Zaburi 37:1-40
Zaburi 37:1-40 SRUV
Usihangaike kwa sababu ya watenda mabaya, Usiwahusudu wafanyao ubatili. Maana kama majani watakatika mara, Kama miche mibichi watanyauka. Umtumaini BWANA ukatende mema, Ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu. Nawe ujifurahishe katika BWANA, Naye atakutimizia haja za moyo wako. Umkabidhi BWANA njia yako, Pia umtumainie, naye atakutendea. Ataitokeza haki yako kama nuru, Na hukumu yako kama jina la adhuhuri. Utulie mbele za BWANA, Nawe umngojee kwa subira; Usihangaike juu ya afanikiwaye katika njia yake, Wala mtu apangaye maovu. Ukomeshe hasira, uache ghadhabu, Usikasirike, mwisho wake ni kutenda mabaya. Maana watenda mabaya watakatiliwa mbali, Bali wamngojao BWANA ndio watakaoirithi nchi. Maana bado kitambo kidogo asiye haki hatakuwapo, Utapaangalia mahali pake wala hatakuwapo. Bali wenye upole watairithi nchi, Watajifurahisha kwa wingi wa amani. Asiye haki hunuia mabaya juu ya mwenye haki, Na kumsagia meno yake. BWANA atamcheka, Maana ameona kwamba siku yake inakuja. Wasio haki wamefuta upanga na kupinda uta, Wamwangushe chini maskini na mhitaji, Na kuwaua wenye mwenendo wa unyofu. Upanga wao utaingia mioyoni mwao wenyewe, Na nyuta zao zitavunjika. Kidogo alicho nacho mwenye haki ni bora Kuliko wingi wa mali wa wasio haki wengi. Maana mikono ya wasio haki itavunjika, Bali BWANA huwategemeza wenye haki. BWANA huwatunza waaminifu, Na urithi wao utakuwa wa milele. Hawataaibika wakati wa ubaya, Na siku za njaa watashiba. Bali wasio haki watapotea, Nao wamchukiao BWANA watatoweka, Kama uzuri wa mashamba, Kama moshi watatoweka. Asiye haki hukopa wala halipi, Bali mwenye haki hufadhili, hukirimu. Maana waliobarikiwa na BWANA watairithi nchi, Nao waliolaaniwa naye watakatiliwa mbali. Hatua za mtu mwema huimarishwa na BWANA, Naye huipenda njia yake. Ajapojikwaa hataanguka chini, Maana BWANA humshika mkono na kumtegemeza. Nilikuwa kijana na sasa ni mzee, Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa Wala mzawa wake akiomba chakula. Mchana kutwa hufadhili na kukopesha, Na mzao wake hubarikiwa. Jiepushe na uovu, utende mema, Na kukaa hata milele. Kwa kuwa BWANA hupenda haki, Wala hawaachi watauwa wake. Wao hulindwa milele, Bali mzawa wa wasio haki ataharibiwa. Wenye haki watairithi nchi, Nao watakaa humo milele. Kinywa chake mwenye haki hunena hekima, Na ulimi wake husema hukumu. Sheria ya Mungu wake imo moyoni mwake. Hatua zake hazitelezi. Mtu asiye haki humvizia mwenye haki, Na kutafuta jinsi ya kumwua. BWANA hatamwacha mkononi mwake, Wala hatamwacha alaumiwe atakapohukumiwa. Wewe umngoje BWANA, Uishike njia yake, Naye atakutukuza uirithi nchi, Utawaona Wasio haki wakiangamizwa. Nimemwona mtu asiye haki mkali sana, Akijieneza kama mwerezi wa Lebanoni. Nikapita na kumbe! Hayuko, Nikamtafuta wala hakuonekana. Umwangalie sana mtu mkamilifu, Umtazame mtu mnyofu, Maana mwisho wake mtu huyo ni amani. Wakosaji wataangamizwa pamoja, Wasio haki mwisho wao wataharibiwa. Na wokovu wa wenye haki una BWANA; Yeye ni ngome yao wakati wa taabu. Naye BWANA huwasaidia na kuwaopoa; Huwaopoa kutoka kwa wasio haki na kuwaponya; Kwa kuwa wamemtumaini Yeye.