Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 89:1-18

Zaburi 89:1-18 SRUV

Fadhili za BWANA nitaziimba milele; Kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako. Maana nimesema, Fadhili zitajengwa milele; Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako. Nimefanya agano na mteule wangu, Nimemuapia Daudi, mtumishi wangu. Wazao wako nitawaimarisha milele, Nitakijenga kiti chako cha enzi hata milele. Ee BWANA, mbingu zitayasifu maajabu yako, Uaminifu wako katika kusanyiko la watakatifu. Maana ni nani katika mbingu awezaye kulinganishwa na BWANA? Ni nani afananaye na BWANA miongoni mwa malaika? Mungu huogopwa sana barazani pa watakatifu, Ni wa kuhofiwa kuliko wote wanaomzunguka. BWANA, Mungu wa majeshi, Ni nani aliye hodari kama Wewe, Ee YAHU? Na uaminifu wako unakuzunguka. Wewe ndiwe ukitawalaye kiburi cha bahari. Mawimbi yake yainukapo, wewe unayatuliza. Ndiwe uliyemponda Rahabu akawa kama aliyeuawa, Kwa mkono hodari umewatawanya wakuchukiao. Mbingu ni mali yako, nchi nayo ni mali yako, Ulimwengu na vyote viujazavyo Ndiwe uliyeupiga msingi wake. Kaskazini na kusini ndiwe uliyeziumba, Tabori na Hermoni hulifurahia jina lako. Mkono wako ni mkono wenye uweza, Mkono wako una nguvu, Mkono wako wa kulia umetukuka. Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chako, Fadhili na kweli zimo mbele za uso wako. Heri watu wale waijuao sauti ya shangwe, Ee BWANA, waendao, katika nuru ya uso wako. Kwa jina lako hufurahi mchana kutwa, Na kwa haki yako hutukuzwa. Maana fahari ya nguvu zao ni Wewe, Na kwa radhi yako pembe yetu itatukuka. Maana ngao yetu ni BWANA, Na mfalme wetu ni wake Mtakatifu wa Israeli.

Soma Zaburi 89