Mithali 6:1-35
Mithali 6:1-35 SRUV
Mwanangu, kama umekuwa mdhamini wa rafiki yako, Ikiwa wewe na mgeni mmepeana mikono, Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako, Sasa, mwanangu, fanya hivi ukajiokoe, Kwa kuwa umejitia mkononi mwa jirani yako; Nenda ukanyenyekee, na kumsihi jirani yako. Usiache macho yako kupata usingizi, Wala kope za macho yako kusinzia. Ujiponye kama paa na mkono wa mwindaji, Na kama ndege katika mkono wa mtega mitego. Ewe mvivu, mwendee chungu, Zitafakari njia zake ukapate hekima. Kwa maana yeye hana kiongozi, Wala msimamizi, wala mkuu, Lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; Hukusanya chakula chake wakati wa mavuno. Ewe mvivu, utalala hadi lini? Utaondoka lini katika usingizi wako? Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, Bado kukunja mikono upate usingizi! Hivyo umaskini wako huja kama mnyang'anyi, Na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha. Mtu asiyefaa kitu, mtu wa uovu; Huenda njiani mwenye kinywa cha upotovu. Hukonyeza kwa macho, hunena kwa miguu, Huwaashiria watu kwa vidole vyake. Mna upotovu moyoni mwake, hutunga uovu daima, Hupanda mbegu za magomvi. Basi msiba utampata kwa ghafla; Ghafla atavunjika, bila njia ya kupona. Kuna vitu sita anavyovichukia BWANA; Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake. Macho ya kiburi, ulimi wa uongo, Na mikono imwagayo damu isiyo na hatia; Moyo uwazao mawazo mabaya; Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu; Shahidi wa uongo asemaye uongo; Naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu. Mwanangu, shika maagizo ya baba yako, Wala usiiache sheria ya mama yako. Yafunge hayo katika moyo wako daima; Jivike hayo shingoni mwako. Uendapo yatakuongoza, ulalapo yatakulinda, Na uamkapo yatazungumza nawe. Maana maagizo hayo ni taa, na sheria hiyo ni nuru, Na maonyo ya kumwadilisha mtu ni njia ya uzima. Yakulinde na mwanamke mwovu, asikupate, Na kukuponya na ubembelezi wa mgeni. Usiutamani uzuri wake moyoni mwako; Wala usikubali akunase kwa kope za macho yake. Maana kwa malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate; Na kahaba humwinda mtu anase nafsi yake iliyo ya thamani Je! Mtu aweza kuchukua moto kifuani pake, Na nguo zake zisiteketezwe? Je! Mtu aweza kukanyaga makaa ya moto, Na nyayo zake zisiungue? Ndivyo alivyo aingiaye kwa mke wa jirani yake; Kila mtu amgusaye huyo atakuwa na hatia. Watu hawamdharau mwizi, Akiiba ili kujishibisha, iwapo aona njaa; Lakini akipatikana, atalipa mara saba; Atatoa mali yote ya nyumba yake. Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake. Atapata jeraha na kuvunjiwa heshima; Wala fedheha yake haitafutika. Maana wivu ni ghadhabu ya mtu; Wala hatahurumia siku ya kujilipizia kisasi. Hatakubali fidia yoyote; Wala hatakuwa radhi, ujapomlipa vitu vingi.