Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 27:32-66

Mathayo 27:32-66 SRUV

Walipokuwa wakitoka, wakamwona mtu Mkirene, jina lake Simoni; huyu wakamshurutisha auchukue msalaba wake. Na walipofika mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la Kichwa, wakampa kunywa divai iliyochanganyika na nyongo; lakini yeye alipoionja hakutaka kunywa. Walipokwisha kumsulubisha, waligawana mavazi yake, kwa kupiga kura; [ili litimie neno lililonenwa na nabii, Waligawa nguo zangu kati yao, na juu ya vazi langu walipiga kura.] Wakaketi, wakamlinda huko. Wakaweka juu ya kichwa chake mashitaka yake, yaliyoandikwa HUYU NI YESU, MFALME WA WAYAHUDI. Wakati uo huo wanyang'anyi wawili wakasulubiwa pamoja naye, mmoja katika mkono wake wa kulia, na mmoja katika mkono wake wa kushoto. Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisatikisa vichwa vyao, wakisema, Ewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe nafsi yako; ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, shuka msalabani. Kadhalika na wale wakuu wa makuhani wakamdhihaki pamoja na waandishi na wazee, wakisema, Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe. Yeye ni mfalme wa Israeli; na ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini. Amemtegemea Mungu; na amwokoe sasa, kama anamtaka; kwa maana alisema, Mimi ni Mwana wa Mungu. Pia wale wanyang'anyi waliosulubiwa pamoja naye walimshutumu vile vile. Basi tangu saa sita palikuwa na giza juu ya nchi yote hadi saa tisa. Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Na baadhi yao waliokuweko, waliposikia, walisema, Huyu anamwita Eliya. Mara mmoja wao akaenda mbio, akatwaa sifongo, akaijaza siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha. Wale wengine wakasema, Acha; na tuone kama Eliya anakuja kumwokoa. Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake. Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hadi chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala; nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi. Basi yule afisa, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la ardhi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu. Palikuwa na wanawake wengi pale wakitazama kwa mbali, hao ndio waliomfuata Yesu toka Galilaya, na kumtumikia. Miongoni mwao alikuwamo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo na Yusufu, na mama yao wana wa Zebedayo. Na ilipokuwa jioni akafika mtu tajiri wa Arimathaya, jina lake Yusufu, naye mwenyewe alikuwa mwanafunzi wa Yesu; mtu huyu alimwendea Pilato akaomba apewe mwili wa Yesu. Ndipo Pilato akaamuru apewe. Yusufu akautwaa mwili, akauzongazonga katika sanda ya kitani safi, akauweka katika kaburi lake jipya, alilokuwa amelichonga mwambani; akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango wa kaburi, akaenda zake. Na pale walikuwapo Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, wameketi kulielekea kaburi. Hata siku ya pili, ndiyo iliyo baada ya Maandalio, wakuu wa makuhani, na Mafarisayo wakamkusanyikia Pilato, wakasema, Bwana, tumekumbuka kwamba yule mjanja alisema, alipokuwa angali hai, Baada ya siku tatu nitafufuka. Basi amuru kwamba kaburi lilindwe salama hadi siku ya tatu; wasije wanafunzi wake wakamwiba, na kuwaambia watu, Amefufuka katika wafu; na udanganyifu wa mwisho utapita ule wa kwanza. Pilato akawaambia, Mna askari; nendeni mkalilinde salama kadiri mjuavyo. Wakaenda, wakalilinda kaburi salama, kwa kulitia lile jiwe mhuri, pamoja na kuwaweka wale askari walinzi.

Soma Mathayo 27