Mambo ya Walawi 24:1-9
Mambo ya Walawi 24:1-9 SRUV
Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Waagize wana wa Israeli wakuletee mafuta ya zeituni safi ya kupondwa kwa ajili ya ile nuru, ili hiyo taa iwake daima. Hapo nje ya pazia la ushahidi, ndani ya hema ya kukutania, Haruni ataitengeneza tangu jioni hadi asubuhi mbele za BWANA daima; ni amri ya milele katika vizazi vyenu. Atazitengeneza hizo taa katika kile kinara kilicho safi mbele za BWANA daima. Nawe utatwaa unga mwembamba, na kuoka mikate kumi na miwili ya huo unga; sehemu za kumi mbili za efa, zitakuwa katika mkate mmoja. Nawe iweke mistari miwili, mikate sita kwa kila mstari, juu ya hiyo meza safi, mbele za BWANA. Nawe utatia ubani safi juu ya kila mstari, ili uwe ukumbusho kwa hiyo mikate, sadaka ya kusongezwa kwa BWANA kwa moto. Kila siku ya Sabato ataipanga mbele za BWANA daima; ni kwa ajili ya wana wa Israeli, agano la milele. Nayo itakuwa ya Haruni na wanawe; nao wataila katika mahali patakatifu; kwa sababu kwake ni takatifu sana katika sadaka zitolewazo kwa BWANA kwa moto, kwa amri ya milele.