Mathayo 12:22-37
Mathayo 12:22-37 Biblia Habari Njema (BHN)
Hapo watu wakamletea Yesu mtu mmoja kipofu na ambaye alikuwa bubu kwa sababu alikuwa amepagawa na pepo. Yesu akamponya hata akaweza kusema na kuona. Umati wote wa watu ulishangaa ukasema, “Je, huenda ikawa huyu ndiye Mwana wa Daudi?” Lakini Mafarisayo waliposikia hayo, wakasema, “Mtu huyu anawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo.” Yesu, akiwa anayajua mawazo yao, akawaambia, “Ufalme wowote uliogawanyika makundimakundi yanayopingana, hauwezi kudumu, na mji wowote au jamaa yoyote iliyogawanyika makundimakundi yanayopingana, itaanguka. Ikiwa Shetani anamfukuza Shetani, anajipinga mwenyewe. Basi, ufalme wake utasimamaje? Nyinyi mnasema ati nawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli; je, wafuasi wenu huwafukuza kwa uwezo wa nani? Kwa sababu hiyo wao ndio watakaowahukumu nyinyi. Lakini ikiwa ninawafukuza pepo kwa nguvu ya Roho wa Mungu, basi jueni kwamba ufalme wa Mungu umekwisha fika kwenu. “Au, anawezaje mtu kuivamia nyumba ya mtu mwenye nguvu na kumnyanganya mali yake, bila kwanza kumfunga huyo mtu mwenye nguvu? Hapo ndipo atakapoweza kumnyanganya mali yake. “Yeyote asiyejiunga nami, ananipinga; na yeyote asiyekusanya pamoja nami, hutawanya. Kwa sababu hiyo, nawaambieni, watu watasamehewa dhambi na kufuru zao zote, lakini hawatasamehewa dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu. Tena, asemaye neno la kumpinga Mwana wa Mtu atasamehewa, lakini yule asemaye neno la kumpinga Roho Mtakatifu, hatasamehewa, wala katika ulimwengu huu, wala katika ulimwengu ujao. “Ufanyeni mti kuwa mzuri na matunda yake yatakuwa mazuri; ufanyeni kuwa mbaya na matunda yake yatakuwa mabaya. Mti hujulikana kwa matunda yake. Enyi kizazi cha nyoka! Mnawezaje kusema mambo mema hali nyinyi ni waovu? Maana mtu husema kutokana na yale yaliyojaa moyoni. Mtu mwema hutoa mambo mema katika hazina yake njema; na mtu mbaya hutoa mambo mabaya katika hazina yake mbaya. “Basi, nawaambieni, siku ya hukumu watu watapaswa kujibu juu ya kila neno lisilofaa wanalosema. Maana kwa maneno yako utakubaliwa kuwa mwadilifu, na kwa maneno yako utahukumiwa kuwa na hatia.”
Mathayo 12:22-37 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wakati ule akaletewa mtu mwenye pepo, kipofu, naye ni bubu; akamponya, hata yule bubu akanena na kuona. Makutano wote wakashangaa, wakasema, Huyu siye mwana wa Daudi? Lakini Mafarisayo waliposikia, walisema, Huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa pepo. Basi Yesu akijua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, hufanyika ukiwa; tena mji au nyumba yoyote ikifitinika juu ya nafsi yake, haitasimama. Na Shetani akimtoa Shetani, amefitinika juu ya nafsi yake; basi ufalme wake utasimamaje? Na mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, je! Wana wenu huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo hao ndio watakaowahukumu. Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajia. Ama awezaje mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuviteka vyombo vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Ndipo atakapoiteka nyumba yake. Mtu asiye pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya. Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa. Naye mtu yeyote atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao. Ufanyeni mti kuwa mzuri na matunda yake kuwa mazuri; au ufanyeni mti kuwa mbaya na matunda yake mabaya, kwa maana kwa matunda yake mti hutambulikana. Enyi wazawa wa nyoka, mwawezaje kunena mema, mkiwa wabaya? Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake. Mtu mwema katika akiba njema hutoa mema; na mtu mbaya katika akiba mbaya hutoa mabaya. Basi, nawaambia, Kila neno lisilo maana, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu. Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.
Mathayo 12:22-37 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wakati ule akaletewa mtu mwenye pepo, kipofu, naye ni bubu; akamponya, hata yule bubu akanena na kuona. Makutano wote wakashangaa, wakasema, Huyu siye mwana wa Daudi? Lakini Mafarisayo waliposikia, walisema, Huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa pepo. Basi Yesu akijua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, hufanyika ukiwa; tena mji au nyumba yo yote ikifitinika juu ya nafsi yake, haitasimama. Na Shetani akimtoa Shetani, amefitinika juu ya nafsi yake; basi ufalme wake utasimamaje? Na mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, je! Wana wenu huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo hao ndio watakaowahukumu. Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia. Ama awezaje mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuviteka vyombo vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Ndipo atakapoiteka nyumba yake. Mtu asiye pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya. Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa. Naye mtu ye yote atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao. Ufanyeni mti kuwa mzuri na matunda yake kuwa mazuri; au ufanyeni mti kuwa mbaya na matunda yake mabaya, kwa maana kwa matunda yake mti hutambulikana. Enyi wazao wa nyoka, mwawezaje kunena mema, mkiwa wabaya? Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake. Mtu mwema katika akiba njema hutoa mema; na mtu mbaya katika akiba mbaya hutoa mabaya. Basi, nawaambia, Kila neno lisilo maana, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu. Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.
Mathayo 12:22-37 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha wakamletea mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, na alikuwa kipofu na bubu. Yesu akamponya, hata akaweza kusema na kuona. Watu wote wakashangaa na kusema, “Je, yawezekana huyu ndiye Mwana wa Daudi?” Lakini Mafarisayo waliposikia jambo hili wakasema, “Mtu huyu anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo wachafu.” Yesu alijua walichokuwa wakiwaza, hivyo akawaambia, “Kila ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe huangamia. Hali kadhalika kila mji au watu wa nyumba moja waliogawanyika dhidi yao wenyewe hawawezi kusimama. Kama Shetani akimtoa Shetani, atakuwa amegawanyika yeye mwenyewe. Basi ufalme wake utawezaje kusimama? Nami kama natoa pepo wachafu kwa nguvu za Beelzebuli, watu wenu je, wao hutoa pepo wachafu kwa uwezo wa nani? Hivyo basi, wao ndio watakaowahukumu. Lakini kama mimi ninatoa pepo wachafu kwa Roho wa Mungu, basi Ufalme wa Mungu umekuja juu yenu. “Au tena, mtu awezaje kuingia katika nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali zake asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Akishamfunga, ndipo hakika anaweza kuteka nyara mali zake. “Mtu asiyekuwa pamoja nami yu kinyume nami, na mtu ambaye hakusanyi pamoja nami, hutawanya. Kwa hiyo nawaambia, kila dhambi na kufuru watu watasamehewa, lakini mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa. Mtu yeyote atakayesema neno dhidi ya Mwana wa Adamu atasamehewa, lakini yeyote anenaye neno dhidi ya Roho Mtakatifu hatasamehewa, iwe katika ulimwengu huu au katika ulimwengu ujao. “Ufanye mti kuwa mzuri, nayo matunda yake yatakuwa mazuri. Au ufanye mti kuwa mbaya, na matunda yake yatakuwa mabaya. Kwa maana mti hutambulika kwa matunda yake. Enyi uzao wa nyoka! Mnawezaje kunena mambo mema, wakati ninyi ni waovu? Kwa maana kinywa cha mtu huyanena yale yaliyoujaza moyo wake. Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka hazina ya mambo mema yaliyohifadhiwa ndani yake, naye mtu mwovu hutoa yaliyo maovu kutoka hazina ya mambo maovu yaliyohifadhiwa ndani yake. Lakini nawaambia, katika siku ya hukumu watu watatoa hesabu kuhusu kila neno lisilo maana walilonena. Kwa maana kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.”