Yohana 19:1-16
Yohana 19:1-16 SRUV
Basi ndipo Pilato alipomtwaa Yesu, akampiga mijeledi. Nao askari wakasokota taji la miiba, wakamtia kichwani, wakamvika vazi la zambarau. Wakawa wakimwendea, wakisema, Salamu! Mfalme wa Wayahudi! Wakampiga makofi. Kisha Pilato akatokea tena nje, akawaambia, Mtu huyu namleta nje kwenu, mpate kufahamu ya kuwa mimi sioni hatia yoyote kwake. Ndipo Yesu alipotoka nje, naye amevaa lile taji la miiba, na lile vazi la zambarau. Pilato akawaambia, Tazama, mtu huyu! Basi wale wakuu wa makuhani na watumishi wao walipomwona, walipiga kelele wakisema, Msulubishe! Msulubishe! Pilato akawaambia, Mtwaeni ninyi basi, mkamsulubishe; kwa maana mimi sioni hatia kwake. Wayahudi wakamjibu, Sisi tunayo sheria, na kwa sheria hiyo amestahili kufa, kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu. Basi Pilato aliposikia neno hilo, akazidi kuogopa. Akaingia tena ndani ya ile Praitorio, akamwambia Yesu, Wewe umetoka wapi? Lakini Yesu hakumpa jibu lolote. Basi Pilato akamwambia, Husemi nami? Hujui ya kuwa mimi nina mamlaka ya kukufungua, nami nina mamlaka ya kukusulubisha? Yesu akamjibu, Wewe hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu, kama usingepewa kutoka juu; kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako ana dhambi iliyo kubwa zaidi. Na tangu hapo Pilato akatafuta kumfungua; lakini Wayahudi wakapiga makelele wakisema, Ukimfungua huyu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu ajifanyaye kuwa mfalme humfitini Kaisari. Basi Pilato, aliposikia maneno hayo, akamleta Yesu nje, akaketi juu ya kiti cha hukumu, mahali paitwapo Sakafu ya Mawe, au kwa Kiebrania, Gabatha. Nayo ilikuwa Maandalio ya Pasaka, yapata saa sita. Akawaambia Wayahudi, Tazama, Mfalme wenu! Basi wale wakapiga kelele, Mwondoshe! Mwondoshe! Msulubishe! Pilato akawaambia, Je! Nimsulubishe mfalme wenu! Wakuu wa makuhani wakamjibu, Sisi hatuna mfalme ila Kaisari. Basi ndipo alipomtia mikononi mwao ili asulubiwe; nao wakampokea Yesu.