Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 11

11
Yesu anafundisha juu ya kusali
(Mat 6:9-13; 7:7-11)
1Siku moja, Yesu alikuwa mahali fulani akisali. Alipomaliza kusali, mmoja wa wanafunzi wake akamwambia, “Bwana, tunakuomba utufundishe kusali kama Yohane Mbatizaji alivyowafundisha wanafunzi wake.”#11:1 Yohane Mbatizaji… wanafunzi wake: Hao wanatajwa mara kadhaa katika Injili (taz Mat 9:14; Yoh 1:35; 3:25). 2Yesu akawaambia, “Mnaposali, semeni:
‘Baba!#11:2 Baba: Uhusiano wa ndani kabisa ambao unaoneshwa hapa ni ule wa neno la Kiaramu “aba” ambalo watoto walilitumia kwa baba zao.
Jina lako litukuzwe;#11:2 Jina lako litukuzwe: Hapa ombi ni kwamba Mungu mwenyewe (Jina lako) adhihirishe utakatifu na uwezo wake au nguvu yake kati ya watu kwa namna ambayo wote wataweza kumtambua kama Mungu.
ufalme wako ufike.
3Utupe daima chakula chetu cha kila siku.#11:3 Cha kila siku: Au: kwa kesho.
4Utusamehe dhambi zetu,
maana sisi tunawasamehe wote waliotukosea;
wala usitutie katika majaribu.’”#11:4 Majaribu: Hapa yawezekana pia kutumia neno kishawishi.
5Kisha akawaambia, “Tuseme mmoja wenu anaye rafiki, akaenda kwake usiku wa manane, akamwambia: ‘Rafiki, tafadhali niazime mikate mitatu,#11:5-10 Mifano hiyo miwili juu ya dhamira ya sala inatokea tu katika Luka (taz maelezo ya Luka 3:21 na pia linganisha Luka 18:1-8). 6kwa kuwa rafiki yangu amepitia kwangu akiwa safarini nami sina cha kumpa.’ 7Naye, akiwa ndani angemjibu: ‘Usinisumbue! Nimekwisha funga mlango. Mimi na watoto wangu tumelala; siwezi kuamka nikupe!’ 8Hakika, ingawa hataamka ampe kwa sababu yeye ni rafiki yake, lakini, kwa sababu ya huyo mtu kuendelea kumwomba, ataamka ampe chochote anachohitaji. 9Kwa hiyo, ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtapata; bisheni mlango nanyi mtafunguliwa. 10Maana yeyote aombaye hupewa, atafutaye hupata na abishaye mlango hufunguliwa. 11Mtoto akimwomba baba yake samaki, je, atampa nyoka badala ya samaki?#11:11 Baadhi ya hati za mkono za kale huongeza hapa: mkate atampa jiwe; au, akiomba. 12Na kama akimwomba yai, je, atampa nge? 13Kama nyinyi, ingawa ni waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, hakika baba yenu wa mbinguni atafanya zaidi; atawapa Roho Mtakatifu#11:13 Roho Mtakatifu: Mathayo ana: Mema; lakini Luka hapa anataja Roho Mtakatifu ambaye ni zawadi kuu kuliko zote kama anavyooneshaonesha katika kitabu chake cha pili, yaani Matendo ya Mitume. wale wanaomwomba.”
Yesu na Beelzebuli
(Mat 12:22-30; Marko 3:20-27)
14Siku moja Yesu alikuwa anamfukuza pepo aliyemfanya mtu mmoja kuwa bubu. Basi, huyo pepo alipomtoka, yule mtu akaweza kuongea, hata umati wa watu ukashangaa. 15Lakini baadhi ya watu hao wakasema, “Anawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli,#11:15 Beelzebuli: Tazama Mat 10:25. Jina la kumtaja pepo mbaya aliyekuwa kiongozi wa pepo wote wabaya, na ambalo limetokana na Kiebrania: “Baal-zebubu” (2Fal 1:2-3) ambalo ni jina la dharau lenye maana ya “Bwana wa nzi”, na ambalo Wayahudi walilitumia kumtaja mungu wa Wakaanani aitwaye Baali. mkuu wa pepo.” 16Wengine, wakimjaribu, wakamtaka afanye ishara kuonesha kama alikuwa na idhini kutoka mbinguni. 17Lakini yeye, akiwa anayajua mawazo yao, akawaambia, “Ufalme wowote uliogawanyika vikundi vinavyopingana hauwezi kudumu; kadhalika, jamaa yoyote iliyo na mafarakano huangamia. 18Kama Shetani anajipinga mwenyewe, utawala wake utasimamaje? Mnasemaje, basi, kwamba ninawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli? 19Kama ninafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, wafuasi wenu huwafukuza kwa uwezo wa nani? Kwa sababu hiyo, wao ndio watakaowahukumu nyinyi. 20Lakini ikiwa ninafukuza pepo kwa uwezo wa Mungu,#11:20 Uwezo wa Mungu: Neno kwa neno: kidole cha Mungu, kwa maana ya kuhusika kwa namna ya pekee kwa Mungu na uwezo wake. Ling na Kut 8:19. basi jueni kwamba ufalme wa Mungu umekwisha fika kwenu.
