Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 14:15-35

Luka 14:15-35 SRUV

Basi aliposikia hayo mmojawapo wa wale walioketi chakulani pamoja naye alimwambia, Heri yule atakayekula mkate katika ufalme wa Mungu. Akamwambia, Mtu mmoja alifanya karamu kubwa akaalika watu wengi, akamtuma mtumwa wake saa ya chakula awaambie wale walioalikwa, Njooni, kwa kuwa vitu vyote vimekwisha kuwekwa tayari. Wakaanza wote kutoa udhuru kwa nia moja. Wa kwanza alimwambia, Nimenunua shamba, sharti niende nikalitazame; tafadhali unisamehe. Mwingine akasema, Nimenunua ng'ombe jozi tano, ninakwenda kuwajaribu; tafadhali unisamehe. Mwingine akasema, Nimeoa mke, na kwa sababu hiyo siwezi kuja. Yule mtumwa akaenda, akamwambia Bwana wake kuhusu mambo hayo. Basi, yule mwenye nyumba akakasirika, akamwambia mtumwa wake, Toka upesi, uende katika njia kuu na vichochoro vya mji, ukawalete hapa maskini, na vilema, na vipofu, na viwete. Mtumwa akasema, Bwana, hayo uliyoagiza yamekwisha tendeka, na hata sasa ingaliko nafasi. Bwana akamwambia mtumwa, Toka nje uende barabarani na mipakani, ukawashurutishe kuingia ndani, nyumba yangu ipate kujaa. Maana nawaambia ya kwamba katika wale walioalikwa, hakuna hata mmoja atakayeionja karamu yangu. Makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia, Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake wa kiume na wa kike; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Mtu yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, haketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza. Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, haketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini? Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akiwa bado mbali. Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Chumvi ni kitu chema; lakini chumvi ikiwa imeharibika, itiwe nini ikolee? Haiifai nchi wala jaa; watu huitupa nje. Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.

Soma Luka 14

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Luka 14:15-35

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha