Mithali 19:1-12
Mithali 19:1-12 SRUV
Afadhali maskini aendaye katika uadilifu wake, Kuliko mpotovu wa midomo aliye mpumbavu. Tena si vizuri nafsi ya mtu ikose maarifa; Naye afanyaye haraka kwa miguu hutenda dhambi. Upumbavu wa mtu hupotosha njia yake; Na moyo wake hununa juu ya BWANA. Utajiri huongeza marafiki wengi; Bali maskini hutengwa na rafiki yake. Shahidi wa uongo hakosi ataadhibiwa; Wala asemaye uongo hataokoka. Watu wengi watamsihi mkuu ili awafadhili; Na kila mtu ni rafiki yake atoaye zawadi. Ndugu zote wa maskini humchukia; Jinsi gani rafiki zake huzidi kujitenga naye! Huwafuata kwa maneno, lakini wametoweka. Apataye hekima hujipenda nafsi yake; Ashikaye ufahamu atapata mema. Shahidi wa uongo hakosi ataadhibiwa; Naye asemaye uongo ataangamia. Maisha ya anasa hayampasi mpumbavu; Sembuse mtumwa awatawale wakuu. Busara ya mtu huiahirisha hasira yake; Nayo ni fahari yake kusamehe makosa. Ghadhabu ya mfalme ni kama ngurumo ya simba; Bali hisani yake kama umande juu ya majani.