Zaburi 9:11-20
Zaburi 9:11-20 SRUV
Mwimbieni BWANA akaaye Sayuni, Yatangazeni kwa watu matendo yake. Maana mlipiza kisasi cha damu awakumbuka, Hakukisahau kilio cha wanyonge. Wewe, BWANA, unifadhili, Tazama mateso niteswayo na wanaonichukia; Wewe uniinuaye katika malango ya mauti, Ili nizisimulie sifa zako zote; Katika malango ya binti Sayuni Nitaufurahia wokovu wako. Mataifa wamezama katika shimo walilolichimba; Kwa wavu waliouficha imenaswa miguu yao. BWANA amejidhihirisha na kutekeleza hukumu; Amemnasa mdhalimu kwa kazi ya mikono yake. Wadhalimu wataenda kuzimu, Naam, mataifa yote wanaomsahau Mungu. Kwa maana mhitaji hatasahauliwa daima; Matumaini ya wanyonge hayatapotea milele. Inuka, ee BWANA, mwanadamu asipate nguvu, Mataifa wahukumiwe mbele zako. Uwatie hofu, ee BWANA, Watu wa mataifa na wajitambue kuwa wao ni binadamu tu!