Luka 11:14-26
Luka 11:14-26 NEN
Basi Yesu alikuwa anamtoa pepo mchafu kutoka kwa mtu aliyekuwa bubu. Yule pepo mchafu alipomtoka yule mtu aliyekuwa bubu, akaanza kuongea, nao umati wa watu ukashangaa. Lakini wengine wakasema, “Anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebuli, yule mkuu wa pepo wachafu wote.” Wengine ili kumjaribu wakataka awaonyeshe ishara kutoka mbinguni. Yesu akajua mawazo yao, naye akawaambia, “Kila ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe huangamia. Nayo nyumba iliyogawanyika dhidi yake yenyewe itaanguka. Kama Shetani amegawanyika mwenyewe, ufalme wake utasimamaje? Nawaambia haya kwa sababu ninyi mnadai ya kuwa mimi ninatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebuli. Kama mimi natoa pepo wachafu kwa nguvu za Beelzebuli, wafuasi wenu nao je, wao hutoa pepo wachafu kwa uwezo wa nani? Hivyo basi, wao ndio watakaowahukumu. Lakini kama mimi ninatoa pepo wachafu kwa kidole cha Mungu, basi Ufalme wa Mungu umewajia. “Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha anapoilinda nyumba yake, mali yake iko salama. Lakini mtu mwenye nguvu zaidi kumliko akimshambulia na kumshinda, yeye humnyangʼanya silaha zake zote alizozitegemea, na kuchukua nyara. “Mtu asiyekuwa pamoja nami yu kinyume nami, na mtu ambaye hakusanyi pamoja nami, hutawanya. “Pepo mchafu amtokapo mtu, hutangatanga katika sehemu zisizo na maji akitafuta mahali pa kupumzika, lakini hapati. Ndipo husema, ‘Nitarudi kwenye nyumba yangu nilikotoka.’ Naye arudipo na kuikuta ile nyumba imefagiliwa na kupangwa vizuri, ndipo huenda na kuchukua pepo wachafu wengine saba wabaya kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo. Nayo hali ya mwisho ya yule mtu huwa ni mbaya kuliko ile ya kwanza.”