Mwanzo 49:1-13
Mwanzo 49:1-13 SRUV
Yakobo akawaita wanawe, akasema, Kusanyikeni, ili niwaambie yatakayowapata siku zijazo. Kusanyikeni, msikie, enyi wana wa Yakobo, Msikilizeni Israeli, baba yenu. Reubeni, u mzaliwa wangu wa kwanza, Nguvu zangu, na malimbuko ya uwezo wangu. Umewapita wengine kwa ukuu na kwa nguvu. Umekuwa kama maji yavukavyo mpaka, basi nawe hutafana tena, Kwa sababu ulikipanda kitanda cha baba yako, Ukakitia unajisi; alikipandia kitanda changu. Simeoni na Lawi ni ndugu; Panga zao ni silaha za jeuri. Nafsi yangu, usiingie katika siri yao, Fahari yangu usiungane na kusanyiko lao, Maana katika ghadhabu yao walimwua mtu, Na kwa ukaidi wao walikata mshipa wa ng'ombe; Ghadhabu yao na ilaaniwe, maana ilikuwa kali, Na hasira yao, maana ilikuwa haina huruma. Nitawagawa katika Yakobo, Nitawatawanya katika Israeli. Yuda, ndugu zako watakusifu, Mkono wako utakuwa shingoni mwa adui zako. Wana wa baba yako watakuinamia. Yuda ni mwanasimba, Kutoka katika mawindo, mwanangu, umepanda; Aliinama akajilaza kama simba, Na kama simba mke; ni nani atakayemwamsha? Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, Wala mfanya sheria kati ya miguu yake, Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa watamtii. Atafunga punda wake katika mzabibu, Na mwanapunda wake katika mzabibu mzuri. Amefua nguo zake kwa mvinyo, Na mavazi yake kwa damu ya zabibu. Macho yake yatakuwa mekundu kwa mvinyo, Na meno yake yatakuwa meupe kwa maziwa. Zabuloni atakaa pwani ya bahari, Naye atakuwa kama pwani za kuegesha merikebu, Na mpaka wake utakuwa kando ya Sidoni.