Mathayo 24:15-28
Mathayo 24:15-28 Biblia Habari Njema (BHN)
“Basi, mtakapoona ‘Chukizo Haribifu lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu, (msomaji na atambue maana yake), hapo, walioko Yudea na wakimbilie milimani. Aliye juu ya paa la nyumba yake asishuke kuchukua kitu nyumbani mwake. Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake. Ole wao kina mama waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo! Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe siku za baridi au siku ya Sabato! Maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo wa ulimwengu mpaka leo, wala haitapata kutokea tena. Kama siku hizo hazingalipunguzwa, hakuna binadamu yeyote ambaye angeokoka; lakini siku hizo zitapunguzwa kwa ajili ya wale walioteuliwa. “Basi, mtu akiwaambieni siku hizo: ‘Kristo yuko hapa’ au ‘Yuko pale,’ msimsadiki. Maana watatokea akina Kristo wa uongo na manabii wa uongo. Watafanya ishara kubwa na maajabu ya kuweza kuwapotosha ikiwezekana hata wateule wa Mungu. Sikilizeni, nimekwisha waonya kabla ya wakati. Basi, wakiwaambieni, ‘Tazameni, yuko jangwani,’ msiende huko; au, ‘Tazameni, amejificha ndani,’ msisadiki; maana, kama vile umeme uangazavyo toka mashariki hadi magharibi, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu. Pale ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai.
Mathayo 24:15-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu), ndipo walio katika Yudea na wakimbilie milimani; naye aliye juu ya dari asishuke kuvichukua vitu vilivyomo nyumbani mwake; wala aliye shambani asirudi nyuma kuichukua nguo yake. Ole wao wenye mimba na wanyonyeshao siku hizo! Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato. Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe. Na kama siku hizo zisingalifupishwa, asingeokoka mtu yeyote; lakini kwa ajili ya wateule siku hizo zitafupishwa. Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki. Kwa maana watatokea Makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, ikiwezekana, hata walio wateule. Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele. Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki. Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa kuwa popote ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai.
Mathayo 24:15-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu), ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani; naye aliye juu ya dari asishuke kuvichukua vitu vilivyomo nyumbani mwake; wala aliye shambani asirudi nyuma kuichukua nguo yake. Ole wao wenye mimba na wanyonyeshao siku hizo! Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato. Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe. Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo. Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki. Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule. Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele. Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki. Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa kuwa po pote ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai.
Mathayo 24:15-28 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Hivyo mtakapoona lile ‘chukizo la uharibifu’ lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu (asomaye na afahamu), basi wale walioko Uyahudi wakimbilie milimani. Yeyote aliye juu ya dari ya nyumba asishuke ili kuchukua chochote kutoka ndani ya nyumba. Aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua vazi lake. Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo! Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi au siku ya Sabato. Kwa maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo wa dunia mpaka sasa: wala haitakuwako tena kamwe. Kama siku hizo zisingefupishwa, hakuna hata mtu mmoja ambaye angeokoka. Lakini kwa ajili ya wateule, siku hizo zitafupizwa. Wakati huo kama mtu yeyote akiwaambia, ‘Tazama, Kristo huyu hapa!’ Au, ‘Kristo yuko kule,’ msisadiki. Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara kubwa na maajabu mengi ili kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale wateule hasa. Angalieni, nimekwisha kuwaambia mapema. “Kwa hiyo mtu yeyote akiwaambia, ‘Yule kule nyikani,’ msiende huko. Au akisema, ‘Yuko kwenye chumba,’ msisadiki. Kwa maana kama vile umeme utokeavyo mashariki na kuonekana hata magharibi, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa maana popote ulipo mzoga, huko ndiko wakusanyikapo tai.