Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waebrania 12

12
Bwana atufunza kuwa na nidhamu#12:1-11 Sehemu hii inaendelea na maneno ya kutia moyo ya Ebr 10:19-39.
1Sisi tunalo kundi hili kubwa la mashahidi#12:1 Tunalo kundi hili …la mashahidi: Mwandishi anatukumbusha kwa jumla hao aliowataja katika sura iliyotangulia ambao wanawakilisha watu wenye imani wa nyakati zote. Kutokana na wazo hilo mwandishi anawahimiza waumini wapige mbio mithili ya wanariadha (aya 1 na 2). mbele yetu. Kwa hiyo tuondoe kila kizuizi kinachotuzuia, na dhambi ile inayotung'ang'ania. Tupige mbio kwa uvumilivu katika mashindano yaliyowekwa mbele yetu. 2Tumwelekee Yesu ambaye ndiye aliyeianzisha imani yetu na ambaye ataikamilisha. Kwa ajili ya furaha iliyokuwa inamngojea, yeye alivumilia kifo msalabani, bila kuijali aibu yake, na sasa anaketi upande wa kulia wa kiti cha enzi cha Mungu.#12:2 Kufa msalabani kulikuwa kifo cha aibu na ukatili kupita vyote. Rejea Ebr 2:10; 5:8-9.
3Fikirini juu ya mambo yaliyompata Yesu, jinsi alivyostahimili upinzani mkubwa kwa watu wenye dhambi. Basi, msife moyo, wala msikate tamaa. 4Maana katika kupambana na dhambi, nyinyi hamjapigana mpaka kiasi cha kumwaga damu yenu. 5Je, mmesahau yale maneno ya kutia moyo ambayo Mungu anawataja nyinyi kuwa wanawe?
“Mwanangu, usidharau adhabu ya Bwana,
wala usife moyo anapokukanya.
6Maana Bwana humpa nidhamu kila anayempenda,
humwadhibu kila anayekubali kuwa mwanawe.”
7Vumilieni adhabu kwani ni mafundisho; Mungu huwatendea nyinyi kama wanawe. Maana ni mwana gani asiyeadhibiwa na baba yake? 8Lakini msipoadhibiwa kama wana wengine, basi, nyinyi si wanawe, bali ni wana haramu. 9Zaidi ya hayo, sisi tunawaheshimu wazazi wetu waliotuzaa hata wanapotuadhibu. Basi, tunapaswa kumtii zaidi Baba yetu wa kiroho ili tupate kuishi. 10Wazazi wetu hapa duniani walituadhibu kwa muda, kama wao wenyewe walivyoona kuwa vema; lakini Mungu anatuadhibu kwa ajili ya faida yetu wenyewe, tupate kuushiriki utakatifu wake. 11Kuadhibiwa si jambo la kufurahisha bali la kuhuzunisha. Lakini wale waliofunzwa kuwa na nidhamu mwishowe watavuna tuzo la amani kutoka katika maisha adili.
Mafundisho na maonyo
12Basi, inueni mikono yenu inayolegea na kuimarisha magoti yenu yaliyo dhaifu.#12:12-13 Mwandishi anaweka pamoja mafungu aliyoyatoa katika Isa 35:3 na Meth 4:26 na kuendeleza ile picha ya mwanariadha ya aya 1-2. 13Endeleeni kutembea katika njia iliyonyoka, ili kile kilicholemaa kisiumizwe, bali kiponywe.
14Jitahidini kuishi kwa amani na watu wote.#12:14 Jitahidini kuishi kwa amani na watu wote: Rom 12:18; rejea Zab 34:14 sehemu ambayo imenukuliwa pia katika 1Pet 3:11. Ishini maisha ya utakatifu, kwa sababu hakuna mtu atakayemwona Bwana bila ya maisha kama hayo. 15Jitahidini sana mtu yeyote asije akapoteza neema ya Mungu. Muwe waangalifu ili mti mchungu usizuke kati yenu na kuwaua wengi kwa sumu yake. 16Jihadharini ili miongoni mwenu pasiwe na mtu mwasherati au mtu asiyemcha Mungu kama Esau, aliyeuza haki yake ya mzaliwa wa kwanza kwa mlo mmoja.#12:16 Mwa 25:29-34. Mapokeo ya Kirabini kuhusu Esau yalimfikiria kuwa mwenye tabia ya uasherati; lakini hatuna mahali penginepo katika A.K. penye wazo la namna hiyo. 17Nyinyi mnafahamu kwamba hata alipotaka kuipata tena ile baraka iliyokuwa yake, alikataliwa, maana hakupata tena nafasi ya kutubu, ingawa aliitafuta kwa machozi.
