Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Lk 14:15-35

Lk 14:15-35 SUV

Basi aliposikia hayo mmojawapo wa wale walioketi chakulani pamoja naye alimwambia, Heri yule atakayekula mkate katika ufalme wa Mungu. Akamwambia, Mtu mmoja alifanya karamu kubwa akaalika watu wengi, akamtuma mtumwa wake saa ya chakula awaambie wale walioalikwa, Njoni, kwa kuwa vitu vyote vimekwisha kuwekwa tayari. Wakaanza wote kutoa udhuru kwa nia moja. Wa kwanza alimwambia, Nimenunua shamba, sharti niende nikalitazame; tafadhali unisamehe. Mwingine akasema, Nimenunua ng’ombe jozi tano, ninakwenda kuwajaribu; tafadhali unisamehe. Mwingine akasema, Nimeoa mke, na kwa sababu hiyo siwezi kuja. Yule mtumwa akaenda, akampa bwana wake habari ya mambo hayo. Basi, yule mwenye nyumba akakasirika, akamwambia mtumwa wake, Toka upesi, uende katika njia kuu na vichochoro vya mji, ukawalete hapa maskini, na vilema, na vipofu, na viwete. Mtumwa akasema, Bwana, hayo uliyoagiza yamekwisha tendeka, na hata sasa ingaliko nafasi. Bwana akamwambia mtumwa, Toka nje uende barabarani na mipakani, ukawashurutishe kuingia ndani, nyumba yangu ipate kujaa. Maana nawaambia ya kwamba katika wale walioalikwa, hapana hata mmoja atakayeionja karamu yangu. Makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia, Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza. Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini? Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali. Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Chumvi ni kitu chema; lakini chumvi ikiwa imeharibika, itiwe nini ikolee? Haiifai nchi wala jaa; watu huitupa nje. Mwenye masikio ya kusikilia, na asikie.

Soma Lk 14

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Lk 14:15-35

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha