Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 89:1-18

Zaburi 89:1-18 NENO

Nitaimba kuhusu upendo mkuu wa Mwenyezi Mungu milele; kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako. Nitatangaza kuwa upendo wako unasimama imara milele na uaminifu wako umeuthibitisha mbinguni. Ulisema, “Nimefanya agano na mteule wangu, nimemwapia mtumishi wangu Daudi, ‘Nitaimarisha uzao wako milele na kudumisha ufalme wako kwa vizazi vyote.’ ” Ee Mwenyezi Mungu, mbingu zinayasifu maajabu yako, uaminifu wako pia katika kusanyiko la watakatifu. Kwa kuwa ni nani katika mbingu anayeweza kulinganishwa na Mwenyezi Mungu? Ni nani miongoni mwa viumbe vya mbinguni aliye kama Mwenyezi Mungu? Katika kusanyiko la watakatifu, Mungu huogopwa sana, anahofiwa kuliko wote wanaomzunguka. Ee Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, ni nani aliye kama wewe? Ee Mwenyezi Mungu, wewe ni mwenye nguvu, na uaminifu wako unakuzunguka. Wewe unatawala bahari yenye msukosuko; mawimbi yake yanapoinuka, wewe unayatuliza. Wewe ulimponda Rahabu kama mmoja wa waliochinjwa; kwa mkono wako wenye nguvu, uliwatawanya adui zako. Mbingu ni zako, nayo nchi pia ni yako, uliuwekea ulimwengu msingi pamoja na vyote vilivyomo. Uliumba kaskazini na kusini; Tabori na Hermoni wanaliimbia jina lako kwa furaha. Mkono wako umejaa uwezo; mkono wako una nguvu, mkono wako wa kuume umetukuka. Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chako cha enzi; upendo na uaminifu vinakutangulia. Heri ni wale ambao wamejifunza kukusifu kwa shangwe, wanaotembea katika mwanga wa uwepo wako, Ee Mwenyezi Mungu. Wanashangilia katika jina lako mchana kutwa, wanafurahi katika haki yako. Kwa kuwa wewe ni utukufu na nguvu yao, kwa wema wako unatukuza pembe yetu. Naam, ngao yetu ni mali ya Mwenyezi Mungu, na mfalme wetu mali ya Aliye Mtakatifu wa Israeli.