Waebrania 11
11
Imani
1Kuwa na imani ni kuwa na hakika ya mambo tunayotumainia; kusadiki kabisa mambo tusiyoyaona.#11:1 Sura hii yote kama inavyoonekana katika 11:1-4 lengo lake ni kuwatia moyo waumini washikilie imani yao kwa Kristo. Kwanza kabisa katika 11:1 mwandishi anatoa maelezo au anafafanua “imani”, Rejea Rom 8:24-25; 2Kor 4:18. 2Maana wazee wa kale walipata kibali cha Mungu kwa sababu ya imani yao.
3Kwa imani sisi tunafahamu kwamba ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu; vitu vinavyoonekana kutoka vitu visivyoonekana.
4Kwa imani Abeli alimtolea Mungu tambiko iliyokuwa bora kuliko ile ya Kaini. Kwa imani yake alikubaliwa na Mungu kuwa mwadilifu; Mungu mwenyewe alizikubali sadaka zake. Kwa imani yake ingawa alikufa, bado ananena.
5Kwa imani Henoki alichukuliwa na Mungu, asipate kufa. Hakuonekana tena kwa sababu Mungu alikuwa amemchukua. Maandiko yasema kwamba kabla ya kuchukuliwa kwake, yeye alikuwa amempendeza Mungu. 6Basi, pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu. Kwa maana kila mtu anayemwendea Mungu ni lazima aamini kwamba Mungu yuko, na kwamba huwatuza wale wanaomtafuta.
7Kwa imani Noa alionywa na Mungu juu ya mambo ya baadaye ambayo hayakuwa yameonekana bado. Alimtii Mungu, akajenga ile safina ambamo aliokolewa yeye pamoja na jamaa yake. Kutokana na hayo ulimwengu ulihukumiwa, naye Noa akapokea uadilifu unaotokana na imani.
8Kwa imani Abrahamu alimtii Mungu alipoitwa aende katika nchi ambayo Mungu angempa iwe yake. Ingawa hakujua alikokuwa anakwenda, Abrahamu alihama. 9Kwa imani aliishi kama mgeni#11:9 Aliishi kama mgeni: Ebr 6:13-15. katika nchi aliyoahidiwa na Mungu. Aliishi huko katika hema kama walivyoishi Isaka na Yakobo, ambao pia walishiriki ahadi ileile.#11:9 Walishiriki ahadi ileile: Mwa 23:4; 26:3; 35:12,27. 10Maana Abrahamu alikuwa akingojea mji#11:10 Mji: Yaani, mji wa mbinguni; rejea aya ya 16. wenye misingi imara, mji ambao Mungu mwenyewe ndiye fundi aliyeubuni na kuujenga. 11Kwa imani hata Sara aliamini kwamba Mungu hutimiza ahadi zake, kwa hiyo akajaliwa kuchukua mimba ingawaje alikuwa amepita umri. 12Kwa hiyo, kutoka katika mtu huyo mmoja, Abrahamu, ambaye alikuwa kama amekufa, walitokea watu wengi wasiohesabika kama vile nyota za mbinguni na mchanga wa pwani.
13Watu hawa wote walikufa wakiwa na imani. Walikufa kabla ya kupokea mambo ambayo Mungu alikuwa ameahidi, lakini kwa mbali waliyaona, wakashangilia, na kukiri wazi kwamba wao walikuwa wageni na wakimbizi duniani. 14Watu wanaosema mambo kama hayo, huonesha wazi kwamba wanaitafuta nchi yao wenyewe. 15Kama wangalikuwa wanaifikiria nchi walikotoka zamani, wangalipata nafasi ya kurudi huko. 16Lakini sasa wanataka nchi iliyo bora zaidi, yaani nchi ya mbinguni.#11:16 Nchi ya mbinguni: Rejea Fil 3:20. Ndio maana Mungu haoni haya wakimwita yeye Mungu wao, kwa sababu yeye mwenyewe amekwisha watayarishia mji.
17Kwa imani Abrahamu alimtoa tambiko mwanawe Isaka wakati Mungu alipomjaribu. Huyo Abrahamu ndiye aliyekuwa amepokea ahadi ya Mungu, lakini, hata hivyo, alikubali kumtoa tambiko mwanawe wa pekee, 18ingawa Mungu alikuwa amemwambia: “Wazawa wako watatokana na Isaka.” 19Abrahamu aliamini kwamba Mungu anaweza kuwafufua wafu; na kwa namna fulani kweli Abrahamu alimpata tena mwanawe kutoka kwa wafu.
20Kwa imani Isaka aliwabariki Yakobo na Esau, wapate baraka zitakazokuja baadaye.
21Kwa imani Yakobo alipokuwa karibu kufa, aliwabariki kila mmoja wa wana wa Yosefu, akamwabudu Mungu akiegemea kichwa cha ile fimbo yake.#11:21 Mwa 47:31—48:20. “Akiegemea ile fimbo yake”; tafsiri kulingana na Kigiriki cha Septuajinta - LXX (Mwa 47:31).
22Kwa imani Yosefu alipokuwa karibu kufa, alinena juu ya kutoka kwa Waisraeli katika nchi ya Misri, na pia akawaachia maagizo kuhusu mifupa yake.#11:22 Mwa 50:24-25; Kut 13:19; Yos 24:32. Kwa kuagiza mifupa yake ipelekwe nchini Kanaani, Yosefu alionesha imani yake kwamba Waisraeli wangepata ile nchi waliyoahidiwa na Mungu.
