Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 14:32-72

Marko 14:32-72 Biblia Habari Njema (BHN)

Basi, wakafika katika bustani iliyoitwa Gethsemane. Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa wakati mimi nasali.” Kisha akawachukua Petro, Yakobo na Yohane; akaanza kufadhaika sana na kuhangaika. Akawaambia, “Nina huzuni kubwa moyoni hata karibu kufa. Kaeni hapa na kukesha.” Akaenda mbele kidogo, akajitupa chini kifudifudi, akasali kwamba, kama ingewezekana, asiipitie saa hiyo ya mateso. Akasema, “Baba yangu, kwako mambo yote yanawezekana. Uniondolee kikombe hiki; lakini isiwe kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe.” Kisha akarudi kwa wanafunzi wale watatu, akawakuta wamelala. Basi, akamwuliza Petro, “Simoni, je, umelala? Hukuweza kukesha hata saa moja?” Kisha akawaambia, “Kesheni na kusali ili msije mkaingia katika majaribu. Roho inataka, lakini mwili ni dhaifu.” Akaenda kusali tena akirudia maneno yaleyale. Kisha akarudi tena, akawakuta wamelala. Macho yao yalikuwa yamebanwa na usingizi. Hawakujua la kumjibu. Alipowajia mara ya tatu aliwaambia, “Mnalala bado na kupumzika? Sasa imetosha! Saa imefika! Mwana wa Mtu anakabidhiwa kwa watu waovu. Amkeni, twende zetu. Tazameni, yule atakayenisaliti amekaribia.” Yesu alipokuwa bado anasema, Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili, akafika pamoja na umati wa watu wenye mapanga na marungu. Watu hao walikuwa wametumwa na makuhani wakuu, waalimu wa sheria na wazee. Msaliti Yuda alikuwa amewapa ishara: “Yule nitakayembusu ndiye; mkamateni na kumpeleka chini ya ulinzi.” Yuda alipofika tu, alimwendea Yesu moja kwa moja, akamwambia, “Mwalimu!” Kisha akambusu. Basi, hao watu wakamkamata Yesu, wakamtia nguvuni. Mmoja wa wale waliokuwa wamesimama hapo pamoja na Yesu, akachomoa upanga wake, akampiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio. Yesu akawaambia, “Je, mmekuja na mapanga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyanganyi? Kila siku nilikuwa pamoja nanyi nikifundisha hekaluni, wala hamkunikamata. Lakini sasa lazima Maandiko Matakatifu yatimie.” Hapo wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia. Kulikuwa na kijana mmoja aliyekuwa anamfuata Yesu akiwa amevaa shuka. Nao wakajaribu kumkamata. Lakini yeye akaponyoka, akaiachilia ile shuka, akakimbia uchi. Basi, wakampeleka Yesu kwa kuhani mkuu ambapo makuhani wakuu wote, wazee na waalimu wa sheria walikuwa wamekutanika. Petro alimfuata Yesu kwa mbali, akaingia ndani ya ua wa kuhani mkuu, akaketi pamoja na walinzi akiota moto. Makuhani wakuu na Baraza lote wakatafuta ushahidi wa kumshtaki Yesu wapate kumwua, lakini hawakuupata. Watu wengi walitoa ushahidi wa uongo juu ya Yesu, lakini ushahidi wao haukupatana. Kisha wengine walisimama, wakatoa ushahidi wa uongo wakisema: “Tulimsikia mtu huyu akisema, ‘Nitaliharibu hekalu hili lililojengwa kwa mikono, na kwa siku tatu nitajenga lingine lisilojengwa kwa mikono.’” Lakini hata hivyo, ushahidi wao haukupatana. Basi, kuhani mkuu akasimama katikati yao, akamwuliza Yesu, “Je, hujibu neno? Watu hawa wanashuhudia nini dhidi yako?” Lakini yeye akakaa kimya; hakusema hata neno moja. Kuhani mkuu akamwuliza tena, “Je, wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu Mtukufu?” Yesu akajibu, “Naam, mimi ndiye. Tena, mtamwona Mwana wa Mtu amekaa upande wa kulia wa yule Bwana Mwenye Nguvu, akija katika mawingu ya mbinguni.” Hapo kuhani mkuu akararua joho lake, akasema, “Tuna haja gani tena ya mashahidi? Mmesikia kufuru yake! Nyinyi mwaonaje?” Wote wakaamua kwamba anastahili kuuawa. Basi, baadhi yao wakaanza kumtemea mate, wakamfunika uso, wakampiga na kumwambia, “Bashiri ni nani amekupiga!” Hata watumishi wakamchukua, wakampiga makofi. Petro alipokuwa bado chini uani, mmoja wa watumishi wa kike wa kuhani mkuu alikuja. Alipomwona Petro akiota moto, alimtazama, akamwambia, “Hata wewe ulikuwa pamoja na Yesu Mnazareti.” Lakini Petro akakana, “Sijui, wala sielewi unayosema!” Kisha Petro akaondoka, akaenda nje uani. Hapo jogoo akawika. Yule mtumishi alipomwona tena Petro, akaanza tena kuwaambia watu waliokuwa wamesimama hapo, “Mtu huyu ni mmoja wao.” Petro akakana tena. Baadaye kidogo, watu waliokuwa wamesimama hapo wakamwambia Petro, “Hakika wewe ni mmoja wao, maana wewe ni Mgalilaya.” Lakini Petro akaanza kulaani na kuapa akisema, “Mimi simjui mtu huyu mnayesema habari zake.” Hapo jogoo akawika mara ya pili. Basi, Petro akakumbuka jinsi Yesu alivyokuwa amemwambia: “Kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu.” Petro akabubujika machozi.

