Ayubu 15:1-16
Ayubu 15:1-16 SRUV
Ndipo Elifazi, Mtemani, akajibu, na kusema, Je! Yapasa mtu mwenye hekima kujibu kwa ujuzi wa uvuvio, Na kulijaza tumbo lake upepo wa mashariki? Je! Ahoji na mazungumzo yasiyo na faida, Au kwa maneno ambayo hawezi kufanya mema kwayo? Naam, wewe wapuuza hofu ya Mungu, Nawe wazuia ibada mbele za Mungu. Kwani uovu wako unakufundisha kinywa chako, Nawe wachagua ulimi wake mwenye hila. Kinywa chako mwenyewe chakuhukumia makosa, wala si mimi; Naam, midomo yako mwenyewe hushuhudia juu yako. Je! Wewe u mtu wa kwanza aliyezaliwa? Au, ulizawa wewe kabla ya milima? Je! Umesikiza ushauri wa siri ya Mungu? Nawe je! Wazuia hekima iwe yako tu? Je! Wewe wajua neno lipi, ambalo sisi hatulijui? Nawe wafahamu nini, ambalo halimo ndani yetu? Wenye mvi, na walio wazee sana, wote wapo pamoja nasi, Ambao ni wazee kuliko baba yako. Je! Utulivu wa Mungu ni mdogo sana kwako, Maliwazo ya Mungu ni madogo sana kwako? Mbona moyo wako unakutaharakisha! Na macho yako, je! Kwa nini yaangae? Hata ukageuza roho yako kinyume cha Mungu, Na kuyatoa maneno kama hayo kinywani mwako. Je! Mwanadamu ni kitu gani, hata akawa safi? Huyo aliyezaliwa na mwanamke, hata awe na haki? Yeye hawategemei watakatifu wake; Naam, mbingu nazo si safi machoni pake. Sembuse mtu ambaye ni mwenye kuchukiza na uchafu, Mwanadamu anywaye uovu kama anywavyo maji!