23Kwa imani wazazi wa Mose walimficha huyo mtoto kwa muda wa miezi mitatu baada ya kuzaliwa kwake. Walimwona kuwa ni mtoto mzuri, wala hawakuiogopa amri ya mfalme.
24Kwa imani Mose alipokuwa mtu mzima, alikataa kuitwa mwana wa binti Farao. 25Aliona ni afadhali kuteseka pamoja na watu wa Mungu kuliko kufurahia raha ya dhambi kwa kitambo kidogo. 26Alitambua kwamba kuteseka kwa ajili ya Kristo kuna faida kubwa kuliko utajiri wote wa nchi ya Misri, maana alikuwa anatazamia tuzo la baadaye.
27Kwa imani Mose alihama kutoka nchi ya Misri bila kuogopa hasira ya mfalme; na wala hakurudi nyuma, kwani alikuwa kama mtu aliyemwona yule Mungu asiyeonekana.#11:27 Haieleweki kwa urahisi; lakini yaweza kuchukuliwa kama rejeo kwa tukio la Kutoka 2:11-15 au hata juu ya kuondoka kwa Waisraeli katika nchi ya Misri chini ya uongozi wa Mose (Kut 13:17—14:30). 28Kwa imani aliadhimisha siku ya Pasaka, akaamuru damu inyunyizwe juu ya milango, ili yule Malaika Mwangamizi asiwaue wazaliwa wa kwanza wa Israeli.
29Kwa imani watu wa Israeli walivuka bahari ya Shamu kana kwamba ilikuwa nchi kavu; lakini Wamisri walipojaribu kufanya hivyo walikufa maji.
30Kwa imani kuta za mji wa Yeriko zilianguka watu wa Israeli walipokwisha zunguka kuta hizo kwa siku saba. 31Kwa imani Rahabu aliyekuwa malaya hakuangamia pamoja na wale waliomwasi Mungu, kwa sababu aliwakaribisha wale wapelelezi.
32Basi, niseme nini zaidi? Wakati hauniruhusu kueleza juu ya Gideoni, Baraki, Samsoni, Yeftha, Daudi, Samueli na manabii.#11:32 Watu wote wanaotajwa katika aya hii, visa vinavyo husika vya hao watu vimo katika Waamuzi 4—12 na 1Sam 1—1Fal 2. 33Kwa imani hawa wote walipigana vita na wafalme, wakashinda. Walitenda mambo adili, wakapokea yale aliyoahidi Mungu. Walifunga vinywa vya simba,#11:33 Walifunga vinywa vya simba: Amu 14:5-6; 1Sam 17:34-37; Dan 6. 34walizima mioto mikali, waliepuka kuuawa kwa upanga, walikuwa dhaifu lakini walipata nguvu. Walikuwa hodari katika vita, wakashinda majeshi ya kigeni. 35Na, wanawake walioamini walirudishiwa wafu wao#11:35 Wanawake walioamini walirudishiwa wafu wao: 1Fal 17:17-24; 2Fal 4:25-37. wakiwa wamefufuliwa.
Baadhi yao walikataa kufunguliwa, wakateswa mpaka kufa ili wapate kufufuliwa na kuingia katika maisha bora zaidi.#11:35 Baadhi yao walikataa kufunguliwa …wapate … kuingia katika maisha bora zaidi: Kwa kusema hivyo mwandishi anataja visa vilivyowasibu Wayahudi katika historia yao, aghalabu visa vya nyakati za Wamakabayo. 36Wengine walidhihakiwa na kupigwa mijeledi, na wengine walifungwa minyororo na kutupwa gerezani.#11:36 Walifungwa minyororo na kutupwa gerezani: 1Fal 22:26-27; 2Nya k 18:25-26; Yer 20:2; 37:15; 38:6. 37Walipigwa mawe,#11:37 Walipigwa mawe: Rejea 2Nya k 24:20-21. Kulingana na mapokeao ya Kiyahudi nabii Yeremia alishambuliwa hivyo kwa kuwa alihubiri dhidi ya kuabudu miungu mingine. walipasuliwa vipandevipande,#11:37 Walipasuliwa vipandevipande: Kulingana na mapokeo ya Kiyahudi nabii Isaya aliuawa namna hiyo. waliuawa kwa upanga. Walizungukazunguka wakiwa wamevaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa watu maskini, walioteswa na kudhulumiwa. 38Ulimwengu haukustahili kuwa na watu hao. Walitangatanga jangwani na milimani, wakaishi katika mashimo na mapango ya ardhi.
39Watu hawa wote walionekana kuwa mashujaa kwa sababu ya imani yao. Hata hivyo, hawakupokea yale ambayo Mungu aliwaahidi, 40maana Mungu alikuwa ameazimia mpango ulio bora zaidi#11:40 Bora zaidi: Neno kitovu katika barua hii; rejea aya 16, 35 na taz Ebr 7:19 maelezo. kwa ajili yetu; yaani wao wangeufikia ukamilifu wakiwa pamoja nasi.
Iliyochaguliwa sasa
Waebrania 11: BHNTLK
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993
The Bible Society of Kenya 1993