Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 22:31-53

Luka 22:31-53 NENO

Isa akasema, “Simoni, Simoni, sikiliza, Shetani ameomba kuwapepeta ninyi wote kama ngano. Lakini nimekuombea wewe Simoni ili imani yako isishindwe, nawe baada ya kunirudia, uwaimarishe ndugu zako.” Petro akajibu, “Bwana, niko tayari kwenda pamoja nawe gerezani na hata katika kifo.” Isa akamjibu, “Ninakuambia Petro, kabla jogoo hajawika usiku wa leo, utakana mara tatu kwamba unanijua.” Kisha Isa akawauliza, “Nilipowatuma bila mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu chochote?” Wakajibu, “La, hatukupungukiwa na kitu chochote.” Akawaambia, “Lakini sasa, aliye na mfuko na auchukue, na aliye na mkoba vivyo hivyo. Naye asiye na upanga, auze joho lake anunue mmoja. Kwa sababu, nawaambia, andiko hili lazima litimizwe kunihusu, kwamba, ‘Alihesabiwa pamoja na wakosaji’; kwa kweli yaliyoandikwa kunihusu hayana budi kutimizwa.” Wanafunzi wake wakamwambia, “Bwana, tazama hapa kuna panga mbili.” Akawajibu, “Inatosha.” Isa akatoka, akaenda kwenye Mlima wa Mizeituni kama ilivyokuwa kawaida yake, nao wanafunzi wake wakamfuata. Walipofika huko, akawaambia wanafunzi wake, “Ombeni, msije mkaingia majaribuni.” Akajitenga nao kama umbali wa kutupa jiwe, akapiga magoti, akaomba akisema, “Baba, kama ni mapenzi yako, niondolee kikombe hiki. Lakini si kama nipendavyo, bali mapenzi yako yatendeke.” Malaika kutoka mbinguni akamtokea, akamtia nguvu. Naye akiwa katika maumivu makuu, akaomba kwa bidii, nalo jasho lake likawa kama matone ya damu yakidondoka ardhini. Baada ya kuomba, akawarudia wanafunzi wake akawakuta wamelala, wakiwa wamechoka kutokana na huzuni. Naye akawauliza, “Mbona mmelala? Amkeni, mwombe ili msije mkaingia majaribuni.” Isa alipokuwa bado anazungumza, umati mkubwa wa watu wakaja. Waliongozwa na Yuda, aliyekuwa mmoja wa wale kumi na wawili. Akamkaribia Isa ili ambusu. Lakini Isa akamwambia, “Yuda, je, unamsaliti Mwana wa Adamu kwa busu?” Wafuasi wa Isa walipoona yale yaliyokuwa yanakaribia kutokea, wakasema, “Bwana, tuwakatekate kwa panga zetu?” Mmoja wao akampiga mtumishi wa kuhani mkuu kwa upanga, akamkata sikio la kuume. Lakini Isa akasema, “Acheni!” Akaligusa lile sikio la yule mtu na kumponya. Kisha Isa akawaambia wale viongozi wa makuhani, maafisa wa walinzi wa Hekalu, pamoja na wazee waliokuwa wamekuja kumkamata, “Mmekuja na panga na marungu, kana kwamba mimi ni mnyang’anyi? Kila siku nilikuwa pamoja nanyi Hekaluni lakini hamkunikamata. Lakini hii ni saa yenu, wakati giza linatawala!”