Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Wimbo ulio Bora 5

5
Ndoto nyingine
1 # Wim 4:16; Lk 15:7; Yn 3:29 Naingia bustanini mwangu, dada yangu, bibi arusi,
Nachuma manemane yangu na rihani,
Nala sega la asali na asali yangu,
Nanywa divai yangu na maziwa.
Kaleni, rafiki zangu, kanyweni,
Naam, nyweni sana, wapendwa wangu.
2 # Mit 8:4; Ufu 3:20 Nilikuwa nimelala, lakini moyo wangu uko macho,
Sikiliza! Mpendwa wangu anabisha!
Nifungulie, dada yangu, mpenzi wangu,
Hua wangu, mkamilifu wangu,
Kwa maana kichwa changu kimelowa umande,
Nywele zangu zina manyunyu ya usiku.
3Nimeivua kanzu yangu; niivaeje?
Nimenawa miguu; niichafueje?
4Mpendwa wangu aliutia mkono wake tunduni,
Na moyo wangu ukasisimuka kwa ajili yake.
5Nikaondoka nimfungulie mpendwa wangu;
Mikono yangu ilidondosha manemane,
Na vidole vyangu matone ya manemane,
Penye vipini vya komeo.
6 # Hes 5:15; Omb 3:8 Nilimfungulia mpendwa wangu,
Lakini mpendwa wangu amegeuka amepita;
(Nimezimia nafsi yangu aliponena),
Nikamtafuta, nisimpate,
Nikamwita, asiniitikie.
7 # Wim 3:3; Mdo 20:29,30 Walinzi wazungukao mjini waliniona,
Wakanipiga na kunitia jeraha,
Walinzi walindao kuta zake
Wakaninyang'anya shela yangu.
8Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu,
Ninyi mkimwona mpendwa wangu,
Ni nini mtakayomwambia?
Ya kwamba nazimia kwa mapenzi.
Maongezi ya marafiki na bibi arusi
9Mpendwa wa namna gani ni mpendwa wako,
Wewe uliye mzuri katika wanawake,
Mpendwa wa namna gani ni mpendwa wako,
Hata wewe utusihi hivyo?
10Mpendwa wangu ni mweupe, tena mwekundu,
Mashuhuri miongoni mwa elfu kumi;
11Kichwa chake ni kama dhahabu safi sana,
Nywele zake ni za ukoka, nyeusi kama kunguru;
12 # Wim 1:15 Macho yake ni kama hua penye vijito,
Wakioga kwa maziwa, wakiikalia mito iliyojaa;
13Mashavu yake ni kama matuta ya rihani
Ambayo hufanyizwa manukato;
Midomo yake ni kama nyinyoro,
Inadondosha matone ya manemane;
14Mikono yake ni kama mianzi ya dhahabu,
lliyopambwa kwa zabarajadi;
Kiwiliwili chake kama kazi ya pembe,
Iliyonakishiwa kwa yakuti samawi;
15Miguu yake ni kama nguzo za marimari,
Zilizowekwa juu ya misingi ya dhahabu;
Sura yake ni kama Lebanoni,
Ni bora mfano wa mierezi;
16 # Zab 45:2; Yer 31:3; Rum 8:35; Flp 3:8 Kinywa chake kimejaa maneno matamu,
Ndiye mzuri sana kwa ujumla.
Ni huyu mpendwa wangu, ni huyu rafiki yangu,
Enyi binti za Yerusalemu.

Iliyochaguliwa sasa

Wimbo ulio Bora 5: SRUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha