Luka 20:9-26
Luka 20:9-26 SRUV
Akaanza kuwaambia watu mfano huu; Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu; akakondisha wakulima, akaenda akakaa katika nchi nyingine muda mrefu. Na wakati wa mavuno alituma mtumwa kwa wale wakulima ili wampe baadhi ya matunda ya mizabibu; wakulima wakampiga wakamfukuza mikono mitupu. Akatuma na mtumwa mwingine. Wakampiga huyu naye, wakamwaibisha wakamfukuza mikono mitupu. Akamtuma na wa tatu; huyu naye wakamtia jeraha, wakamtupa nje. Basi, bwana wa shamba la mizabibu alisema, Nifanyeje? Nitamtuma mwanangu, mpendwa wangu; yamkini watamheshimu yeye. Lakini, wale wakulima walipomwona, walishauriana wao kwa wao, wakisema, Huyu ndiye mrithi; haya, na tumwue, ili urithi uwe wetu. Wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi, bwana wa shamba la mizabibu atawatendaje? Atakuja na kuwaangamiza wakulima wale, na lile shamba la mizabibu atawapa wengine. Waliposikia hayo walisema, Hasha! Yasitukie haya! Akawakazia macho akasema, Maana yake nini basi neno hili lililoandikwa, Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni? Kila mtu aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjikavunjika; na yeyote ambaye litamwangukia litamsaga kabisa. Nao waandishi na wakuu wa makuhani walitaka kumkamata saa iyo hiyo, wakawaogopa watu, maana walitambua ya kwamba mfano huu amewanenea wao. Wakamviziavizia, wakatuma wapelelezi waliojifanya kuwa watu wa haki, ili wamnase katika maneno yake, wapate kumtia katika enzi na mamlaka ya mtawala. Wakamwuliza, wakisema, Mwalimu, twajua ya kwamba wasema na kufundisha yaliyo ya haki, wala hujali cheo cha mtu, bali unafundisha njia ya Mungu kwa kweli. Je! Ni halali tumpe Kaisari kodi, au sivyo? Lakini yeye alitambua hila yao, akawaambia, Nionesheni dinari. Ina sura na anwani ya nani? Wakamjibu, Ya Kaisari. Akawaambia, Basi, vya Kaisari mpeni Kaisari, na vya Mungu mpeni Mungu. Wala hawakuweza kumshitaki kwa maneno yake mbele ya watu; wakastaajabia majibu yake, wakanyamaza.