Shirikisha
Soma Marko 14

Marko 14:32-72 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kisha wakaja mpaka katika bustani iitwayo Gethsemane; akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa pindi niombapo. Akamtwaa Petro na Yakobo na Yohana pamoja naye, akaanza kufadhaika sana na kuhangaika. Akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa mkeshe. Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akiomba ya kuwa, ikiwezekana, saa hiyo imwepuke. Akasema, Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; lakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe. Akaja akawakuta wamelala usingizi, akamwambia Petro, Je! Simoni, umelala? Hukuweza kukesha saa moja? Kesheni na kuomba, msije mkaingia majaribuni, roho i radhi ila mwili ni dhaifu. Akaenda zake tena, akaomba, akisema neno lilo hilo. Akaja tena akawakuta wamelala, maana macho yao yamekuwa mazito, wala hawakujua la kumjibu. Akaja mara ya tatu, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike; yatosha, saa imekuja; tazama, Mwana wa Adamu anatiwa mikononi mwao wenye dhambi. Ondokeni, twendeni zetu; tazama, yule anayenisaliti amekaribia. Basi alipokuwa katika kusema, mara Yuda alifika, mmoja wa wale Kumi na Wawili, na pamoja naye mkutano, wakiwa na panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani, na waandishi, na wazee. Na yule anayemsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni na kumpeleka chini ya ulinzi. Basi alipokuja, mara akamwendea, akasema, Rabi, akambusu. Wakanyosha mikono yao wakamkamata. Na mmoja wao waliokuwapo akafuta upanga, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio. Yesu akajibu, akawaambia, Je! Mmekuja na panga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyang'anyi? Kila siku nilikuwa mbele yenu hekaluni nikifundisha, msinikamate; lakini haya yamekuwa ili maandiko yapate kutimia. Ndipo wakamwacha, wakakimbia wote. Na kijana mmoja alimfuata, akiwa amejitanda mwili wake nguo ya kitani; wakamkamata; naye akaiacha ile nguo ya kitani, akakimbia akiwa uchi. Nao wakamchukua Yesu kwa Kuhani Mkuu; wakamkusanyikia wote, wakuu wa makuhani na wazee na waandishi. Naye Petro akamfuata kwa mbali, hadi ndani katika behewa ya Kuhani Mkuu; akawa ameketi pamoja na watumishi, akiota moto. Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda juu ya Yesu wapate kumwua; wasione. Kwa maana wengi walimshuhudia uongo, lakini ushuhuda wao haukupatana. Hata wengine wakasimama, wakamshuhudia uongo, wakisema, Sisi tulimsikia akisema, Mimi nitalivunja hekalu hili lililofanyika kwa mikono, na katika siku tatu nitajenga jingine lisilofanyika kwa mikono. Wala hata hivyo ushuhuda wao haukupatana. Kisha Kuhani Mkuu akasimama katikati, akamwuliza Yesu, akisema, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini? Lakini akanyamaza, wala hakujibu neno. Kuhani Mkuu akamwuliza tena, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wake Mtukufu? Yesu akasema, Mimi ndiye, nanyi mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kulia wa nguvu, akija na mawingu ya mbinguni. Kuhani Mkuu akararua nguo zake, akisema, Tuna haja gani tena ya mashahidi? Mmesikia kufuru yake; mwaonaje ninyi? Wote wakamhukumu kuwa imempasa kuuawa. Wengine wakaanza kumtemea mate, wakamfunika uso, na kumpiga makonde, na kumwambia, tabiri. Hata watumishi nao wakamchukua wakampiga makofi. Na Petro alikuwa chini behewani; akaja mmoja wa vijakazi wa Kuhani Mkuu, akamwona Petro akiota moto; akamkazia macho, akasema, Wewe nawe ulikuwapo pamoja na yule Mnazareti, Yesu. Akakana, akasema, Sijui wala sisikii unayoyasema wewe. Akatoka nje hadi ukumbini; jogoo akawika. Na yule kijakazi akamwona tena, akaanza tena kuwaambia waliosimama pale, Huyu ni mmoja wao. Akakana tena. Kitambo kidogo tena wale waliosimama pale wakamwambia Petro, Hakika u mmoja wao, kwa sababu u Mgalilaya wewe. Akaanza kulaani na kuapiza, Simjui mtu huyu mnayemnena. Na mara jogoo akawika mara ya pili. Petro akalikumbuka lile neno aliloambiwa na Yesu, Kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu. Na alipolifikiri, akalia.

Shirikisha
Soma Marko 14

Marko 14:32-72 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kisha wakaja mpaka bustani iitwayo Gethsemane; akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa muda niombapo. Akamtwaa Petro na Yakobo na Yohana pamoja naye, akaanza kufadhaika sana na kuhangaika. Akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa mkeshe. Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akiomba ya kuwa, ikiwezekana, saa hiyo imwepuke. Akasema, Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; walakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe. Akaja akawakuta wamelala usingizi, akamwambia Petro, Je! Simoni, umelala? Hukuweza kukesha saa moja? Kesheni mwombe, msije mkaingia majaribuni, roho i radhi ila mwili ni dhaifu. Akaenda zake tena, akaomba, akisema neno lilo hilo. Akaja tena akawakuta wamelala, maana macho yao yamekuwa mazito, wala hawakujua la kumjibu. Akaja mara ya tatu, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike; yatosha, saa imekuja; tazama, Mwana wa Adamu anatiwa mikononi mwao wenye dhambi. Ondokeni, twendeni zetu; tazama, yule anayenisaliti amekaribia. Basi alipokuwa katika kusema, mara Yuda alifika, mmoja wa wale Thenashara, na pamoja naye mkutano, wana panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani, na waandishi, na wazee. Na yule anayemsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni, mkamchukue salama. Basi alipokuja, mara akamwendea, akasema, Rabi, akambusu. Wakanyosha mikono yao wakamkamata. Na mmoja wao waliokuwapo akafuta upanga, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio. Yesu akajibu, akawaambia, Je! Ni kama juu ya mnyang’anyi mmetoka wenye panga na marungu, kunitwaa mimi? Kila siku nalikuwa mbele yenu hekaluni nikifundisha, msinikamate; lakini haya yamekuwa ili maandiko yapate kutimia. Ndipo wakamwacha, wakakimbia wote. Na kijana mmoja alimfuata, amejitanda mwili wake nguo ya kitani; wakamkamata; naye akaiacha ile nguo ya kitani, akakimbia yu uchi. Nao wakamchukua Yesu kwa Kuhani Mkuu; wakamkusanyikia wote, wakuu wa makuhani na wazee na waandishi. Naye Petro akamfuata kwa mbali, hata ndani katika behewa ya Kuhani Mkuu; akawa ameketi pamoja na watumishi, anakota moto mwangani. Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda juu ya Yesu wapate kumwua; wasione. Kwa maana wengi walimshuhudia uongo, walakini ushuhuda wao haukupatana. Hata wengine wakasimama, wakamshuhudia uongo, wakisema, Sisi tulimsikia akisema, Mimi nitalivunja hekalu hili lililofanyika kwa mikono, na katika siku tatu nitajenga jingine lisilofanyika kwa mikono. Wala hata hivi ushuhuda wao haukupatana. Kisha Kuhani Mkuu akasimama katikati, akamwuliza Yesu, akisema, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini? Lakini akanyamaza, wala hakujibu neno. Kuhani Mkuu akamwuliza tena, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wake Mtukufu? Yesu akasema, Mimi ndiye, nanyi mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija na mawingu ya mbinguni. Kuhani Mkuu akararua nguo zake, akisema, Tuna haja gani tena ya mashahidi? Mmesikia kufuru yake; mwaonaje ninyi? Wote wakamhukumu kuwa imempasa kuuawa. Wengine wakaanza kumtemea mate, wakamfunika uso, na kumpiga makonde, na kumwambia, tabiri. Hata watumishi nao wakampiga makofi. Na Petro alikuwa chini behewani; akaja mmoja wa vijakazi wa Kuhani Mkuu, akamwona Petro akikota moto; akamkazia macho, akasema, Wewe nawe ulikuwapo pamoja na yule Mnazareti, Yesu. Akakana, akasema, Sijui wala sisikii unayoyasema wewe. Akatoka nje hata ukumbini; jogoo akawika. Na yule kijakazi akamwona tena, akaanza tena kuwaambia waliosimama pale, Huyu ni mmoja wao. Akakana tena. Kitambo kidogo tena wale waliosimama pale wakamwambia Petro, Hakika u mmoja wao, kwa sababu u Mgalilaya wewe. Akaanza kulaani na kuapiza, Simjui mtu huyu mnayemnena. Na mara jogoo akawika mara ya pili. Petro akalikumbuka lile neno aliloambiwa na Yesu, Kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu. Na alipolifikiri, akalia. a.

Shirikisha
Soma Marko 14

Marko 14:32-72 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Wakaenda mahali paitwapo Gethsemane. Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa, nami niende nikaombe.” Kisha akawachukua pamoja naye Petro, Yakobo na Yohana. Akaanza kuhuzunika sana na kutaabika. Akawaambia, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa na mkeshe.” Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba kwamba kama ingewezekana saa hiyo ya mateso imwondokee. Akasema, “ Abba, Baba, mambo yote yawezekana kwako. Niondolee kikombe hiki. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali vile upendavyo wewe.” Akarudi kwa wanafunzi wake, akawakuta wamelala. Akamwambia Petro, “Simoni, umelala? Je, hukuweza kukesha hata kwa saa moja? Kesheni na mwombe, msije mkaingia majaribuni. Roho iko radhi, lakini mwili ni mdhaifu.” Akaenda tena kuomba, akisema maneno yale yale. Aliporudi, akawakuta tena wamelala kwa sababu macho yao yalikuwa mazito. Nao hawakujua la kumwambia. Akaja mara ya tatu, akawaambia, “Bado mmelala na kupumzika? Imetosha! Saa imewadia. Tazameni, Mwana wa Adamu anasalitiwa na kutiwa mikononi mwa wenye dhambi. Inukeni, twende zetu! Tazameni, msaliti wangu yuaja!” Yesu alipokuwa bado anazungumza, Yuda, mmoja wa wale wanafunzi Kumi na Wawili, akatokea. Alikuwa amefuatana na umati wa watu wenye panga na marungu, waliokuwa wametumwa na viongozi wa makuhani, walimu wa sheria, na wazee. Basi msaliti alikuwa amewapa hao watu ishara, kwamba: “Yule nitakayembusu ndiye. Mkamateni, mkamchukue chini ya ulinzi.” Mara Yuda akamjia Yesu na kusema, “Rabi.” Akambusu. Wale watu wakamkamata Yesu, wakamweka chini ya ulinzi. Ndipo mmoja wa wale waliokuwa wamesimama karibu aliuchomoa upanga wake na kumpiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio. Kisha Yesu akawaambia, “Mmekuja na panga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyangʼanyi? Siku kwa siku nilikuwa pamoja nanyi nikifundisha Hekaluni, wala hamkunikamata. Lakini Maandiko sharti yatimie.” Ndipo wanafunzi wake wote wakamwacha, wakakimbia. Kijana mmoja, ambaye hakuwa amevaa kitu isipokuwa alijitanda nguo ya kitani, alikuwa akimfuata Yesu. Walipomkamata, alikimbia uchi, akaliacha vazi lake. Wakampeleka Yesu kwa kuhani mkuu, nao viongozi wa makuhani wote, na wazee na walimu wa sheria wote wakakusanyika pamoja. Petro akamfuata kwa mbali, hadi uani kwa kuhani mkuu. Huko akaketi pamoja na walinzi, akiota moto. Viongozi wa makuhani na Baraza la Wayahudi lote wakatafuta ushahidi dhidi ya Yesu ili wapate kumuua. Lakini hawakupata jambo lolote. Wengi walitoa ushahidi wa uongo dhidi yake, lakini maelezo yao hayakukubaliana. Ndipo wengine wakasimama wakatoa ushahidi wa uongo dhidi yake, wakisema: “Sisi tulimsikia akisema, ‘Mimi nitalibomoa Hekalu hili lililojengwa na wanadamu, na katika siku tatu nitajenga jingine ambalo halikujengwa na wanadamu.’ ” Lakini hata hivyo, ushahidi wao haukukubaliana. Basi kuhani mkuu akasimama mbele yao, akamuuliza Yesu, “Je, wewe hutajibu? Ni ushahidi gani hawa watu wanauleta dhidi yako?” Lakini Yesu akakaa kimya, hakusema neno lolote. Kuhani mkuu akamuuliza tena, “Je, wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu Aliyebarikiwa?” Yesu akajibu, “Mimi ndimi. Nanyi mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kuume wa Mwenye Nguvu, na akija juu ya mawingu ya mbinguni.” Kuhani mkuu akararua mavazi yake, akasema, “Tuna haja gani tena ya mashahidi zaidi? Ninyi mmesikia hayo makufuru. Uamuzi wenu ni gani?” Wote wakamhukumu kwamba anastahili kifo. Kisha baadhi ya watu wakaanza kumtemea mate; wakamfunga kitambaa machoni, wakampiga kwa ngumi na kumwambia, “Tabiri!” Walinzi wakamchukua na kumpiga makofi. Petro alipokuwa bado yuko chini kwenye ua wa jumba la kifalme, tazama akaja mmoja wa watumishi wa kike wa kuhani mkuu. Alipomwona Petro akiota moto, akamtazama sana, akamwambia, “Wewe pia ulikuwa pamoja na Yesu, Mnazareti.” Lakini Petro akakana, akasema, “Sijui wala sielewi unalosema.” Naye akaondoka kuelekea kwenye njia ya kuingilia. Yule mtumishi wa kike alipomwona mahali pale, akawaambia tena wale waliokuwa wamesimama hapo, “Huyu mtu ni mmoja wao.” Lakini Petro akakana tena. Baada ya muda kidogo wale waliokuwa wamesimama hapo karibu na Petro wakamwambia, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana wewe pia ni Mgalilaya!” Petro akaanza kujilaani na kuwaapia, “Mimi simjui huyu mtu mnayesema habari zake!” Papo hapo jogoo akawika mara ya pili. Ndipo Petro akakumbuka lile neno Yesu alikuwa amemwambia: “Kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu.” Akavunjika moyo, akalia sana.

Shirikisha
Soma Marko 14