Ayubu 31:1-12
Ayubu 31:1-12 SRUV
Nilifanya agano na macho yangu; Basi ningewezaje kumwangalia msichana? Kwani sehemu ya Mungu itokayo juu ingekuwa nini, Na urithi wa Mwenyezi utokao juu? Je! Siyo msiba kwa wasio haki, Na hasara kwao watendao uovu? Je! Yeye hazioni njia zangu, Na kuzihesabu hatua zangu zote? Kwamba nimetembea katika ubatili, Na mguu wangu umeukimbilia udanganyifu; (Na nipimwe katika mizani iliyo sawasawa, Ili Mungu aujue uelekevu wangu); Kwamba hatua yangu imekengeuka na kuiacha njia, Na moyo wangu kuyaandama macho yangu, Tena kwamba kipaku chochote kimeshikamana na mikono yangu; Basi na nipande, mwingine ale; Naam, mazao ya shamba langu na yang'olewe. Kama moyo wangu ulishawishwa kwa mwanamke, Nami nimeotea mlangoni pa jirani yangu; Ndipo hapo mke wangu na asage kwa mwingine, Na wengine na wainame juu yake. Kwani hilo lingekuwa kosa kuu; Naam, lingekuwa ni uovu wa kuadhibiwa na waamuzi; Kwa kuwa ni moto uteketezao hata Uharibifu, Nao ungeyang'oa mavuno yangu yote.