Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ruthu 2:8-23

Ruthu 2:8-23 SRUV

Basi Boazi akamwambia Ruthu, Mwanangu, sikiliza; wewe usiende kuokota masazo katika shamba lingine, wala usiondoke hapa, lakini ukae papa hapa karibu na wasichana wangu. Macho yako na yaelekee shamba walivunalo, ufuatane nao; je! Sikuwaagiza vijana wasikusumbue? Tena, ukiona kiu, uende kwenye vyombo, nawe uyanywe waliyoyateka hao vijana. Ndipo aliposujudia, akainama mpaka nchi, akamwambia, Jinsi gani nimepata kibali machoni pako, hata ukanifahamu, mimi niliye mgeni? Naye Boazi akajibu, akamwambia, Nimeelezwa sana yote uliyomfanyia mkweo, tangu alipokufa mumeo; na jinsi ulivyowaacha baba yako na mama yako, na nchi yako uliyozaliwa, ukawafikia watu usiowajua tangu hapo. BWANA akujaze kwa kazi yako, nawe upewe thawabu kamili na BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye umekuja kukimbilia chini ya mabawa yake. Ndipo aliposema, Bwana wangu, na nipate kibali machoni pako; kwa sababu wewe umeniburudisha moyo, na kumwambia mema mjakazi wako, ingawa mimi si kama mmojawapo wa wajakazi wako. Tena wakati wa chakula huyo Boazi akamwambia, Karibu kwetu, ule katika mkate wetu, na ulichovye tonge lako katika siki yetu. Basi akaketi pamoja na wavunaji, nao wakampitishia bisi, naye akala akashiba, hata akasaza. Naye alipoinuka tena ili aende kuokota masazo, huyo Boazi aliwaagiza vijana wake akisema, Mwacheni aokote hata kati ya miganda, wala msimkemee. Tena mtoleeni kidogo katika matita na kukiacha, na akiokote, wala msimkataze. Basi Ruthu akaokota mabaki shambani hadi jioni; kisha akazipura zile nafaka alizoziokota, zikawa yapata efa moja ya shayiri. Akajitwika, akaenda zake mjini. Akamwonesha mkwewe zile alizoziokota; akavitoa vile vyakula alivyovisaza alipokwisha kushiba, akampa. Basi mkwewe akamwuliza, Je! Umeokota wapi leo? Umefanya kazi wapi? Na abarikiwe yeye aliyekufahamu. Naye akamwarifu mkwewe ni nani ambaye alifanya kazi kwake, akasema, Yule mtu niliyefanya kazi kwake leo jina lake aitwa Boazi. Naye Naomi akamwambia mkwewe, Na abarikiwe huyo na BWANA, ambaye hakuuacha wema wake, wala kwa hao walio hai wala kwa waliokufa. Kisha Naomi akamwambia, Mtu huyu ni wa ukoo wetu, mmojawapo wa jamaa yetu aliye karibu. Naye Ruthu Mmoabi akasema, Naam, akaniambia, Ukae papa hapa karibu na watumishi wangu, hadi watakapomaliza mavuno yangu yote. Kisha Naomi akamwambia Ruthu mkwewe, Mwanangu, ni vizuri wewe ufuatane na wasichana wake, ili watu wasikusumbue katika shamba lingine lolote lile. Hivyo yeye akafuatana na wasichana wake Boazi na kuokota, hadi mwisho wa mavuno ya shayiri na mavuno ya ngano pia; naye alikuwa akikaa kwa mkwewe.

Soma Ruthu 2