Luka 20:9-26
Luka 20:9-26 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu akaendelea kuwaambia watu mfano huu: “Mtu mmoja alilima shamba la mizabibu, akalikodisha kwa wakulima; kisha akasafiri hadi nchi ya mbali, akakaa huko kwa muda mrefu. Wakati wa mavuno, mtu huyo alimtuma mtumishi wake kwa wale wakulima, akachukue sehemu ya matunda ya shamba la mizabibu. Lakini wale wakulima wakampiga mtumishi huyo, wakamrudisha mikono mitupu. Yule bwana akamtuma tena mtumishi mwingine; lakini wao wakampiga huyo vilevile na kumtendea vibaya, wakamrudisha mikono mitupu. Akamtuma tena wa tatu; huyu naye, baada ya kumwumiza, wakamfukuza. Yule mwenye shamba akafikiri: ‘Nitafanya nini? Nitamtuma mwanangu mpenzi; labda watamjali yeye.’ Wale wakulima walipomwona tu, wakasemezana: ‘Huyu ndiye mrithi. Basi, tumuue ili urithi wake uwe wetu.’ Basi, wakamtoa nje ya lile shamba la mizabibu, wakamuua.” Yesu akauliza, “Yule mwenye shamba atawafanya nini hao wakulima? Atakuja kuwaangamiza wakulima hao, na kuwapa wakulima wengine hilo shamba la mizabibu.” Watu waliposikia maneno hayo, walisema: “Hasha! Yasitukie hata kidogo!” Lakini Yesu akawatazama, akawaambia, “Maandiko haya Matakatifu yana maana gani, basi? ‘Jiwe walilokataa waashi, sasa limekuwa jiwe kuu la msingi!’ Mtu yeyote akianguka juu ya jiwe hilo atavunjika vipandevipande; na likimwangukia mtu yeyote, litamponda.” Waalimu wa sheria na makuhani wakuu walifahamu kwamba mfano huo ulikuwa unawahusu, na hivyo walitaka kumkamata palepale, ila tu waliogopa watu. Basi, wakawa wanatafuta wakati wa kufaa. Wakawahonga watu fulani wajisingizie kuwa wema, wakawatuma wamnase Yesu kwa maswali, na hivyo waweze kumtia nguvuni na kumpeleka kwa wakuu wa serikali. Hao wapelelezi wakamwambia, “Mwalimu, tunajua kwamba unasema na kufundisha mambo ya kweli; tunajua kwamba wewe huna ubaguzi; wewe wafundisha ukweli juu ya njia ya Mungu. Basi, tuambie kama ni halali au la, kulipa kodi kwa Kaisari!” Yesu alitambua mtego wao, akawaambia, “Nionesheni sarafu. Je, sura na chapa ni vya nani?” Nao wakamjibu, “Ni ya Kaisari.” Yesu akawaambia, “Basi, ya Kaisari mpeni Kaisari, na ya Mungu mpeni Mungu.” Hawakufaulu kumnasa kwa neno lolote pale mbele ya watu na hivyo wakakaa kimya wakilistaajabia jibu lake.
Luka 20:9-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akaanza kuwaambia watu mfano huu; Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu; akakondisha wakulima, akaenda akakaa katika nchi nyingine muda mrefu. Na wakati wa mavuno alituma mtumwa kwa wale wakulima ili wampe baadhi ya matunda ya mizabibu; wakulima wakampiga wakamfukuza mikono mitupu. Akatuma na mtumwa mwingine. Wakampiga huyu naye, wakamwaibisha wakamfukuza mikono mitupu. Akamtuma na wa tatu; huyu naye wakamtia jeraha, wakamtupa nje. Basi, bwana wa shamba la mizabibu alisema, Nifanyeje? Nitamtuma mwanangu, mpendwa wangu; yamkini watamheshimu yeye. Lakini, wale wakulima walipomwona, walishauriana wao kwa wao, wakisema, Huyu ndiye mrithi; haya, na tumwue, ili urithi uwe wetu. Wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi, bwana wa shamba la mizabibu atawatendaje? Atakuja na kuwaangamiza wakulima wale, na lile shamba la mizabibu atawapa wengine. Waliposikia hayo walisema, Hasha! Yasitukie haya! Akawakazia macho akasema, Maana yake nini basi neno hili lililoandikwa, Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni? Kila mtu aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjikavunjika; na yeyote ambaye litamwangukia litamsaga kabisa. Nao waandishi na wakuu wa makuhani walitaka kumkamata saa iyo hiyo, wakawaogopa watu, maana walitambua ya kwamba mfano huu amewanenea wao. Wakamviziavizia, wakatuma wapelelezi waliojifanya kuwa watu wa haki, ili wamnase katika maneno yake, wapate kumtia katika enzi na mamlaka ya mtawala. Wakamwuliza, wakisema, Mwalimu, twajua ya kwamba wasema na kufundisha yaliyo ya haki, wala hujali cheo cha mtu, bali unafundisha njia ya Mungu kwa kweli. Je! Ni halali tumpe Kaisari kodi, au sivyo? Lakini yeye alitambua hila yao, akawaambia, Nionesheni dinari. Ina sura na anwani ya nani? Wakamjibu, Ya Kaisari. Akawaambia, Basi, vya Kaisari mpeni Kaisari, na vya Mungu mpeni Mungu. Wala hawakuweza kumshitaki kwa maneno yake mbele ya watu; wakastaajabia majibu yake, wakanyamaza.
Luka 20:9-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akaanza kuwaambia watu mfano huu; Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu; akapangisha wakulima, akaenda akakaa katika nchi nyingine muda mrefu. Na wakati wa mavuno alituma mtumwa kwa wale wakulima ili wampe baadhi ya matunda ya mizabibu; wakulima wakampiga wakamfukuza mikono mitupu. Akatuma na mtumwa mwingine. Wakampiga huyu naye, wakamwaibisha wakamfukuza mikono mitupu. Akamtuma na wa tatu; huyu naye wakamtia jeraha, wakamtupa nje. Basi, bwana wa shamba la mizabibu alisema, Nifanyeje? Nitamtuma mwanangu, mpendwa wangu; yamkini watamheshimu yeye. Lakini, wale wakulima walipomwona, walishauriana wao kwa wao, wakisema, Huyu ndiye mrithi; haya, na tumwue, ili urithi uwe wetu. Wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi, bwana wa shamba la mizabibu atawatendeje? Atakuja na kuwaangamiza wakulima wale, na lile shamba la mizabibu atawapa wengine. Waliposikia hayo walisema, Hasha! Yasitukie haya! Akawakazia macho akasema, Maana yake nini basi neno hili lililoandikwa, Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni? Kila mtu aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika-vunjika; na ye yote ambaye litamwangukia litamsaga kabisa. Nao waandishi na wakuu wa makuhani walitafuta kumkamata saa iyo hiyo, wakawaogopa watu, maana walitambua ya kwamba mfano huu amewanenea wao. Wakamvizia-vizia, wakatuma wapelelezi waliojifanya kuwa watu wa haki, ili wamnase katika maneno yake, wapate kumtia katika enzi na mamlaka ya liwali. Wakamwuliza, wakisema, Mwalimu, twajua ya kwamba wasema na kufundisha yaliyo ya haki, wala hujali cheo cha mtu, bali unafundisha njia ya Mungu kwa kweli. Je! Ni halali tumpe Kaisari kodi, au sivyo? Lakini yeye alitambua hila yao, akawaambia, Nionyesheni dinari. Ina sura na anwani ya nani? Wakamjibu, Ya Kaisari. Akawaambia, Basi, vya Kaisari mpeni Kaisari, na vya Mungu mpeni Mungu. Wala hawakuweza kumshitaki kwa maneno yake mbele ya watu; wakastaajabia majibu yake, wakanyamaa.
Luka 20:9-26 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Akaendelea kuwaambia watu mfano huu: “Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu, akalikodisha kwa wakulima fulani, kisha akasafiri kwa muda mrefu. Wakati wa mavuno ulipofika, akamtuma mtumishi wake kwa hao wapangaji ili wampe sehemu ya mavuno ya shamba la mizabibu. Lakini wale wakulima wakampiga, wakamfukuza mikono mitupu. Akamtuma mtumishi mwingine, huyo naye wakampiga, wakamfanyia mambo ya aibu na kumfukuza. Bado akamtuma na mwingine wa tatu, huyu pia wakamjeruhi na kumtupa nje ya shamba. “Basi yule mwenye shamba la mizabibu akasema, ‘Nifanye nini? Nitamtuma mwanangu mpendwa, huenda yeye watamheshimu.’ “Lakini wale wapangaji walipomwona, wakasemezana wao kwa wao. Wakasema, ‘Huyu ndiye mrithi. Basi na tumuue ili urithi uwe wetu.’ Kwa hiyo wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamuua.” “Sasa basi yule mwenye shamba la mizabibu atawafanyia nini wapangaji hawa? Atakuja na kuwaua hao wapangaji, na kuwapa wapangaji wengine hilo shamba la mizabibu.” Watu waliposikia hayo wakasema, “Mungu apishie mbali jambo hili lisitokee!” Lakini Yesu akawakazia macho, akasema, “Basi ni nini maana ya yale yaliyoandikwa: “ ‘Jiwe walilolikataa waashi, limekuwa jiwe kuu la pembeni’? Kila mtu aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika vipande vipande, lakini yule litakayemwangukia atasagwa kabisa.” Walimu wa sheria na viongozi wa makuhani wakatafuta njia ya kumkamata mara moja, kwa sababu walifahamu kwamba amesema mfano huo kwa ajili yao. Lakini waliwaogopa watu. Kwa hiyo wakawa wanamchunguza na kutuma wapelelezi waliojifanya kuwa wenye haki ili wapate kumtega kwa maneno asemayo, ili wamtie katika uwezo na mamlaka ya mtawala. Hivyo wale wapelelezi wakamuuliza, “Mwalimu, tunajua unasema na kufundisha yaliyo kweli wala humpendelei mtu, bali wafundisha njia ya Mungu katika kweli. Je, ni halali sisi kulipa kodi kwa Kaisari, au la?” Lakini Yesu akatambua hila yao, kwa hiyo akawaambia, “Nionyesheni dinari. Je, sura hii na maandishi haya yaliyoko juu yake ni vya nani?” Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.” Akawaambia, “Basi mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.” Wakashindwa kumkamata kwa yale aliyokuwa amesema hadharani. Nao wakashangazwa mno na majibu yake, wakanyamaza kimya.