21“Mtu mwenye nguvu anapolinda jumba lake kwa silaha, mali yake yote iko salama. 22Lakini akija mwenye nguvu zaidi akamshambulia na kumshinda, huyo huziteka silaha zake alizotegemea na kugawanya nyara. 23Yeyote asiyejiunga nami, ananipinga; na yeyote asiyekusanya pamoja nami, hutawanya.
Kurudi kwa pepo mbaya
(Mat 12:43-45)
24“Pepo mchafu akifukuzwa kwa mtu, huzururazurura jangwani kukavu akitafuta mahali pa kupumzika. Asipopata, hujisemea: ‘Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka.’ 25Anaporudi, huikuta ile nyumba imefagiwa na kupambwa. 26Basi, huenda na kuwachukua pepo wengine saba wabaya kuliko yeye; wote huenda, wakamwingia mtu huyo. Hivyo, hali ya mtu huyo sasa huwa mbaya zaidi kuliko hapo mwanzo.”
Furaha ya kweli
27Alipokuwa akisema hayo, mwanamke mmoja katika lile kundi la watu, akasema kwa sauti kubwa: “Heri mwanamke aliyekuzaa na kukunyonyesha!” 28Lakini Yesu akasema, “Lakini heri zaidi wale wanaolisikia neno la Mungu na kulishika.”
Wanataka ishara
(Mat 12:38-42)
29Umati wa watu ulipozidi kuongezeka, Yesu akawaambia, “Kizazi hiki ni kizazi kiovu. Kinataka ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ile ishara ya Yona.#11:29-30 Yona: Yona alitumwa na Mungu kwa watu wa Ninewi lakini mara ya kwanza alikwepa. Mara ya pili, alipokwishakaa tumboni mwa samaki kwa siku tatu, alitemwa na yule samaki, akaenda kuwahubiria watu wa Ninewi. Yesu kwa kutaja kisa cha Yona cha kukaa tumboni mwa samaki siku tatu na kukilinganisha na muda atakaotumia kaburini (Luka 23:50-24:12). Ninewi: tazama Mat 12:41. Ninewi ulikuwa mji mkuu wa kale wa Ashuru, mashariki mwa mto Tigri. 30Jinsi Yona alivyokuwa ishara kwa watu wa Ninewi, ndivyo pia Mwana wa Mtu atakavyokuwa ishara kwa kizazi hiki. 31Malkia wa kusini#11:31 Malkia wa kusini: Yahusu malkia wa Sheba, eno linalofikiriwa kuwa mahali fulani katika Afrika ya kaskazini au hata sehemu ya kusini ya Arabia. atatokea wakati kizazi hiki kitakapohukumiwa, naye atakihukumu kwamba kina hatia. Maana yeye alisafiri kutoka mbali, akaja kusikiliza maneno ya hekima ya Solomoni#11:31 Solomoni: Taz 1Fal 10:1-10. na kumbe hapa pana mkuu kuliko Solomoni. 32Watu wa Ninewi watatokea wakati wa hukumu, nao watakihukumu kizazi hiki kwamba kina hatia. Maana Waninewi walitubu kwa sababu ya mahubiri ya Yona; na kumbe hapa pana kikuu kuliko Yona!
Mwanga wa mwili
(Mat 5:15; 6:22-23)
33“Hakuna mtu anayewasha taa na kuifunika kwa debe, bali huiweka juu ya kinara ili watu wanaoingia ndani wapate kuona mwanga. 34Jicho lako ni taa ya mwili wako; likiwa zima, mwili wako wote utakuwa katika mwanga. Jicho lako likiwa bovu, na mwili wako pia utakuwa katika giza.#11:34 Kuhusu jicho zima na jicho bovu tazama Mat 6:22-23. Yamkini yahusika hapa macho mema (au mabaya) ambayo yanapokea (au kukataa kupokea) mwangaza wa Injili. 35Uwe mwangalifu basi, mwanga ulio ndani yako usije ukawa giza. 36Basi, kama mwili wako wote una mwanga, bila kuwa na sehemu yoyote yenye giza, mwili huo utang'aa kikamilifu kama vile taa inavyokuangazia kwa mwanga wake.”
