Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 19:1-16

Yohana 19:1-16 NEN

Ndipo Pilato akamtoa Yesu akaamuru apigwe mijeledi. Askari wakasokota taji ya miiba, wakamvika Yesu kichwani. Wakamvalisha joho la zambarau. Wakawa wanapanda pale alipo tena na tena, wakisema, “Salamu! Mfalme wa Wayahudi!” Huku wakimpiga makofi usoni. Pilato akatoka tena nje akawaambia wale waliokusanyika, “Tazameni, namkabidhi Yesu kwenu kuwajulisha kwamba mimi sikumwona ana hatia.” Kwa hiyo Yesu akatoka nje akiwa amevaa ile taji ya miiba na lile vazi la zambarau. Pilato akawaambia, “Tazameni, huyu hapa huyo mtu!” Wale viongozi wa makuhani na maafisa walipomwona, wakapiga kelele wakisema, “Msulubishe! Msulubishe!” Pilato akawaambia, “Mchukueni ninyi mkamsulubishe, mimi sioni hatia juu yake.” Wayahudi wakamjibu, “Sisi tunayo sheria na kutokana na sheria hiyo, hana budi kufa kwa sababu yeye alijiita Mwana wa Mungu.” Pilato aliposikia haya, akaogopa zaidi. Akaingia tena ndani ya jumba la kifalme, akamuuliza Yesu, “Wewe umetoka wapi?” Lakini Yesu hakumjibu. Pilato akamwambia, “Wewe unakataa kuongea na mimi? Hujui ya kuwa nina mamlaka ya kukuachia huru au kukusulubisha?” Ndipo Yesu akamwambia, “Wewe hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu kama hungepewa kutoka juu. Kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako ana hatia ya dhambi iliyo kubwa zaidi.” Tangu wakati huo, Pilato akajitahidi kutafuta njia ya kumfungua Yesu, lakini Wayahudi wakazidi kupiga kelele wakisema, “Ukimwachia huyu mtu, wewe si rafiki wa Kaisari. Mtu yeyote anayedai kuwa mfalme anampinga Kaisari.” Pilato aliposikia maneno haya akamtoa Yesu nje tena akaketi katika kiti chake cha hukumu, mahali palipoitwa Sakafu ya Jiwe, kwa Kiebrania paliitwa Gabatha Basi ilikuwa siku ya Maandalio ya Pasaka, yapata kama saa sita hivi. Pilato akawaambia Wayahudi, “Huyu hapa mfalme wenu!” Wao wakapiga kelele, “Mwondoe! Mwondoe! Msulubishe!” Pilato akawauliza, “Je, nimsulubishe mfalme wenu?” Wale viongozi wa makuhani wakamjibu, “Sisi hatuna mfalme mwingine ila Kaisari.” Ndipo Pilato akamkabidhi Yesu kwao ili wamsulubishe.