Yohana 16
16
1Nimewaambia mambo haya yote ili msipoteze imani mtakapokutana na matatizo. 2Watu watawafukuza mtoke katika masinagogi#16:2 masinagogi Maeneo katika miji mingi ambako Wayahudi walikusanyika kwa ajili ya sala, kujifunza Maandiko, na mikutano mingine ya wote. Sinagogi ni nyumba ya ibada. na msirudi humo tena. Hakika, unakuja wakati watapofikiri kuwa kwa kuwaua ninyi watakuwa wanatoa huduma kwa Mungu. 3Watafanya hivyo kwa sababu hawajamjua Baba, na hawajanijua mimi pia. 4Nimewaambia haya sasa ili kuwaandaa. Hivyo wakati wa mambo haya kutimia utakapofika, mtakumbuka kwamba niliwapa tahadhari mapema.
Kazi za Roho Mtakatifu
Sikuwaambia mambo haya tangu mwanzo, kwa sababu bado nilikuwa pamoja nanyi. 5Sasa narudi kwake yeye aliyenituma, ingawa hakuna hata mmoja wenu anayeniuliza, ‘Unakwenda wapi?’ 6Nanyi mmejawa na huzuni kwa vile nimewaambia mambo haya yote. 7Hakika nawaambieni, ni kwa faida yenu mimi nikiondoka. Nasema hivi kwa sababu, nitakapoondoka nitamtuma kwenu Msaidizi. Lakini nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja.
8Ila huyo Msaidizi atakapokuja, atawaonesha watu wa ulimwengu jinsi walivyofanya dhambi. Atawaonesha nani ana hatia ya dhambi, nani ana haki mbele za Mungu, na nani anastahili kuhukumiwa na Mungu. 9Huyo Msaidizi atawaonesha kuwa wana hatia ya dhambi kwa sababu hawaniamini mimi. 10Atawaonesha jinsi wasivyoelewa mtu anavyohesabiwa haki na Mungu. Hakika mimi nina kibali kwa sababu naenda kwa Baba nanyi hamtaniona tena. 11Naye atawaonesha watu wa ulimwengu huu jinsi hukumu yao isivyo sahihi, kwa sababu mkuu wao ulimwenguni#16:11 mkuu wao ulimwenguni Kwa maana ya kawaida, “mkuu wa ulimwengu huu”, ina maana ya Shetani. Ni sawa na kusema “kiongozi wao mkuu Ulimwenguni”. Tazama Shetani katika Orodha ya Maneno. amekwisha hukumiwa.
12Ninayo mambo mengi ya kuwaeleza, lakini ni magumu kwenu kuyapokea kwa sasa. 13Hata hivyo atakapokuja huyo Roho wa kweli, Yeye atawaongoza hadi kwenye kweli yote. Hatasema maneno yake mwenyewe bali atayasema yale tu anayosikia na atawajulisha yale yatakayotokea baadaye. 14Roho wa kweli atanipa mimi utukufu kwa kuwaeleza ninyi yote aliyopokea kutoka kwangu. 15Yote aliyonayo Baba ni yangu pia. Ndiyo sababu nilisema kwamba Roho atawaeleza yote anayopokea kutoka kwangu.
Huzuni Itageuzwa Kuwa Furaha
16Baada ya kipindi kifupi hamtaniona. Kisha baada ya kipindi kingine kifupi mtaniona tena.”
17Baadhi ya wafuasi wake wakaambiana wao kwa wao, “Ana maana gani anaposema, ‘Baada ya kipindi kifupi hamtaniona tena. Kisha baada ya kipindi kifupi kingine mtaniona tena?’ Tena ana maana gani anaposema, ‘Kwa sababu naenda kwa Baba’?” 18Wakauliza pia, “Ana maana gani anaposema ‘Kipindi kifupi’? Sisi hatuelewi anayosema.” 19Yesu alitambua kuwa wafuasi wake walitaka kumwuliza juu ya jambo hilo. Hivyo akawaambia, “Je! mnaulizana ninyi kwa ninyi kwamba nilikuwa na maana gani niliposema, ‘Baada ya kipindi kifupi hamtaniona. Kisha baada ya kipindi kifupi kingine mtaniona tena’? 20Hakika nawaambia, ninyi mtapata huzuni na kulia, bali ulimwengu utakuwa na furaha. Ndio, mtapata huzuni, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha.
21Mwanamke anapojifungua mtoto, hupata maumivu, kwa sababu wakati wake umefika. Lakini baada ya mtoto kuzaliwa, huyasahau maumivu yale. Husahau kwa sababu huwa na furaha kwa kuwa mtoto amezaliwa ulimwenguni. 22Ndivyo ilivyo hata kwenu pia. Sasa mna huzuni lakini nitawaona tena, nanyi mtafurahi. Mtakuwa na furaha ambayo hakuna mtu atakayewaondolea. 23Katika siku hiyo, hamtapaswa kuniuliza mimi kitu chochote. Nami kwa hakika nawaambia, Baba yangu atawapa lo lote mtakalomwomba kwa jina langu. 24Hamjawahi kuomba lo lote kwa namna hii hapo awali. Bali ombeni kwa jina langu nanyi mtapewa. Kisha mtakuwa na furaha iliyotimia ndani yenu.
Ushindi Dhidi ya Ulimwengu
25Nimewaambia mambo haya kwa kutumia maneno yenye mafumbo. Isipokuwa utakuja wakati ambapo sitatumia tena maneno ya jinsi hiyo kuwaeleza mambo. Nami nitasema nanyi kwa maneno ya wazi wazi juu ya Baba. 26Kisha, mtaweza kumwomba Baba vitu kwa jina langu. Sisemi kwamba nitapaswa kumwomba Baba kwa ajili yenu. 27Baba mwenyewe anawapenda kwa sababu ninyi mmenipenda mimi. Naye anawapenda kwa sababu mmeamini kwamba nimetoka kwa Mungu. 28Mimi nimetoka kwa Baba kuja ulimwenguni. Sasa naondoka ulimwenguni na kurudi kwa Baba.”
29Kisha wafuasi wake wakasema, “Tayari unaongea nasi wazi wazi. Hutumii tena maneno yanayoficha maana. 30Sasa tunatambua kuwa unajua mambo yote. Wewe unajibu maswali yetu hata kabla hatujayauliza. Hii inatufanya tuamini kwamba ulitoka kwa Mungu.”
31Yesu akasema, “Kwa hiyo sasa mnaamini? 32Basi nisikilizeni! Wakati unakuja mtakapotawanywa, kila mmoja nyumbani kwake. Kwa hakika, wakati huo tayari umekwisha fika. Ninyi mtaniacha, nami nitabaki peke yangu. Lakini kamwe mimi siko peke yangu, kwa sababu Baba yupo pamoja nami.
33Nimewaambia mambo haya ili muwe na amani ndani yangu. Katika ulimwengu huu mtapata mateso. Lakini muwe jasiri! Mimi nimeushinda ulimwengu!”
Iliyochaguliwa sasa
Yohana 16: TKU
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International