Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Obadia 1

1
Kiburi cha Edomu kitashushwa
1 # Isa 21:11; Eze 25:12-14; Yoe 3:19; Mal 1:3 Maono yake Obadia.
Ndivyo asemavyo Bwana MUNGU juu ya Edomu;
Tumepata habari kwa BWANA,
Na mjumbe ametumwa kati ya mataifa,
Akisema, Haya, inukeni ninyi;
Na tuinuke tupigane naye.
2Tazama, nimekufanya mdogo kati ya mataifa;
Umedharauliwa sana.
3 # 2 Fal 14:7; 2 Nya 25:12; Isa 14:13; Ufu 18:7 Kiburi cha moyo wako kimekudanganya,
Wewe ukaaye katika pango za majabali,
Mwenye makao yako juu sana;
Asemaye moyoni, Ni nani atakayenishusha mimi?
4 # Ayu 20:6; Isa 14:14,15; Yer 49:16; Amo 9:2; Hab 2:9 Ujapopanda juu kama tai,
Ijapokuwa kiota chako kimewekwa kati ya nyota,
Nitakushusha kutoka huko; asema BWANA.
Ukatili wa Edomu walipizwa kwa uporaji na mauaji
5Kama wezi wangekujia, kama wanyang'anyi wangekujia usiku, (jinsi ulivyokatiliwa mbali!) Je! Wasingeiba kiasi cha kuwatosha? Kama wachumao zabibu wangekujia, je! Wasingeacha baadhi ya zabibu, ziokotwe? 6Jinsi watu wa Esau wanavyotafutwatafutwa! Jinsi hazina zake zilizofichwa zinavyoulizwaulizwa!
7Watu wote wa mapatano yako
Wamekufukuza, hadi mipakani;
Wale waliofanya amani nawe
Wamekudanganya, na kukushinda;
Walao mkate wako wameweka mtego chini yako;
Wala hana ufahamu wa hayo ndani yake.
8Siku hiyo, je! Sitawaangamiza watu wenye akili katika Edomu, na wenye ufahamu katika kilima cha Esau? Asema BWANA. 9#Zab 76:5; Yer 49:22; Amo 2:16; Nah 3:13 Na mashujaa wako, Ee Temani, watafadhaika, hata iwe kila mtu akatiliwe mbali kwa kuuawa katika kilima cha Esau.
Edomu alimdhulumu nduguye
10 # Mwa 47:21; Zab 137:7; Eze 35:5,15; Amo 1:11; Mal 1:4 Kwa sababu ya udhalimu aliotendwa ndugu yako Yakobo, aibu itakufunika, nawe utakatiliwa mbali hata milele. 11#Nah 3:10 Siku ile uliposimama upande, siku ile wageni walipochukua mali zake, na watu wa kabila nyingine walipoingia katika malango yake, na kumpigia kura Yerusalemu, wewe nawe ulikuwa kama mmoja wao. 12#Mik 4:11; Mit 24:17 Lakini usiitazame siku ya ndugu yako, siku ya mashaka yake, wala usisimange juu ya wana wa Yuda siku ya kuangamizwa kwao; wala usinene maneno ya kiburi katika siku ya shida yao. 13Usiingie katika lango la watu wangu, siku ya msiba wao; naam, usiyatazame mateso yao, siku ya msiba wao; wala usitie mikono yako juu ya mali zao, siku ya msiba wao. 14#Isa 34:5-17; 63:1-6; Yer 49:7-22; Eze 25:12-14; 35:1-15; Amo 1:11-12; Mal 1:2-5 Wala usisimame penye njia panda, ili kuwakatilia mbali watu wake wakimbiao; wala usiwatoe watu wake waliosalia, katika siku ya dhiki. 15#Amu 1:7; Zab 137:8; Eze 35:15; Yoe 3:7,8 Kwa maana hiyo siku ya BWANA i karibu juu ya mataifa yote; kama ulivyotenda, ndivyo utakavyotendwa; malipo yako yatakurudia juu ya kichwa chako mwenyewe. 16Kwa maana kama vile mlivyokunywa juu ya mlima wangu mtakatifu, ndivyo mataifa yote watakavyokunywa daima; naam, watakunywa na kuyumbayumba, nao watakuwa kana kwamba hawakuwa kamwe.
Ushindi wa mwisho wa Israeli
17Bali katika mlima Sayuni kutakuwa na watakaookoka, nao utakuwa mtakatifu; na nyumba ya Yakobo watamiliki tena milki zao. 18Na nyumba ya Yakobo itakuwa moto, na nyumba ya Yusufu itakuwa muali wa moto, na nyumba ya Esau itakuwa mabua makavu, nao watawaka kati yao, na kuwateketeza; wala hatasalia mtu awaye yote katika nyumba ya Esau; kwa kuwa BWANA amesema hayo. 19#Sef 2:7 Na watu wa Negebu wataumiliki mlima wa Esau; na watu wa Shefela watawamiliki Wafilisti; nao wataimiliki nchi ya Efraimu, na nchi ya Samaria, na Benyamini atamiliki Gileadi. 20#1 Fal 17:9 Na watu wa jeshi hili la wana wa Israeli waliotekwa, walio kati ya Wakanaani, watamiliki mpaka Sarepta; na hao watu wa Yerusalemu waliotekwa, waliomo Sefaradi, wataimiliki miji ya Negebu. 21#Isa 19:20; Dan 2:24; Zek 14:9; Ufu 11:15 Tena waokoaji watakwea juu ya mlima Sayuni ili kuuhukumu mlima wa Esau; na huo ufalme utakuwa ni mali ya BWANA.

Iliyochaguliwa sasa

Obadia 1: SRUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha