Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 12:22-37

Mathayo 12:22-37 SRUV

Wakati ule akaletewa mtu mwenye pepo, kipofu, naye ni bubu; akamponya, hata yule bubu akanena na kuona. Makutano wote wakashangaa, wakasema, Huyu siye mwana wa Daudi? Lakini Mafarisayo waliposikia, walisema, Huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa pepo. Basi Yesu akijua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, hufanyika ukiwa; tena mji au nyumba yoyote ikifitinika juu ya nafsi yake, haitasimama. Na Shetani akimtoa Shetani, amefitinika juu ya nafsi yake; basi ufalme wake utasimamaje? Na mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, je! Wana wenu huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo hao ndio watakaowahukumu. Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajia. Ama awezaje mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuviteka vyombo vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Ndipo atakapoiteka nyumba yake. Mtu asiye pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya. Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa. Naye mtu yeyote atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao. Ufanyeni mti kuwa mzuri na matunda yake kuwa mazuri; au ufanyeni mti kuwa mbaya na matunda yake mabaya, kwa maana kwa matunda yake mti hutambulikana. Enyi wazawa wa nyoka, mwawezaje kunena mema, mkiwa wabaya? Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake. Mtu mwema katika akiba njema hutoa mema; na mtu mbaya katika akiba mbaya hutoa mabaya. Basi, nawaambia, Kila neno lisilo maana, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu. Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.

Soma Mathayo 12