Yohana 17
17
Yesu Aomba Kwa ajili Yake na Wafuasi Wake
1Baada ya Yesu kusema maneno hayo, alitazama mbinguni na kuomba, “Baba, wakati umefika. Mpe utukufu Mwanao ili Mwanao naye akupe wewe utukufu. 2Ulimpa Mwana mamlaka juu ya watu wote ili awape uzima wa milele wale wote uliompa. 3Na uzima wa milele ndiyo huu: kwamba watu watakujua wewe, Mungu pekee wa kweli, na kwamba watamjua Yesu Kristo, Yeye uliyemtuma. 4Mimi nimeimaliza kazi uliyonipa niifanye. Nami nimekupa utukufu duniani. 5Sasa, Bwana, unipe utukufu wako niwe nao pamoja nawe, utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya kuumbwa ulimwengu.
6Wewe ulinipa baadhi ya wafuasi kutoka watu wa ulimwengu huu. Hao nimewaonesha jinsi wewe ulivyo. Walikuwa watu wako, lakini ukawakabidhi kwangu. Wao wameyashika mafundisho yako. 7Sasa wanajua kuwa kila kitu nilichonacho kimetoka kwako. 8Mimi niliwaeleza maneno uliyonipa, nao wakayapokea. Walitambua ukweli kuwa mimi nilitoka kwako na wakaamini kuwa wewe ndiye uliyenituma. 9Mimi ninawaombea hao sasa. Siwaombei watu walioko ulimwenguni. Bali nawaombea wale watu ulionipa, kwa sababu hao ni wako. 10Vyote nilivyo navyo ni vyako, na vyote ulivyo navyo ni vyangu. Kisha utukufu wangu umeonekana ndani yao.
11Sasa nakuja kwako. Mimi sitakaa ulimwenguni, lakini hawa wafuasi wangu bado wamo ulimwenguni. Baba Mtakatifu, uwaweke hao salama kwa nguvu ya jina lako ulilonipa. Ndipo watapokuwa na umoja, kama vile mimi na wewe tulivyo. 12Nilipokuwa pamoja nao niliwaweka salama kwa nguvu ya jina lako ulilonipa. Niliwalinda. Ni mmoja wao tu aliyepotea; yule ambaye kwa hakika angelikuja kupotea. Hii ilikuwa hivyo ili kuonesha ukweli wa yale yaliyosemwa na Maandiko kuwa yangetokea.
13Nami nakuja kwako sasa. Lakini maneno haya nayasema ningali nimo ulimwenguni ili wafuasi hawa wawe na furaha kamili ndani yao. 14Nimewapa mafundisho yako. Nao ulimwengu umewachukia, kwa sababu wao sio wa ulimwengu, kama mimi nisivyokuwa wa ulimwengu.
15Siombi kwamba uwaondoe katika ulimwengu. Bali ninaomba uwalinde salama kutoka kwa Yule Mwovu.#17:15 Mwovu Ni Shetani au Ibilisi. 16Wao si wa ulimwengu huu, kama mimi nisivyokuwa wa ulimwengu huu. 17Kupitia kweli yako uwatayarishe kwa utumishi wako. Mafundisho yako ndiyo kweli. 18Mimi nimewatuma ulimwenguni, kama wewe ulivyonituma mimi ulimwenguni. 19Nami najiweka tayari kabisa kukutumikia wewe. Ninafanya hivi kwa ajili yao ili wao nao wawe wamekamilika kukutumikia.
20Siwaombei tu hao wafuasi wangu lakini nawaombea pia wale watakaoniamini kutokana na mafundisho yao. 21Baba, naomba kwamba wote wanaoniamini waungane pamoja na kuwa na umoja. Wawe na umoja kama vile wewe na mimi tulivyoungana; wewe umo ndani yangu nami nimo ndani yako. Nami naomba nao pia waungane na kuwa na umoja ndani yetu. Ndipo ulimwengu nao utaamini kuwa ndiwe uliyenituma. 22Mimi nimewapa utukufu ule ulionipa. Nimewapa utukufu huo ili wawe na umoja, kama mimi na wewe tulivyo na umoja. 23Nitakuwa ndani yao, nawe utakuwa ndani yangu. Hivyo watakuwa na umoja kamili. Kisha ulimwengu utajua kwamba wewe ndiwe uliyenituma na ya kuwa uliwapenda jinsi ulivyonipenda mimi.
24Baba, ninataka hawa watu ulionipa wawe nami mahali pale nitakapokuwa. Nataka wauone utukufu wangu, utukufu ule ulionipa kwa sababu ulinipenda kabla ulimwengu haujaumbwa. 25Baba wewe ndiye unayetenda yaliyo haki. Ulimwengu haukujui, bali mimi nakujua, na hawa wafuasi wangu wanajua kuwa wewe ndiye uliyenituma. 26Nimewaonesha jinsi ulivyo, na nitawaonesha tena. Kisha watakuwa na upendo ule ule ulio nao wewe kwangu, nami nitaishi ndani yao.”
Iliyochaguliwa sasa
Yohana 17: TKU
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International