Yesu anawalaumu Mafarisayo na waalimu wa sheria
(Mat 23:1-36; Marko 12:38-40)
37Yesu alipokuwa akiongea, Mfarisayo mmoja alimkaribisha chakula nyumbani kwake, naye akaenda, akaketi kula chakula. 38Huyo Mfarisayo alistaajabu kuona kwamba alikula chakula bila kunawa kwanza.#11:38 Mat 15:1-2; Marko 7:1-2. Hapa yahusu desturi za jadi za Wayahudi kuhusu kutawadha kidini. Ling na Marko 7:2-4. 39Bwana akamwambia, “Nyinyi Mafarisayo huosha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa udhalimu na uovu. 40Wapumbavu nyinyi! Je, aliyetengeneza nje si ndiye aliyetengeneza ndani pia? 41Toeni kwa maskini vile vitu vilivyomo#11:41 Toeni kwa maskini vile vitu vilivyomo: Tafsiri nyingine yamkini: Toeni kutoka kwa kile mnachoweza, au kile kilicho ndani (yaani moyoni). ndani, na vingine vyote vitakuwa halali kwenu.
42“Lakini ole wenu Mafarisayo, kwa sababu mnatoza watu zaka hata juu ya majani ya kukolezea chakula, mchicha na majani mengine, na huku hamjali juu ya haki na upendo kwa Mungu. Mambo haya iliwapasa muwe mmeyazingatia bila kuyasahau yale mengine.#11:42 Lawi 27:30; Amo 5:21-24; Mika 6:8. Desturi ya kutoa zaka sehemu moja ya kumi ya vitu vya thamani ndogo ilitiliwa mkazo sana na waalimu wa sheria.
43“Ole wenu nyinyi Mafarisayo, kwa sababu mnapenda kuketi mbele mahali pa heshima katika masunagogi, na kusalimiwa kwa heshima hadharani. 44Ole wenu, kwa sababu mko kama makaburi yaliyofichika; watu hutembea juu yake bila kufahamu.”#11:44 Mtu aliyegusa kaburi alikuwa najisi kidini (Hes 19:16). Taz Mat 23:27 ambapo makaburi yasemekana yalipakwa chokaa bila shaka kusudi kutahadharisha watu wasije kuyagusa na kuwa najisi.
45Mmoja wa waalimu wa sheria akamwambia, “Mwalimu, maneno yako yanatukashifu na sisi pia.” 46Yesu akamjibu, “Na nyinyi waalimu wa sheria, ole wenu; maana mnawatwika watu mizigo isiyochukulika, huku nyinyi wenyewe hamnyoshi hata kidole kuwasaidia. 47Ole wenu, kwa kuwa mnajenga makaburi ya manabii wale ambao wazee wenu waliwaua. 48Kwa hiyo mnashuhudia na kukubaliana na matendo ya wazee wenu; maana wao waliwaua hao manabii, nanyi mnajenga makaburi yao. 49Kwa hiyo, Hekima ya Mungu ilisema hivi: ‘Nitawapelekea manabii na mitume, lakini watawaua baadhi yao, na kuwatesa wengine.’ 50Matokeo yake ni kwamba kizazi hiki kitaadhibiwa kwa sababu ya damu ya manabii wote iliyomwagika tangu mwanzo wa ulimwengu; 51tangu kumwagwa damu ya Abeli#11:50-51 Abeli: Alikuwa mtu wa kwanza kuuawa ambaye anatajwa katika A.K. (Mwa 4:8), na Zakaria ni wa mwisho kulingana na orodha ya vitabu katika kanuni ya vitabu vya Biblia ya Kiebrania (2Nya 24:20-22). mpaka ile ya Zekaria ambaye walimuua kati ya madhabahu na mahali patakatifu.#11:51 Mahali Patakatifu: Taz Mwa 4:8; 2Nya 24:20-22. Naam, hakika kizazi hiki kitaadhibiwa kwa matendo hayo.
52“Ole wenu nyinyi waalimu wa sheria, kwa sababu mmeuficha ule ufunguo wa mlango wa elimu; nyinyi wenyewe hamkuingia na mmewazuia waliokuwa wanaingia wasiingie.”
53Alipokuwa akitoka pale, wale Mafarisayo na waalimu wa sheria walianza kumshambulia vikali na kumsonga kwa maswali mengi 54ili wapate kumnasa kwa maneno yake.

Iliyochaguliwa sasa

Luka 11: BHNTLK

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia