Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 14:32-72

Marko 14:32-72 SRUV

Kisha wakaja mpaka katika bustani iitwayo Gethsemane; akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa pindi niombapo. Akamtwaa Petro na Yakobo na Yohana pamoja naye, akaanza kufadhaika sana na kuhangaika. Akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa mkeshe. Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akiomba ya kuwa, ikiwezekana, saa hiyo imwepuke. Akasema, Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; lakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe. Akaja akawakuta wamelala usingizi, akamwambia Petro, Je! Simoni, umelala? Hukuweza kukesha saa moja? Kesheni na kuomba, msije mkaingia majaribuni, roho i radhi ila mwili ni dhaifu. Akaenda zake tena, akaomba, akisema neno lilo hilo. Akaja tena akawakuta wamelala, maana macho yao yamekuwa mazito, wala hawakujua la kumjibu. Akaja mara ya tatu, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike; yatosha, saa imekuja; tazama, Mwana wa Adamu anatiwa mikononi mwao wenye dhambi. Ondokeni, twendeni zetu; tazama, yule anayenisaliti amekaribia. Basi alipokuwa katika kusema, mara Yuda alifika, mmoja wa wale Kumi na Wawili, na pamoja naye mkutano, wakiwa na panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani, na waandishi, na wazee. Na yule anayemsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni na kumpeleka chini ya ulinzi. Basi alipokuja, mara akamwendea, akasema, Rabi, akambusu. Wakanyosha mikono yao wakamkamata. Na mmoja wao waliokuwapo akafuta upanga, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio. Yesu akajibu, akawaambia, Je! Mmekuja na panga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyang'anyi? Kila siku nilikuwa mbele yenu hekaluni nikifundisha, msinikamate; lakini haya yamekuwa ili maandiko yapate kutimia. Ndipo wakamwacha, wakakimbia wote. Na kijana mmoja alimfuata, akiwa amejitanda mwili wake nguo ya kitani; wakamkamata; naye akaiacha ile nguo ya kitani, akakimbia akiwa uchi. Nao wakamchukua Yesu kwa Kuhani Mkuu; wakamkusanyikia wote, wakuu wa makuhani na wazee na waandishi. Naye Petro akamfuata kwa mbali, hadi ndani katika behewa ya Kuhani Mkuu; akawa ameketi pamoja na watumishi, akiota moto. Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda juu ya Yesu wapate kumwua; wasione. Kwa maana wengi walimshuhudia uongo, lakini ushuhuda wao haukupatana. Hata wengine wakasimama, wakamshuhudia uongo, wakisema, Sisi tulimsikia akisema, Mimi nitalivunja hekalu hili lililofanyika kwa mikono, na katika siku tatu nitajenga jingine lisilofanyika kwa mikono. Wala hata hivyo ushuhuda wao haukupatana. Kisha Kuhani Mkuu akasimama katikati, akamwuliza Yesu, akisema, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini? Lakini akanyamaza, wala hakujibu neno. Kuhani Mkuu akamwuliza tena, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wake Mtukufu? Yesu akasema, Mimi ndiye, nanyi mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kulia wa nguvu, akija na mawingu ya mbinguni. Kuhani Mkuu akararua nguo zake, akisema, Tuna haja gani tena ya mashahidi? Mmesikia kufuru yake; mwaonaje ninyi? Wote wakamhukumu kuwa imempasa kuuawa. Wengine wakaanza kumtemea mate, wakamfunika uso, na kumpiga makonde, na kumwambia, tabiri. Hata watumishi nao wakamchukua wakampiga makofi. Na Petro alikuwa chini behewani; akaja mmoja wa vijakazi wa Kuhani Mkuu, akamwona Petro akiota moto; akamkazia macho, akasema, Wewe nawe ulikuwapo pamoja na yule Mnazareti, Yesu. Akakana, akasema, Sijui wala sisikii unayoyasema wewe. Akatoka nje hadi ukumbini; jogoo akawika. Na yule kijakazi akamwona tena, akaanza tena kuwaambia waliosimama pale, Huyu ni mmoja wao. Akakana tena. Kitambo kidogo tena wale waliosimama pale wakamwambia Petro, Hakika u mmoja wao, kwa sababu u Mgalilaya wewe. Akaanza kulaani na kuapiza, Simjui mtu huyu mnayemnena. Na mara jogoo akawika mara ya pili. Petro akalikumbuka lile neno aliloambiwa na Yesu, Kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu. Na alipolifikiri, akalia.

Soma Marko 14