kuzimu”. na akawa katika maumivu makuu. Alimwona Abrahamu kwa mbali na Lazaro akiwa kifuani pake. 24Akaita, ‘Baba Abrahamu, nihurumie! Mtume Lazaro kwangu ili achovye ncha ya kidole chake kwenye maji na kuupoza ulimi wangu, kwa sababu ninateseka katika moto huu!’
25Lakini Abrahamu akamjibu, ‘Mwanangu, unakumbuka ulipokuwa unaishi? Ulikuwa na mambo yote mazuri katika maisha. Lakini Lazaro hakuwa na chochote ila matatizo. Sasa yeye anafarijiwa hapa, na wewe unateseka. 26Pia kuna korongo pana na lenye kina kati yetu sisi na ninyi. Hakuna anayeweza kuvuka kuja kukusaidia na hakuna anayeweza kuja huku kutoka huko.’
27Tajiri akasema, ‘Basi, nakuomba baba, mtume Lazaro nyumbani kwa baba yangu duniani, 28Nina ndugu watano. Mtume ili akawape tahadhari wasije wakafika mahali hapa pa mateso.’
29Lakini Abrahamu akasema, ‘Wanayo Sheria ya Musa na maandishi ya manabii kwa ajili ya kuyasoma; wasikilize na kutii.’
30Tajiri akasema, ‘Hapana Baba Abrahamu! Lakini ikiwa mtu kutoka kwa wafu akiwaendea ndipo wataamua kutubu na kubadili maisha yao.’
31Lakini Abrahamu akamwambia, ‘Ikiwa ndugu zako hawatawasikiliza Musa na manabii, hawataweza kumsikiliza mtu yeyote kutoka kwa wafu.’”

Iliyochaguliwa sasa

Luka 16: TKU

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia