Luka 17:1-10
Luka 17:1-10 SRUV
Akawaambia wanafunzi wake, Vikwazo havina budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye vinakuja kwa sababu yake! Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusagia lifungwe shingoni mwake, akatupwe baharini, kuliko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hawa. Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe. Na kama akikukosea mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe. Mitume wakamwambia Bwana, Tuongezee imani. Bwana akasema, Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng'oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii. Lakini, ni nani kwenu mwenye mtumwa alimaye au achungaye ng'ombe, atakayemwambia mara arudipo kutoka shambani, Njoo upesi, keti, ule chakula? Je! Hatamwambia, Nitayarishie chakula, nile; jifunge unitumikie, hata niishe kula na kunywa, ndipo nawe utakapokula na kunywa? Je! Atampa asante yule mtumwa, kwa sababu ameyafanya aliyoagizwa? Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya.