Mithali 6:1-35
Mithali 6:1-35 NEN
Mwanangu, kama umekuwa mdhamini wa jirani yako, ikiwa umeshika mikono kwa kuweka ahadi kwa ajili ya mwingine, kama umetegwa na ulichosema, umenaswa kwa maneno ya kinywa chako, basi fanya hivi mwanangu, ili ujiweke huru, kwa kuwa umeanguka mikononi mwa jirani yako: Nenda ukajinyenyekeshe kwake; msihi jirani yako! Usiruhusu usingizi machoni pako, usiruhusu kope zako zisinzie. Jiweke huru, kama swala mkononi mwa mwindaji, kama ndege kutoka kwenye mtego wa mwindaji. Ewe mvivu, mwendee mchwa; zitafakari njia zake ukapate hekima! Kwa maana yeye hana msimamizi, wala mwangalizi, au mtawala, lakini hujiwekea akiba wakati wa kiangazi na hukusanya chakula chake wakati wa mavuno. Ewe mvivu, utalala hata lini? Utaamka lini kutoka usingizi wako? Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, bado kukunja mikono kidogo upate kupumzika: hivyo umaskini utakuja juu yako kama mnyangʼanyi, na kupungukiwa kutakujia kama mtu mwenye silaha. Mtu mbaya sana na mlaghai, ambaye huzungukazunguka na maneno ya upotovu, ambaye anakonyeza kwa jicho lake, anayetoa ishara kwa miguu yake na kuashiria kwa vidole vyake, ambaye hupanga ubaya kwa udanganyifu moyoni mwake: daima huchochea fitina. Kwa hiyo maafa yatamkumba ghafula; ataangamizwa mara, pasipo msaada. Kuna vitu sita anavyovichukia BWANA, naam, viko saba vilivyo chukizo kwake: macho ya kiburi, ulimi udanganyao, mikono imwagayo damu isiyo na hatia, moyo uwazao mipango miovu, miguu iliyo myepesi kukimbilia uovu, shahidi wa uongo ambaye humwaga uongo, na mtu ambaye huchochea fitina kati ya ndugu. Mwanangu, zishike amri za baba yako, wala usiyaache mafundisho ya mama yako. Yafunge katika moyo wako daima, yakaze kuizunguka shingo yako. Wakati utembeapo, yatakuongoza; wakati ulalapo, yatakulinda; wakati uamkapo, yatazungumza nawe. Kwa maana amri hizi ni taa, mafundisho haya ni mwanga na maonyo ya maadili ni njia ya uzima, yakikulinda na mwanamke aliyepotoka, kutokana na maneno laini ya mwanamke aliyepotoka. Moyo wako usitamani uzuri wake wala macho yake yasikuteke, kwa maana kahaba atakufanya uwe maskini, hata ukose kipande cha mkate, naye mwanamke mzinzi huwinda maisha yako hasa. Je, mtu aweza kuchotea moto kwenye paja lake bila nguo zake kuungua? Je, mtu aweza kutembea juu ya makaa ya moto yanayowaka bila miguu yake kuungua? Ndivyo alivyo mtu alalaye na mke wa mwanaume mwingine; hakuna yeyote amgusaye huyo mwanamke ambaye hataadhibiwa. Watu hawamdharau mwizi kama akiiba kukidhi njaa yake wakati ana njaa. Pamoja na hayo, kama akikamatwa, lazima alipe mara saba, ingawa inamgharimu utajiri wote wa nyumba yake. Lakini mwanaume aziniye na mwanamke hana akili kabisa; yeyote afanyaye hivyo hujiangamiza mwenyewe. Mapigo na aibu ni fungu lake na aibu yake haitafutika kamwe; kwa maana wivu huamsha ghadhabu ya mume, naye hataonyesha huruma alipizapo kisasi. Hatakubali fidia yoyote; atakataa malipo, hata yakiwa makubwa kiasi gani.