Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohane 17

17
Yesu anawaombea wanafunzi wake
1Yesu alipokwisha sema hayo,#17:1-26 Sala hii rasmi ambayo Yesu anajiombea mwenyewe (1-5), anawaombea wanafunzi wake (6-19), na anawaombea wote wale ambao baadaye watamwamini (20-26), pengine inajulikana kama “sala ya kikuhani”. Rejea Rom 8:34; Ebr 7:24-27. alitazama juu mbinguni, akasema, “Baba, ile saa imefika! Mtukuze Mwanao#17:1 Saa imefika …Mtukuze Mwanao: Taz 2:4 maelezo. Na kuhusu kutukuzwa kwake taz 7:39 maelezo; 12:16,23,26; 13:31-32.Saa ya kifo chake ambacho kitawaletea binadamu wokovu. ili naye Mwana apate kukutukuza. 2Maana ulimpa Mwanao mamlaka juu ya watu wote ili awape uhai wa milele wote hao uliompa. 3Na uhai wa milele ndio huu: kukujua wewe#17:3 Kukujua wewe: Huku kumjua Mungu haihusu namna ya utambuzi wa akili tu bali inajumuisha pamoja na hilo kukubali kwa moyo, kumwamini, kumpenda na kumtii Mungu na Mwanawe Yesu Kristo (rejea 14:7,9; 16:3; 17:25; 1Yoh 2:3-6,13-14; 3:1,6; 4:7-8; 5:20). uliye peke yako Mungu wa kweli, na kumjua Yesu Kristo uliyemtuma. 4Mimi nimekutukuza hapa duniani; nimeikamilisha ile kazi uliyonipa niifanye. 5Sasa, Baba, nitukuze mbele yako kwa ule utukufu niliokuwa nao kabla ya kuumbwa ulimwengu.#17:5 Utukufu niliokuwa nao kabla ya kuumbwa ulimwengu: Katika Injili hii Yohane anadokezea kwa namna mbali mbali jambo la kuweko kwa Yesu Kristo kabla ya kuumbwa ulimwengu 1:1-3,15,30; 8:58. Rejea pia Meth 8:23; Sira 1:4; 24:9; Hek 9:9, mahali ambapo kwa jumla kuweko kwa “hekima” kabla ya kuumbwa ulimwengu kunatajwa.
6“Nimekufanya ujulikane kwa watu wale ulionipa kutoka duniani. Walikuwa watu wako, nawe ukanipa wawe wangu; nao wamelishika neno lako. 7Sasa wanajua kwamba kila ulichonipa kimetoka kwako. 8Mimi nimewapa ule ujumbe ulionipa, nao wameupokea; wanajua kwamba kweli nimetoka kwako, na wanaamini kwamba wewe ulinituma.
9“Nawaombea hao; siuombei ulimwengu,#17:9 Ulimwengu: Taz 12:31 maelezo. ila nawaombea wale ulionipa, maana ni wako. 10Yote niliyo nayo ni yako, na yako ni yangu; na utukufu wangu umeonekana katika hao ulionipa. 11Na sasa naja kwako; simo tena ulimwenguni, lakini wao wamo ulimwenguni. Baba Mtakatifu! Kwa nguvu ya jina lako ulilonipa, tafadhali uwaweke salama ili wawe kitu kimoja kama sisi tulivyo mmoja. 12Nilipokuwa nao, mimi niliwaweka salama kwa nguvu ya jina lako ulilonipa. Mimi nimewalinda, wala hakuna hata mmoja wao aliyepotea, isipokuwa yule mwana mpotevu,#17:12 Mwana mpotevu: Ndivyo ilivyo neno kwa neno kutoka Kigiriki. Tafsiri nyingine yamkini ni “yule ambaye ilibidi apotee”. Hapa Yesu alikuwa anasema juu ya Yuda Iskarioti. Taz pia 6:70,71; 13:2. ili Maandiko Matakatifu yapate kutimia. 13Basi, sasa naja kwako, na nimesema mambo haya ulimwenguni, ili waweze kushiriki kikamilifu furaha yangu. 14Mimi nimewapa ujumbe wako, nao ulimwengu ukawachukia, kwa sababu wao si wa ulimwengu, kama vile nami nisivyo wa ulimwengu. 15Siombi uwatoe ulimwenguni, bali naomba uwakinge na yule Mwovu.#17:15 Yule Mwovu: Yaani Shetani. 16Wao si wa ulimwengu, kama vile nami nisivyo wa ulimwengu. 17Waweke wakfu katika ukweli; neno lako ni ukweli. 18Kama vile ulivyonituma ulimwenguni, nami pia nimewatuma wao ulimwenguni; 19na kwa ajili yao mimi mwenyewe najiweka wakfu ili nao pia wafanywe wakfu katika ukweli.
20“Siwaombei hao tu, bali nawaombea pia wote watakaoamini kutokana na ujumbe wao. 21Naomba ili wote wawe kitu kimoja.#17:21 Wote wawe kitu kimoja: Rom 12:4-5; 1Kor 10:17; Efe 4:3-6. Ombi la Yesu kwa ajili ya waamini wote wa nyakati zote ni kwamba wawe na umoja kama vile Yesu na Baba walivyo mmoja. Baba! Naomba wawe ndani yetu kama vile wewe ulivyo ndani yangu nami ndani yako. Naomba wawe kitu kimoja kusudi ulimwengu upate kuamini kwamba wewe ulinituma. 22Mimi nimewapa utukufu uleule ulionipa mimi, ili wawe kitu kimoja kama nasi tulivyo mmoja; 23mimi niwe ndani yao, nawe uwe ndani yangu; naomba wakamilishwe na kuwa kitu kimoja, ili ulimwengu upate kujua kwamba wewe ulinituma, na kwamba unawapenda wao kama unavyonipenda mimi.
24“Baba! Nataka hao ulionipa wawe pamoja nami pale nilipo, ili wauone utukufu wangu ulionipa; kwa kuwa ulinipenda kabla ya kuumbwa ulimwengu. 25Baba Mwema! Ulimwengu haukujui, lakini mimi nakujua. Hawa nao wanajua kwamba wewe ulinituma. 26Nimekufanya ujulikane kwao na nitaendelea kufanya hivyo, ili upendo ulio nao kwangu uwe ndani yao, nami niwe ndani yao.”

Iliyochaguliwa sasa

Yohane 17: BHNTLK

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia