Marko 14:1-26
Marko 14:1-26 SRUV
Baada ya siku mbili ilikuwa sikukuu ya Pasaka, na mikate isiyochachwa; wakuu wa makuhani na waandishi wakatafuta njia ya kumkamata kwa hila na kumwua. Kwa maana walisema, Isiwe kwa wakati wa sikukuu, isije ikatokea ghasia katika watu. Naye alipokuwapo Bethania, nyumbani mwa Simoni mwenye ukoma, akiwa amekaa mezani, alikuja mwanamke mwenye chupa ya marhamu yenye manukato ya nardo safi ya thamani kubwa; akaivunja chupa akaimimina kichwani pake. Palikuwa na watu waliochukizwa katika nafsi zao wakisema, Kwa nini kupoteza marhamu namna hii? Maana marhamu hii ingaliweza kuuzwa kwa dinari mia tatu na kuzidi, wakapewa maskini. Wakamnung'unikia sana yule mwanamke. Yesu akasema, Mwacheni; mbona mnamsumbua? Amenitendea kazi njema; maana sikuzote mnao maskini pamoja nanyi, na kila mpendapo mwaweza kuwatendea mema; lakini mimi hamko nami sikuzote. Ametenda alivyoweza; ametangulia kuupaka mwili wangu marhamu kwa ajili ya maziko. Amin, nawaambia, Kila ihubiriwapo Injili katika ulimwengu wote, na hili alilotenda huyu litatajwa kwa kumbukumbu lake. Yuda Iskarioti, yule mmoja katika wale Kumi na Wawili, akaenda zake kwa wakuu wa makuhani, apate kumsaliti kwao. Nao waliposikia walifurahi, wakaahidi kumpa fedha. Akatafuta njia ya kumsaliti wakati wa kufaa. Katika siku ya kwanza ya mikate isiyochachwa, walipoichinja Pasaka, wanafunzi wake wakamwambia, Ni wapi utakapo tuende tukuandalie uile Pasaka? Akatuma wawili katika wanafunzi wake, akawaambia, Nendeni zenu mjini; atakutana nanyi mwanamume amebeba mtungi wa maji; mfuateni; na popote atakapoingia, mwambieni mwenye nyumba, Mwalimu asema, Kiko wapi chumba changu cha wageni, niile Pasaka humo, pamoja na wanafunzi wangu? Naye mwenyewe atawaonesha ghorofa kubwa, iliyotayarishwa; humo tuandalieni. Wanafunzi wakatoka, wakaenda mjini, wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa Pasaka. Basi ilipokuwa jioni akaja pamoja na wale Kumi na Wawili. Nao walipokuwa wameketi chakulani, wakila, Yesu alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu, naye anakula pamoja nami, atanisaliti. Wakaanza kuhuzunika, wakamwambia mmoja mmoja, Je! Ni mimi? Akawaambia, Ni mmoja wa hao Kumi na Wawili, ambaye achovya pamoja nami katika kombe. Kwa maana Mwana wa Adamu aenda zake kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu; ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa. Nao walipokuwa wakila, alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa, akasema, Twaeni; huu ndio mwili wangu. Akatwaa kikombe, akashukuru, akawapa; wakakinywea wote. Akawaambia, Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi. Amin, nawaambia ninyi, Sitakunywa tena kabisa uzao wa mzabibu, hata siku ile nitakapounywa mpya katika ufalme wa Mungu. Nao walipokwisha kuimba walitoka kwenda katika mlima wa Mizeituni.