Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 11:14-26

Luka 11:14-26 SRUV

Naye alikuwa akitoa pepo bubu; ikawa pepo alipotoka, yule bubu akanena, watu wakastaajabu. Wengine wao wakasema, Atoa pepo kwa Beelzebuli, mkuu wa pepo. Wengine walimjaribu, wakimtaka afanye ishara itokayo mbinguni. Naye akajua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme uliofitinika wenyewe kwa wenyewe hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka. Basi, ikiwa Shetani naye amefitinika juu ya nafsi yake, ufalme wake utasimamaje? Kwa kuwa ninyi mnasema kwamba mimi natoa pepo kwa Beelzebuli. Basi, kama mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, wana wenu je! Huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo, hao ndio watakaowahukumu. Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajia. Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha zake, alindapo nyumba yake, vitu vyake viko salama; lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda, amnyang'anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea, na kuyagawanya mateka yake. Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutawanya. Pepo mchafu amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika; asipoona, husema, Nitairudia nyumba yangu niliyotoka. Hata afikapo, akaiona imefagiwa na kupambwa, ndipo huenda akachukua pepo wengine saba, walio waovu kuliko yeye mwenyewe, wakaingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza.

Soma Luka 11