Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 24:15-28

Mathayo 24:15-28 SRUV

Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu), ndipo walio katika Yudea na wakimbilie milimani; naye aliye juu ya dari asishuke kuvichukua vitu vilivyomo nyumbani mwake; wala aliye shambani asirudi nyuma kuichukua nguo yake. Ole wao wenye mimba na wanyonyeshao siku hizo! Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato. Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe. Na kama siku hizo zisingalifupishwa, asingeokoka mtu yeyote; lakini kwa ajili ya wateule siku hizo zitafupishwa. Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki. Kwa maana watatokea Makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, ikiwezekana, hata walio wateule. Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele. Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki. Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa kuwa popote ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai.

Soma Mathayo 24