Yobu 15:1-16
Yobu 15:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha Elifazi, Mtemani, akajibu: “Je, mtu wa hekima hujibu kwa maneno ya upuuzi? Je, mtu huyo amejaa maneno matupu? Je, mwenye hekima hujitetea kwa maneno yasiyofaa, au kwa maneno yasiyo na maana? Lakini wewe unapuuza uchaji wa Mungu; na kuzuia kutafakari mbele ya Mungu. Uovu wako ndio unaokifundisha kinywa chako, nawe wachagua kusema kama wadanganyifu. Maneno yako mwenyewe yanakuhukumu, sio mimi; matamshi yako yashuhudia dhidi yako. Je, wewe ni mtu wa kwanza kuzaliwa? Je, wewe ulizaliwa kabla ya kuweko vilima? Je, ulipata kuweko katika halmashauri ya Mungu? au, wewe ndiwe peke yako mwenye hekima? Unajua kitu gani tusichokijua sisi? Unafahamu kitu gani tusichokifahamu sisi? Miongoni mwetu wapo wazee wenye hekima, wenye miaka mingi kuliko baba yako. Je, faraja anazokupa Mungu ni ndogo mno? Au je, neno lake la upole kwako si kitu? Mbona moyo unakusukuma kukasirika na kutoa macho makali, hata kumwasi Mungu na kusema maneno mabaya kama hayo? Mtu ni nini hata aweze kuwa mwadilifu? au yule aliyezaliwa na mwanamke hata aweze kuwa mwema? Ikiwa Mungu hawaamini hata watakatifu wake, nazo mbingu si safi mbele yake, sembuse binadamu aliye kinyaa na mpotovu binadamu atendaye uovu kama kunywa maji!
Yobu 15:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo Elifazi, Mtemani, akajibu, na kusema, Je! Yapasa mtu mwenye hekima kujibu kwa ujuzi wa uvuvio, Na kulijaza tumbo lake upepo wa mashariki? Je! Ahoji na mazungumzo yasiyo na faida, Au kwa maneno ambayo hawezi kufanya mema kwayo? Naam, wewe wapuuza hofu ya Mungu, Nawe wazuia ibada mbele za Mungu. Kwani uovu wako unakufundisha kinywa chako, Nawe wachagua ulimi wake mwenye hila. Kinywa chako mwenyewe chakuhukumia makosa, wala si mimi; Naam, midomo yako mwenyewe hushuhudia juu yako. Je! Wewe u mtu wa kwanza aliyezaliwa? Au, ulizawa wewe kabla ya milima? Je! Umesikiza ushauri wa siri ya Mungu? Nawe je! Wazuia hekima iwe yako tu? Je! Wewe wajua neno lipi, ambalo sisi hatulijui? Nawe wafahamu nini, ambalo halimo ndani yetu? Wenye mvi, na walio wazee sana, wote wapo pamoja nasi, Ambao ni wazee kuliko baba yako. Je! Utulivu wa Mungu ni mdogo sana kwako, Maliwazo ya Mungu ni madogo sana kwako? Mbona moyo wako unakutaharakisha! Na macho yako, je! Kwa nini yaangae? Hata ukageuza roho yako kinyume cha Mungu, Na kuyatoa maneno kama hayo kinywani mwako. Je! Mwanadamu ni kitu gani, hata akawa safi? Huyo aliyezaliwa na mwanamke, hata awe na haki? Yeye hawategemei watakatifu wake; Naam, mbingu nazo si safi machoni pake. Sembuse mtu ambaye ni mwenye kuchukiza na uchafu, Mwanadamu anywaye uovu kama anywavyo maji!
Yobu 15:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo Elifazi, Mtemani, akajibu, na kusema, Je! Yapasa mtu mwenye hekima kujibu kwa ujuzi wa uvuvio, Na kujaza tumbo lake na upepo wa mashariki? Je! Ahoji na mazungumzo yasiyo faida, Au kwa maneno ambayo hawezi kufanya mema kwayo? Naam, wewe waondoa kicho, Nawe wazuia ibada mbele za Mungu. Kwani uovu wako unakufundisha kinywa chako, Nawe wachagua ulimi wake mwenye hila. Kinywa chako mwenyewe chakuhukumia makosa, wala si mimi; Naam, midomo yako mwenyewe hushuhudia juu yako. Je! Wewe u mtu wa kwanza aliyezaliwa? Au, ulizawa wewe kabla ya milima? Je! Umesikia mashauri ya siri ya Mungu? Nawe je! Wazuia hekima iwe yako tu? Je! Wewe wajua neno lipi, ambalo sisi hatulijui? Nawe wafahamu nini, ambalo halimo ndani yetu? Wenye mvi, na walio wazee sana, wote wapo pamoja nasi, Ambao ni wazee kuliko baba yako. Je! Utulizi wa Mungu ni mdogo sana kwako, Na hilo neno la upole si kitu kwako? Mbona moyo wako unakutaharakisha! Na macho yako, je! Kwani kung’ariza? Hata ukageuza roho yako iwe kinyume cha Mungu, Na kuyatoa maneno kama hayo kinywani mwako. Je! Mwanadamu ni kitu gani, hata akawa safi? Huyo aliyezaliwa na mwanamke, hata awe na haki? Yeye hawategemei watakatifu wake; Naam, mbingu nazo si safi machoni pake. Sembuse mtu ambaye ni mwenye kuchukiza na uchafu, Mwanadamu anywaye uovu kama anywavyo maji!
Yobu 15:1-16 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha Elifazi Mtemani akajibu: “Je, mtu mwenye hekima hujibu kwa mawazo matupu, au kujaza tumbo lake kwa upepo wenye joto wa mashariki? Je, aweza kubishana juu ya maneno yasiyofaa, kwa hotuba zisizo na maana? Lakini unadhoofisha hata uchaji wa Mungu na kuzuia ibada mbele za Mungu. Dhambi yako inasukuma kinywa chako, nawe umechagua ulimi wa hila. Kinywa chako mwenyewe kinakuhukumu, wala si changu; midomo yako mwenyewe inashuhudia dhidi yako. “Je, wewe ni mtu wa kwanza kuzaliwa? Ulizaliwa kabla ya vilima? Je, wewe husikiliza mashauri ya siri ya Mungu? Je, wewe unaizuia hekima iwe yako mwenyewe? Wewe unajua kitu gani tusichokijua sisi? Unafahamu kitu gani tusichokifahamu sisi? Wale wenye mvi na wazee wako upande wetu, watu ambao ni wazee hata kuliko baba yako. Je, faraja za Mungu hazikutoshi, au maneno yaliyosemwa kwako kwa upole si kitu? Kwa nini moyo wako unakudanganya, na kwa nini macho yako yanangʼaa, ili kwamba upate kutoa hasira yako dhidi ya Mungu, na kumwaga maneno kama hayo kutoka kinywani mwako? “Mwanadamu ni kitu gani, hata aweze kuwa safi, au yeye aliyezaliwa na mwanamke, hata aweze kuwa mwadilifu? Kama Mungu hawaamini watakatifu wake, kama hata mbingu zenyewe si safi machoni pake, sembuse mwanadamu ambaye ni mwovu na mpotovu, ambaye hunywa uovu kama anywavyo maji!