Zaburi 37:1-40
Zaburi 37:1-40 NEN
Usisumbuke kwa ajili ya watendao maovu, wala usiwaonee wivu watendao mabaya, kwa maana kama majani watanyauka mara, kama mimea ya kijani watakufa mara. Mtumaini BWANA na utende yaliyo mema; Kaa katika nchi ukafurahie malisho salama. Jifurahishe katika BWANA naye atakupa haja za moyo wako. Mkabidhi BWANA njia yako, mtumaini yeye, naye atatenda hili: Yeye atafanya haki yako ingʼae kama mapambazuko, na hukumu ya shauri lako kama jua la adhuhuri. Tulia mbele za BWANA na umngojee kwa uvumilivu; usisumbuke watu wanapofanikiwa katika njia zao, wanapotekeleza mipango yao miovu. Epuka hasira na uache ghadhabu, usihangaike: itakuongoza tu kutenda uovu. Kwa maana waovu watakatiliwa mbali, bali wale wanaomtumaini BWANA watairithi nchi. Bado kitambo kidogo, nao waovu hawataonekana, ingawa utawatafuta, hawataonekana. Bali wanyenyekevu watairithi nchi na wafurahie amani tele. Waovu hula njama dhidi ya wenye haki na kuwasagia meno, bali Bwana huwacheka waovu, kwa sababu anajua siku yao inakuja. Waovu huchomoa upanga na kupinda upinde, ili wawaangushe maskini na wahitaji, kuwachinja wale ambao njia zao ni nyofu. Lakini panga zao zitachoma mioyo yao wenyewe, na pinde zao zitavunjwa. Bora kidogo walicho nacho wenye haki kuliko wingi wa mali wa waovu wengi; kwa maana nguvu za waovu zitavunjwa, lakini BWANA humtegemeza mwenye haki. BWANA anazifahamu siku za wanyofu, na urithi wao utadumu milele. Siku za maafa hawatanyauka, siku za njaa watafurahia wingi wa vitu. Lakini waovu wataangamia: Adui za BWANA watakuwa kama uzuri wa mashamba, watatoweka, watatoweka kama moshi. Waovu hukopa na hawalipi, bali wenye haki hutoa kwa ukarimu. Wale wanaobarikiwa na BWANA watairithi nchi, bali wale anaowalaani watakatiliwa mbali. Kama BWANA akipendezwa na njia ya mtu, yeye huimarisha hatua zake, ajapojikwaa, hataanguka, kwa maana BWANA humtegemeza kwa mkono wake. Nilikuwa kijana na sasa ni mzee, lakini sijaona kamwe wenye haki wameachwa au watoto wao wakiombaomba chakula. Wakati wote ni wakarimu na hukopesha bila masharti. Watoto wao watabarikiwa. Acha ubaya na utende wema, nawe utaishi katika nchi milele. Kwa kuwa BWANA huwapenda wenye haki naye hatawaacha waaminifu wake. Watalindwa milele, lakini uzao wa waovu utakatiliwa mbali. Wenye haki watairithi nchi, na kuishi humo milele. Kinywa cha mwenye haki hutamka hekima, nao ulimi wake huzungumza lililo haki. Sheria ya Mungu wake imo moyoni mwake; nyayo zake hazitelezi. Watu waovu huvizia wenye haki, wakitafuta kuwaua; lakini BWANA hatawaacha mikononi mwao wala hatawaacha wahukumiwe kuwa wakosa wanaposhtakiwa. Mngojee BWANA, na uishike njia yake. Naye atakutukuza uirithi nchi, waovu watakapokatiliwa mbali, utaliona hilo. Nimemwona mtu mwovu na mkatili akistawi kama mwerezi wa Lebanoni, lakini alitoweka mara na hakuonekana, ingawa nilimtafuta, hakupatikana. Watafakari watu wasio na hatia, wachunguze watu wakamilifu, kuna mafanikio kwa mtu apendaye amani. Lakini watenda dhambi wote wataangamizwa, mafanikio yao yatakatiliwa mbali. Wokovu wa wenye haki hutoka kwa BWANA, yeye ni ngome yao wakati wa shida. BWANA huwasaidia na kuwaokoa, huwaokoa kutoka kwa waovu na kuwahifadhi, kwa maana wanamkimbilia.