Luka 22:31-53
Luka 22:31-53 SRUV
Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isipungue; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako. Akamwambia, Bwana, niwapo pamoja nawe, mimi ni tayari kwenda gerezani au hata kifoni. Akasema, Nakuambia, Petro, jogoo hatawika leo, kabla wewe hujanikana mara tatu ya kuwa hunijui. Akawauliza, Je! Hapo nilipowatuma hamna mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu? Wakasema, La! Akawaambia, Lakini sasa mwenye mfuko na auchukue, na mkoba vivyo hivyo; naye asiye na upanga, na auze joho lake akanunue. Kwa kuwa nawaambia, hayo yaliyoandikwa hayana budi kutimizwa kwangu; ya kuwa, Alihesabiwa pamoja na wahalifu. Kwa sababu yanipasayo yanao mwisho wake. Wakasema, Bwana, tazama, hapa pana panga mbili. Akawaambia, Basi. Akatoka akaenda mpaka mlima wa Mizeituni kama ilivyokuwa desturi yake; wanafunzi wake nao wakafuatana naye. Alipofika mahali pale aliwaambia, Ombeni kwamba msiingie majaribuni. Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; lakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke. [ Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu. Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; jasho yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini.] Alipoondoka katika kuomba kwake, akawajia wanafunzi wake, akawakuta wamelala usingizi kwa huzuni. Akawaambia, Mbona mmelala usingizi? Ondokeni, mkaombe, msije mkaingia majaribuni. Basi alipokuwa katika kusema, tazama, mkutano wa watu, na yule aitwaye Yuda, ambaye ni mmoja wa wale Kumi na Wawili, amewatangulia. Akamkaribia Yesu ili kumbusu. Yesu akamwambia, Yuda, wamsaliti Mwana wa Adamu kwa kumbusu? Na wale waliokuwa karibu naye walipoona yatakayotokea, walisema, Bwana, tuwapige kwa upanga? Mmoja wao akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kulia. Yesu akajibu akasema, Muwe radhi kwa hili. Akamgusa sikio, akamponya. Yesu akawaambia wakuu wa makuhani, na maofisa wa hekalu, na wazee, waliokuja juu yake, Je! Mmekuja mkiwa na panga na marungu kama kukamata mnyang'anyi? Kila siku nilipokuwa pamoja nanyi hekaluni hamkuninyoshea mikono, lakini hii ndiyo saa yenu, na mamlaka ya giza.