Marko 14:32-72
Marko 14:32-72 NEN
Wakaenda mahali paitwapo Gethsemane. Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa, nami niende nikaombe.” Kisha akawachukua pamoja naye Petro, Yakobo na Yohana. Akaanza kuhuzunika sana na kutaabika. Akawaambia, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa na mkeshe.” Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba kwamba kama ingewezekana saa hiyo ya mateso imwondokee. Akasema, “ Abba, Baba, mambo yote yawezekana kwako. Niondolee kikombe hiki. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali vile upendavyo wewe.” Akarudi kwa wanafunzi wake, akawakuta wamelala. Akamwambia Petro, “Simoni, umelala? Je, hukuweza kukesha hata kwa saa moja? Kesheni na mwombe, msije mkaingia majaribuni. Roho iko radhi, lakini mwili ni mdhaifu.” Akaenda tena kuomba, akisema maneno yale yale. Aliporudi, akawakuta tena wamelala kwa sababu macho yao yalikuwa mazito. Nao hawakujua la kumwambia. Akaja mara ya tatu, akawaambia, “Bado mmelala na kupumzika? Imetosha! Saa imewadia. Tazameni, Mwana wa Adamu anasalitiwa na kutiwa mikononi mwa wenye dhambi. Inukeni, twende zetu! Tazameni, msaliti wangu yuaja!” Yesu alipokuwa bado anazungumza, Yuda, mmoja wa wale wanafunzi Kumi na Wawili, akatokea. Alikuwa amefuatana na umati wa watu wenye panga na marungu, waliokuwa wametumwa na viongozi wa makuhani, walimu wa sheria, na wazee. Basi msaliti alikuwa amewapa hao watu ishara, kwamba: “Yule nitakayembusu ndiye. Mkamateni, mkamchukue chini ya ulinzi.” Mara Yuda akamjia Yesu na kusema, “Rabi.” Akambusu. Wale watu wakamkamata Yesu, wakamweka chini ya ulinzi. Ndipo mmoja wa wale waliokuwa wamesimama karibu aliuchomoa upanga wake na kumpiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio. Kisha Yesu akawaambia, “Mmekuja na panga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyangʼanyi? Siku kwa siku nilikuwa pamoja nanyi nikifundisha Hekaluni, wala hamkunikamata. Lakini Maandiko sharti yatimie.” Ndipo wanafunzi wake wote wakamwacha, wakakimbia. Kijana mmoja, ambaye hakuwa amevaa kitu isipokuwa alijitanda nguo ya kitani, alikuwa akimfuata Yesu. Walipomkamata, alikimbia uchi, akaliacha vazi lake. Wakampeleka Yesu kwa kuhani mkuu, nao viongozi wa makuhani wote, na wazee na walimu wa sheria wote wakakusanyika pamoja. Petro akamfuata kwa mbali, hadi uani kwa kuhani mkuu. Huko akaketi pamoja na walinzi, akiota moto. Viongozi wa makuhani na Baraza la Wayahudi lote wakatafuta ushahidi dhidi ya Yesu ili wapate kumuua. Lakini hawakupata jambo lolote. Wengi walitoa ushahidi wa uongo dhidi yake, lakini maelezo yao hayakukubaliana. Ndipo wengine wakasimama wakatoa ushahidi wa uongo dhidi yake, wakisema: “Sisi tulimsikia akisema, ‘Mimi nitalibomoa Hekalu hili lililojengwa na wanadamu, na katika siku tatu nitajenga jingine ambalo halikujengwa na wanadamu.’ ” Lakini hata hivyo, ushahidi wao haukukubaliana. Basi kuhani mkuu akasimama mbele yao, akamuuliza Yesu, “Je, wewe hutajibu? Ni ushahidi gani hawa watu wanauleta dhidi yako?” Lakini Yesu akakaa kimya, hakusema neno lolote. Kuhani mkuu akamuuliza tena, “Je, wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu Aliyebarikiwa?” Yesu akajibu, “Mimi ndimi. Nanyi mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kuume wa Mwenye Nguvu, na akija juu ya mawingu ya mbinguni.” Kuhani mkuu akararua mavazi yake, akasema, “Tuna haja gani tena ya mashahidi zaidi? Ninyi mmesikia hayo makufuru. Uamuzi wenu ni gani?” Wote wakamhukumu kwamba anastahili kifo. Kisha baadhi ya watu wakaanza kumtemea mate; wakamfunga kitambaa machoni, wakampiga kwa ngumi na kumwambia, “Tabiri!” Walinzi wakamchukua na kumpiga makofi. Petro alipokuwa bado yuko chini kwenye ua wa jumba la kifalme, tazama akaja mmoja wa watumishi wa kike wa kuhani mkuu. Alipomwona Petro akiota moto, akamtazama sana, akamwambia, “Wewe pia ulikuwa pamoja na Yesu, Mnazareti.” Lakini Petro akakana, akasema, “Sijui wala sielewi unalosema.” Naye akaondoka kuelekea kwenye njia ya kuingilia. Yule mtumishi wa kike alipomwona mahali pale, akawaambia tena wale waliokuwa wamesimama hapo, “Huyu mtu ni mmoja wao.” Lakini Petro akakana tena. Baada ya muda kidogo wale waliokuwa wamesimama hapo karibu na Petro wakamwambia, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana wewe pia ni Mgalilaya!” Petro akaanza kujilaani na kuwaapia, “Mimi simjui huyu mtu mnayesema habari zake!” Papo hapo jogoo akawika mara ya pili. Ndipo Petro akakumbuka lile neno Yesu alikuwa amemwambia: “Kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu.” Akavunjika moyo, akalia sana.