18Nyinyi hamkuwasili mlimani Sinai, ambao unaweza kushikika kama walivyofanya watu wa Israeli; hamkufika kwenye moto uwakao, penye giza, tufani, 19mvumo wa tarumbeta na sauti ya maneno. Wale waliosikia sauti hiyo waliomba wasisikie tena neno lingine, 20kwani hawakuweza kustahimili amri iliyotolewa: “Atakayegusa mlima huu, hata kama ni mnyama, atapigwa mawe.” 21Hayo yote yalionekana ya kutisha mno, hata Mose akasema, “Naogopa na kutetemeka.”#12:21 Rejea Kumb 9:19. Katika 12:18-21 mwandishi analinganisha mlima Sinai (Kut 19:16-22) na mlima Siyoni unaotajwa katika 12:22 na kuiona kuwa mifano ya Agano la Kale na Agano Jipya (aya 23-24).
22Lakini nyinyi mmefika katika mlima wa Siyoni,#12:22 Mlima wa Siyoni: Sawa na Yerusalemu, mfano wa mji wa mbinguni. Yerusalemu ya hapa duniani ni kivuli tu cha mji ule utakaokuja (tazama Ebr 8:3-5). Rejea 11:10,14-16; 13:14; pia Gal 4:26; Ufu 21:2. kwenye mji wa Mungu aliye hai. Mmefika Yerusalemu, mji wa mbinguni, ambapo wamekusanyika malaika kwa maelfu. 23Mmefika kwenye kusanyiko kubwa la wazaliwa wa kwanza wa Mungu, ambao majina yao yameandikwa mbinguni. Mnasimama mbele ya Mungu aliye hakimu wa wote, na mbele ya roho za watu waadilifu waliofanywa wakamilifu. 24Mmefika kwa Yesu ambaye ni mpatanishi katika agano jipya,#12:24 Yesu ambaye ni mpatanishi katika agano jipya: Taz Ebr 8:6. na ambaye damu yake iliyomwagika inasema mambo mema kuliko ile ya Abeli.#12:24 Damu …ya Abeli: Iliita kisasi (Mwa 4:10) lakini ile ya Yesu ambayo yasema mambo mema zaidi inawapatia watu msamaha.
25Basi, jihadharini msije mkakataa kumsikiliza huyo anayesema nanyi. Kama wale waliokataa kumsikiliza yule aliyewaonya hapa duniani hawakuokoka, sisi tutawezaje kuokoka kama tukikataa kumsikiliza yule anayetuonya kutoka mbinguni?#12:25 Kut 20:22. Kule jangwani Waisraeli walikataa mara kwa mara kumsikiliza Mungu. Rejea Ebr 10:28-29. 26Wakati ule sauti ilitetemesha nchi, lakini sasa ameahidi: “Nitatetemesha nchi tena, lakini si nchi tu bali pia mbingu.”#12:26 Hag 2:6; rejea Kut 19:18; Isa 13:13. Huenda aya hizi mbili (26-27) zinagusia jambo la hukumu ya mwisho (rejea 2Pet 3:10; Ufu 6:12-17; 16:18-21; 20:11; 21:1); jambo hilo la hukumu ya mwisho lilikwisha tajwa katika Ebr 1:10-12. 27Neno hili: “tena” linatuonesha kwamba vitu vyote vilivyoumbwa vitatetemeshwa na kutoweka ili vibaki vile visivyotetemeshwa.
28Sisi basi, na tushukuru, kwani tunapokea ufalme usiotikisika. Tuwe na shukrani na kumwabudu Mungu kwa namna itakayompendeza, kwa ibada na hofu; 29maana Mungu wetu kweli ni moto mkali unaoteketeza.

Iliyochaguliwa sasa

Waebrania 12: BHNTLK

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia