Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 2:1-35

Luka 2:1-35 SRUV

Siku zile amri ilitoka kwa Kaisari Augusto ya kwamba iandikwe orodha ya majina ya watu wote wa ulimwengu. Orodha hii ndiyo ya kwanza iliyoandikwa hapo Kirenio alipokuwa mtawala wa Shamu. Watu wote wakaenda kuandikwa, kila mtu mjini kwao. Yusufu naye aliondoka Galilaya, toka mji wa Nazareti, akapanda kwenda Yudea mpaka katika mji wa Daudi, uitwao Bethlehemu, kwa kuwa yeye ni wa ukoo na jamaa ya Daudi; ili aandikwe pamoja na Mariamu mkewe, ambaye amemposa, naye ana mimba. Ikawa, katika kukaa huko, siku zake za kuzaa zikatimia, akamzaa mwanawe, kifungua mimba, akamvika nguo za kitoto, akamlaza katika hori ya kulia ng'ombe, kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni. Na katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku. Malaika wa Bwana akawatokea ghafla, utukufu wa Bwana ukawang'aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu. Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng'ombe. Mara walikuwapo pamoja na huyo malaika, wingi wa jeshi la mbinguni, wakimsifu Mungu, na kusema, Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia. Ikawa, malaika hao walipoondoka kwenda zao mbinguni, wale wachungaji waliambiana, Haya, na twendeni mpaka Bethlehemu, tukalione hilo lililofanyika, alilotujulisha Bwana. Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini. Walipomwona wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto. Wote waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji. Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake. Wale wachungaji wakarudi, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona, kama walivyoambiwa. Hata zilipotumia siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu; kama alivyoitwa na malaika kabla hajachukuliwa mimba. Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo Torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto wa kiume aliye kifungua mimba wa mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana), wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili. Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi.

Soma Luka 2

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Luka 2:1-35