Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 47:13-26

Mwanzo 47:13-26 SRUV

Baadaye hapakuwa na chakula katika nchi yote, kwa kuwa njaa ilikuwa kali sana, hata nchi ya Misri na nchi ya Kanaani zikataabika, kwa sababu ya njaa. Yusufu akakusanya fedha zote zilizoonekana katika nchi ya Misri na katika nchi ya Kanaani, kwa nafaka waliyoinunua. Yusufu akazileta zile fedha nyumbani mwa Farao. Fedha zote zilipokwisha katika nchi ya Misri na katika nchi ya Kanaani, Wamisri wote walimjia Yusufu, wakisema, Tupe sisi chakula, kwa nini tufe mbele ya macho yako? Maana fedha zetu zimekwisha. Yusufu akasema, Toeni wanyama wenu, nami nitawapa chakula badala ya wanyama wenu, kama fedha zenu zimekwisha. Wakaleta wanyama wao kwa Yusufu; Yusufu akawapa chakula kwa kubadilisha na farasi, kondoo, ng'ombe na punda, naye akawalisha chakula badala ya wanyama wao wote mwaka ule. Na mwaka ule ulipokwisha wakamjia mwaka wa pili, wakamwambia, Hatumfichi bwana wetu ya kwamba fedha zetu zimekwisha, na makundi ya wanyama ni mali ya bwana wetu, hakikusalia kitu mbele za bwana wetu, ila miili yetu na nchi zetu. Kwa nini tufe mbele ya macho yako, sisi na nchi yetu? Utununue sisi na nchi yetu kwa chakula, na sisi na nchi yetu tutakuwa watumwa wa Farao; kisha utupe mbegu, tuishi wala tusife, wala nchi yetu isipotee. Basi Yusufu akamnunulia Farao nchi yote ya Misri; maana Wamisri waliuza kila mtu shamba lake; kwa sababu njaa ilikuwa imewazidi sana, nchi ikawa mali yake Farao. Akawahamisha hao watu, akawaweka katika miji, tangu upande huu wa Misri hata upande huu. Ila nchi ya makuhani hakuinunua; maana makuhani walikuwa na posho yao kutoka kwa Farao, wakala posho yao waliyopewa na Farao. Kwa hiyo hawakuuza nchi yao. Yusufu akawaambia watu, Angalieni, nimewanunua leo, ninyi, na nchi yenu, kuwa mali ya Farao; basi mbegu zenu ni hizi, zipandeni katika nchi. Wakati wa mavuno mtampa Farao sehemu ya tano, na sehemu nne zitakaposalia zitakuwa zenu wenyewe, kuwa mbegu za nchi, na chakula chenu, na chakula chao waliomo nyumbani mwenu, na chakula cha watoto wenu. Wakasema, Umeyaokoa maisha yetu, na tuone kibali machoni pa bwana wetu, nasi tutakuwa watumwa wa Farao. Yusufu akaifanya kuwa sheria ya nchi ya Misri hata leo, ya kwamba sehemu ya tano iwe mali ya Farao. Ila nchi ya makuhani tu haikuwa mali ya Farao.

Soma Mwanzo 47

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mwanzo 47:13-26