Luka 17:1-10
Luka 17:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha, Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Haiwezekani kabisa kusitokee vikwazo vinavyosababisha dhambi; lakini ole wake mtu yule atakayevisababisha. Ingekuwa afadhali kwake kufungiwa shingoni jiwe kubwa la kusagia na kutoswa baharini, kuliko kumkwaza mmoja wa wadogo hawa. Jihadharini! Kama ndugu yako akikukosea, muonye; akitubu, msamehe. Na kama akikukosea mara saba kwa siku, na kila mara akarudi kwako akisema, ‘Nimetubu,’ lazima umsamehe.” Mitume wakamwambia Bwana, “Utuongezee imani.” Naye Bwana akajibu, “Kama imani yenu ingekuwa ndogo hata kama chembe ndogo ya haradali, mngeweza kuuambia mti huu wa mkuyu: ‘Ngoka ukajipandikize baharini,’ nao ungewatii. “Tuseme mmoja wenu ana mtumishi ambaye analima shambani au anachunga kondoo. Je, anaporudi kutoka shambani, atamwambia huyo mtumishi: ‘Haraka, njoo ule chakula?’ La! Atamwambia: ‘Nitayarishie chakula, ujifunge tayari kunitumikia mpaka nitakapomaliza kula na kunywa, ndipo nawe ule na kunywa.’ Je, utamshukuru huyo mtumishi kwa sababu ametimiza aliyoamriwa? Hali kadhalika na nyinyi mkisha fanya yote mliyoamriwa, semeni: ‘Sisi ni watumishi tusio na faida, tumetimiza tu yale tuliyotakiwa kufanya.’”
Luka 17:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akawaambia wanafunzi wake, Vikwazo havina budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye vinakuja kwa sababu yake! Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusagia lifungwe shingoni mwake, akatupwe baharini, kuliko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hawa. Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe. Na kama akikukosea mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe. Mitume wakamwambia Bwana, Tuongezee imani. Bwana akasema, Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng'oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii. Lakini, ni nani kwenu mwenye mtumwa alimaye au achungaye ng'ombe, atakayemwambia mara arudipo kutoka shambani, Njoo upesi, keti, ule chakula? Je! Hatamwambia, Nitayarishie chakula, nile; jifunge unitumikie, hata niishe kula na kunywa, ndipo nawe utakapokula na kunywa? Je! Atampa asante yule mtumwa, kwa sababu ameyafanya aliyoagizwa? Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya.
Luka 17:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akawaambia wanafunzi wake, Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake! Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusagia lifungwe shingoni mwake, akatupwe baharini, kuliko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hawa. Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe. Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe. Mitume wakamwambia Bwana, Tuongezee imani. Bwana akasema, Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng’oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii. Lakini, ni nani kwenu mwenye mtumwa alimaye au achungaye ng’ombe, atakayemwambia mara arudipo kutoka shambani, Njoo upesi, keti, ule chakula? Je! Hatamwambia, Nifanyie tayari chakula, nile; jifunge unitumikie, hata niishe kula na kunywa, ndipo nawe utakapokula na kunywa? Je! Atampa asante yule mtumwa, kwa sababu ameyafanya aliyoagizwa? Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya.
Luka 17:1-10 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Isa akawaambia wanafunzi wake, “Mambo yanayosababisha watu watende dhambi hayana budi kutukia. Lakini ole wake mtu yule anayeyasababisha. Ingekuwa heri kama mtu huyo angefungiwa jiwe la kusagia shingoni na kutoswa baharini, kuliko kumsababisha mmoja wa hawa wadogo kutenda dhambi. Kwa hiyo, jilindeni. “Ndugu yako akikukosea, mwonye; naye akitubu, msamehe. Akikukosea mara saba kwa siku moja, na mara saba kwa siku moja akaja kwako akisema, ‘Ninatubu,’ msamehe.” Mitume wake wakamwambia Bwana, “Tuongezee imani.” Bwana akawajibu, “Kama mngekuwa na imani ndogo kama punje ya haradali, mngeweza kuuambia mti huu wa mkuyu, ‘Ng’oka ukaote baharini,’ nao ungewatii. “Ikiwa mmoja wenu ana mtumishi anayelima shambani au anayechunga kondoo, je, mtumishi huyo arudipo atamwambia, ‘Karibu hapa keti ule chakula’? Je, badala yake, hatamwambia, ‘Niandalie chakula, nile, jifunge unitumikie ninapokula na kunywa; baadaye unaweza kula na kunywa’? Je, huyo mtu atamshukuru mtumishi huyo kwa kutimiza yale aliyoamriwa? Vivyo hivyo nanyi mkishafanya mliyoagizwa, semeni, ‘Sisi tu watumishi tusiostahili; tumefanya tu yale tuliyopaswa kufanya.’ ”