Yoshua 24:19-33
Yoshua 24:19-33 SRUV
Yoshua akawaambia watu, Hamwezi kumtumikia BWANA; kwa kuwa yeye ni Mungu mtakatifu; yeye ni Mungu mwenye wivu; hatawasamehe makosa yenu, wala dhambi zenu. Kama mkimwacha BWANA na kuitumikia miungu migeni, ndipo atageuka na kuwatenda mabaya na kuwaangamiza, baada ya kuwatendea mema. Lakini hao watu wakamwambia Yoshua, La! Lakini tutamtumikia BWANA. Yoshua akawaambia watu, Ninyi mmekuwa mashahidi juu ya nafsi zenu, ya kuwa mmemchagua BWANA, ili kumtumikia yeye. Wakasema, Sisi tu mashahidi. Akasema, Basi sasa, iondoeni miungu migeni iliyo kati yenu, mkaielekeze mioyo yenu kwa BWANA, Mungu wa Israeli. Ndipo hao watu wakamwambia Yoshua, BWANA, Mungu wetu, ndiye tutakayemtumikia; na sauti yake ndiyo tutakayoitii. Basi Yoshua akafanya agano na wale watu siku ile, akawapa amri na agizo huko Shekemu. Yoshua akayaandika maneno haya katika kitabu cha Torati ya Mungu; kisha akatwaa jiwe kubwa, akalisimamisha huko, chini ya ule mwaloni uliokuwa karibu na patakatifu pa BWANA. Yoshua akawaambia watu wote, Tazama, jiwe hili litakuwa shahidi juu yetu; kwa maana limesikia maneno yote ya BWANA aliyotuambia, basi litakuwa shahidi juu yenu, msije mkamkana Mungu wenu. Basi Yoshua akawaruhusu watu, wakaenda zao, kila mtu kwenye urithi wake. Ikawa, baada ya hayo, Yoshua, mwana wa Nuni, mtumishi wa BWANA, akafa, mwenye umri wa miaka mia moja na kumi. Wakamzika katika nchi ya urithi wake, huko Timnath-sera; ulio katika nchi ya vilima ya Efraimu, upande wa kaskazini wa mlima wa Gaashi. Nao Israeli wakamtumikia BWANA siku zote za Yoshua, na siku zote za hao wazee walioishi baada ya kufa kwake Yoshua, hao walioijua kazi yote ya BWANA, aliyowatendea Israeli. Na hiyo mifupa ya Yusufu, ambayo wana wa Israeli walikuwa wameileta kutoka Misri, wakaizika huko Shekemu katika ile sehemu ya nchi, Yakobo aliyoinunua kwa wana wa Hamori, babaye Shekemu, kwa vipande mia moja vya fedha; nayo ikawa ni urithi wa wana wa Yusufu. Huyo Eleazari mwana wa Haruni naye akafa; wakamzika Gibea, mji wa Finehasi mwanawe, ambao alipewa katika nchi ya vilima ya Efraimu.